Mhehimiwa Mhandisi Isack Kamwelwe |
Muhtasari wa Taarifa ya Mheshimiwa
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe kwenye kilele cha maadhimisho
ya siku ya Hali ya Hewa Duniani “World Meteorological Day (WMD)”, Ukumbi wa
Wizara, Dar es Salaam, 23 Machi 2019.
Ni heshima kubwa
kwangu kuwepo nanyi kwenye kilele cha maadhimisho haya ya siku ya Hali ya Hewa
Duniani “World Meteorological Day (WMD)” kwa mwaka 2019. Naipongeza Mamlaka ya
Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kuandaa maadhimisho haya. Haya ni maadhimisho
ya 69 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) mwaka 1950.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni
“Jua, Dunia, na Hali ya Hewa (The Sun, The Earth, and the Weather)”, ambayo imelenga kutoa elimu kwa jamii na kuongeza uelewa wa sayansi ya hali ya
hewa, hususan maandalizi, usambazaji na matumizi ya taarifa za hali ya hewa.
Siku ya Hali ya Hewa Duniani ni muhimu sana kwani inatupa
nafasi ya kutafakari mchango wa Tanzania, kama mwanachama wa WMO katika utoaji
wa huduma za hali ya hewa hapa Tanzania na ulimwenguni kote.
Kwa upande wa Tanzania, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
ndiyo taasisi iliyopewa jukumu la kusimamia na kutoa huduma za hali ya hewa
katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa minajili hii Serikali yetu
inaendelea kuwekeza katika kuimarisha huduma za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na
kuimarisha miundombinu ya uangazi, kwa mfano ununuzi wa RADAR na vifaa vingine
vya hali ya hewa ambavyo ni kipaumbele kama ilivyolekezwa katika Mpando wa
Maendeleo wa Miaka Mitano wa Taifa
(2016/2017-2020/2021) chini ya Serikali ya awamu ya Tano. Mpaka
sasa Serikali tayari imenunua RADAR mbili za hali ya hewa ambazo zimewekwa Dar
es Salaam na Mwanza. RADAR nyingine tatu zinatarajiwa kuwekwa Mtwara, Mbeya na
Kigoma na ziko katika hatua za ununuzi.
Ni dhahiri kwamba huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Hali
ya Hewa Tanzania zimeendelea kuongezeka viwango vya ubora ikiwa ni pamoja na
usahihi wa utabiri na hivyo zinafaa kutumika katika sekta mbali mbali za
maendeleo hapa nchini. Ninatoa wito kwa wadau wote wa hali ya hewa kutoka sekta
zote za kiuchumi na kijamii na wananchi kwa ujumla kuendelea kufuatilia na
kutumia huduma za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
kwa ajili ya kupanga na kufanya maamuzi katika shughuli za kiuchumi na kijamii
kwa ajili ya ustawi wa Taifa letu.
Serikali imeendelea kuwekeza katika kuboresha huduma za
hali ya hewa kwa matumizi ya sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya usafiri wa anga,
ambapo katika mwaka 2019 Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi tatu barani Afrika
zilizopata cheti cha ubora wa huduma za hali ya hewa katika usafiri na usalama
wa anga (ISO 9001:2015) kwa mujibu wa Shirika la Viwango Duniani (ISO). Katika
kuboresha usambazaji wa huduma za hali ya hewa, TMA imebuni mfumo wa kusambaza
taarifa za hali ya hewa kwa njia ya simu za mkononi uitwao FarmSMS ambao umerahisisha
upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa kwa wadau.
Haya ni mafanikio makubwa katika kutekeleza mkataba wa Shirika
la Hali ya Hewa Duniani na kauli mbiu ya siku ya hali ya hewa Duniani ya mwaka
huu. Pamoja na mafanikio haya, bado kuna changamoto nyingi zikiwemo gharama
kubwa za vifaa vya hali ya hewa, kuendana na mabadiliko ya kukua kwa teknolojia
katika tasnia ya hali ya hewa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi
(Climate Change). Utatuzi wa changamoto hizi unahitaji jitihada za pamoja za
wadau mbalimbali.
Hivyo napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa wadau
mbalimbali wa huduma za hali ya hewa kushirikiana na Serikali katika kutekeleza
Programu ya Kitaifa ya Huduma za Hali ya Hewa (National Framework for Climate
Servives), ambayo ni mwongozo muhimu katika utoaji na utumiaji wa huduma za
hali ya hewa hapa nchini.
Mwisho, napenda kuwashukuru tena na kuwapongeza TMA na
WMO kwa maadhimisho haya ya siku ya hali ya hewa Duniani. Natoa wito kwa jamii
yote, ambao kimsingi ndio watumiaji wa taarifa za hali ya hewa tusherehekee
siku hii kwa kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa kwa usalama wetu na
mali zetu.
Nawatakia maadhimisho mema ya Siku ya Hali ya Hewa
Duniani 2019
“Jua, Dunia, na Hali ya Hewa
UJUMBE WA MKURUGENZI
MKUU WA MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA), DKT. AGNES KIJAZI KWENYE KILELE
CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI “WORLD METEOROLOGICAL DAY
(WMD)”, 23 MACHI, 2019.
Leo
ni siku ya Hali ya Hewa Duniani “the World Meteorological Day (WMD)”, siku
ambayo dunia inaadhimisha kuanzishwa kwa Shirika la Hali Duniani (WMO) ambapo Mkataba
wa kuanzishwa kwa Shirika hilo ulisainiwa mnamo tarehe 23 Machi 1950. Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ikiwa moja wapo ya Taasisi za Hali ya Hewa za
nchi 192 wanachama wa WMO inaungana na Jumuiya ya Hali ya Hewa Ulimwenguni kote kusheherekea siku hii. Taasisi za Hali ya Hewa, hutumia
siku hii kueleza huduma za hali ya hewa na umuhimu wa kuzingatia na kujumuisha
taarifa za hali ya hewa, ikiwemo utabiri na tahadhari katika kupanga na
kutekeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kimaendeleo kwa ujumla.
Kwa
upande wa hapa nchini Tanzania, huduma za hali ya hewa hutolewa na kusimamiwa
na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA). TMA ni taasisi ya serikali chini ya Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Mamlaka imepewa dhamana ya kutoa na kusimamia
huduma za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ili kusisitiza
na kuhamasisha umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika mipango na
maamuzi ya shughuli za kiuchumi na kijamii katika sekta mbalimbali, Uadhimishaji
wa sherehe za siku ya Hali ya Hewa Duniani unaambatana na kauli mbiu maalumu
kwa kila mwaka. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Jua, Dunia na Hali ya hewa (The
Sun, The Earth, and the Weather)”. Kauli mbiu hii imechaguliwa kwa
kuzingatia ukweli kwamba jua ndicho chanzo kikuu cha nishati ambayo huwezesha
maisha ya viumbe vyote hapa duniani na huendesha mifumo ya hali ya hewa,
mikondo ya bahari na mzunguko wa maji (hydrological cycle) na kuchangia katika
shughuli zetu za kila siku za kiuchumi na kijamii katika uso wa Dunia.
Jua ndio nyota iliyo karibu zaidi na Dunia, umbali upatao Kilometa milioni
150 kutoka uso wa Dunia. Jua ndicho kitovu cha Unajimu na chanzo kikuu cha joto
lililopo katika uso wa dunia ambalo linahitajika na viumbe hai mbalimbali ili
viweze kuishi. Bila mwanga na joto litolewalo na jua kusingekuwa na maisha
yoyote katika uso wa Dunia. Hivyo, joto litokanalo na jua ndilo husababisha
mzunguko wa maji (hydrological cycle), mvukizo wa maji angani (evaporation) ambayo
huganda na kufanyika mawingu na kisha kurudi tena kwenye uso wa Dunia kwa njia
ya mvua. Mbali na kuwa chanzo kikuu cha mifumo ya hali ya hewa tunayoipata na
kuwezesha maisha ya viumbe hai, mwanga wa jua una mchango wa pekee katika afya
na ustawi wa viumbe hai na masuala ya Nishati. Inatazamiwa kuwa mchango wa
Nishati mbadala katika mahitaji ya nishati ya dunia utafikia asilimia 40%
ifikapo mwaka 2040. Uimarishaji wa upatikanaji na matumizi ya Nishati mbadala,
ikiwemo nishati ya Jua na nishati ya upepo unahitaji jitihada kubwa za
kuimarisha shughuli za uangazi wa hali ya hewa, ambapo mchango na wajibu wa
Taasisi za Hali ya Hewa ikiwemo TMA ni mkubwa. Utoaji wa taarifa za hali ya
hewa mahsusi kwa ajili ya masuala ya nishati ni wa muhimu sana, ukizingatia
mikakati ya jumuiya ya kimataifa ya kuimarisha matumizi ya nishati mbadala ili
kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa (climate change). Uelewa
kuhusu hali ya klimatolojia ya eneo husika ikiwemo mwenendo wa jua na nguvu
yake, pamoja na nishati ya upepo ni muhimu sana katika kutoa mwongozo na
kuongeza ufanisi na tija kwa uwekezaji unaolenga
kuimarisha nishati mbadala.
Katika kuimarisha upatikanaji na utumiaji wa taarifa za
hali ya hewa katika kupanga shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii na
kufikia maendeleo endelevu jitihada mbalimbali za kuboresha huduma za hali ya
hewa katika ngazi ya kidunia na kitaifa zinafanyika. Katika ngazi ya kidunia,
Programu ya Kidunia ya Huduma za Hali ya Hewa “The Global Framework for Climate
Services (GFCS)” ndiyo programu inayotoa mwongoza wa namna ya kuboresha utoaji
na utumiaji wa taarifa za hali ya hewa
katika mipango na maamuzi kwenye sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii
duniani. Katika kuendeleza jitihada za kidunia, Tanzania inatekeleza Programu
ya Kitaifa ya Huduma za Hali ya Hewa “the National Framework for Climate
Services (NFCS)”, ambayo ilizunduliwa rasmi mwezi julai, 2018 ikiwa na malengo
ya kuboresha huduma za hali ya hewa hususan kwa sekta zilizo katika hatari ya kuathirika
zaidi na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na mabadiliko ya tabia nchi zikiwemo
Kilimo na Usalama wa chakula, Maji, Afya, Nishati na Maafa. Utekelezaji wa
mpango wa NFCS umejikita katika kuimairisha shughuli za uangazi, utabiri,
utafiti, ushirikishwaji wa Wadau na kujenga uwezo wa wataalamu na watumiaji wa
taarifa za hali ya hewa.
Utabiri utolewao na TMA ni pamoja na utabiri wa kila siku (masaa 24), siku
tano, siku kumi, mwezi, msimu na taarifa za hali mbaya ya hewa (severe weather
warnings and alerts). Tabiri hizi za hali ya hewa ni kwa jamii yote kwa ujumla,
na kwa sekta maalumu kama vile sekta ya usafiri wa anga, usafiri wa kwenye maji
na nchi kavu, kilimo (kilimo mazao, mifugo na uvuvi), nishati, maji, utalii,
afya, na usimamizi wa majanga kwa kutaja maeneo machache.
Taarifa hizi husambazwa kwa njia mbalimbali zikiwemo tovuti ya TMA (www.meteo.go.tz), radio, runinga, mitandao ya kijamii (facebook, twitter
and Youtube), magazeti na Mfumo wa Kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa njia
ya simu za mkononi (FarmSMS).
Katika kuadhimisha siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka 2019, napenda kutoa
wito kwa wadau wote kuzifuatilia na kuzitumia taarifa za hali ya hewa katika
kupanga mipango ya kiuchumi na kijamii kwa ajili ya maendeleo endelevu ya nchi yetu na hasa kuchangia katika azma ya
nchi yetu kwenda katika uchumi wa kati na uchumi wa viwanda
Nawatakia maadhimisho mema ya Siku
ya Hali ya Hewa Duniani “World Meteorological Day” (WMD).
“Jua, Dunia
na Hali ya Hewa”.
Siku ya Hali ya Hewa Duniani 2019
Tunafarijika kuona namna ambavyo TMA yetu inavyoendelea kuboresha huduma za hali ya hewa kwa jamii. Viva TMA
ReplyDeleteTMA ni taasisi inayoendelea kujipambanua vyema katika majukumu yake ya kuhakikisha usalama wa raia na malizao unatekelezwa ipasavyo katika kufikia nchi ya uchumi wa kati na maendeleo ya viwanda.
ReplyDelete