Taarifa hiyo imeelezea uwepo wa migandamizo midogo ya hewa kuanzia tarehe 5 Machi, umepelekea kutokea kwa kimbunga (Idai) kuanzia tarehe 10 hadi 15 Machi, 2019 katika rasi ya Msumbiji na kusababisha upepo wenye unyevunyevu kusukumwa kusini mwa Afrika na hivyo kupelekea upungufu wa mvua katika maeneo mengi ya nchi hususan ukanda wa kaskazini. Migandamizo midogo ya hewa inaendelea kujitokeza katika maeneo ya kaskazini mwa Madagascar, ambapo kwa sasa moja ya migandamizo hiyo imeimarika na kuwa kimbunga Savannah. Migandamizo na vimbunga hivi vinatarajiwa kusababisha mvua kuelekea zaidi katika maeneo ya bahari ya Hindi na upungufu katika maeneo mengi ya nchi, kutokana na mahali mwelekeo unaotarajiwa.
Kutokana na mifumo ya hali ya hewa ilivyo kwa sasa na jinsi inavyotarajiwa kuwa kwa kipindi cha Machi – Mei 2019 (kama ilivyoelezwa katika kipengele II cha taarifa hii);
Uwezekano mkubwa wa upungufu wa mvua katika mikoa ya Dar es salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na vipindi vichache vya upungufu wa mvua katika maeneo machache ya mikoa ya Kilimanjaro na Manyara.
Mwelekeo wa mvua za Masika uliotolewa ulionesha kuwa mvua zinatarajiwa kuwa za muda mfupi na kuisha mapema kati ya wiki ya nne ya mwezi Aprili na wiki ya kwanza ya mwezi Mei, 2019. Hata hivyo, hali iliyopo sasa inaonesha uwezekano wa mvua za Masika kuisha mapema zaidi katika baadhi ya maeneo wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2019.
Mvua za msimu (Novemba-Aprili) zinatarajiwa kuendelea kama zilivyotabiriwa. “Mvua za Msimu ambazo zilianza mwezi Novemba, 2018 zinatarajiwa kuendelea hadi mwishoni mwa mwezi April 2019. Katika kipindi hicho mvua hizo za Msimu zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo mengi. Hata hivyo, mvua za chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo machache ya kanda ya Kusini (Ruvuma), pamoja na mikoa ya Dodoma na Singida”.
I. MREJEO WA MWELEKEO WA MSIMU WA MVUA KIPINDI CHA MACHI - MEI 2019
Msimu wa mvua za Masika ni mahususi katika maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini-mashariki, pwani ya Kaskazini na visiwa vya Unguja na Pemba, ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Ufuatao ni mwelekeo wa mvua za Masika kwa kipindi kilichosalia;
a) Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Mara na Simiyu): Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani kwa ujumla katika maeneo ya mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu na Mara. Hata hivyo, maeneo machache ya mkoa wa Kagera na wilaya ya Kibondo yanatarajiwa kuwa na upungufu wa mvua. Mvua zinatarajiwa kuisha mapema katika wiki ya tatu ya mwezi Aprili, 2019.
b) Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro):
Katika kipindi cha msimu kilichosalia, mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga pamoja na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro. Aidha, mvua za wastani kwa ujumla zinatarajiwa katika maeneo mengi ya visiwa vya Unguja na Pemba. Pamoja na mvua za juu ya wastani kujitokeza katika maeneo machache ya visiwa vya Unguja na Pemba, mvua zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2019. Mvua katika maeneo ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro zinatarajiwa kuisha katika wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2019.
c) Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara):
Kwa ujumla, mvua za wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi. Hata hivyo, mvua za juu ya wastani zinatarajiwa kujitokeza katika maeneo machache ya mkoa wa Arusha. Mvua zinatarajiwa kuisha mapema katika wiki ya tatu ya mwezi Aprili, 2019.
II. MIFUMO YA HALI YA HEWA
Hali ya joto la bahari pamoja na mifumo ya hali ya hewa inaonesha upungufu wa mvua katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka. Katika kipindi cha msimu kilichosalia, joto la bahari la juu ya wastani linatarajiwa katika maeneo ya kati na kusini magharibi mwa bahari ya Hindi, hali ambayo inatarajiwa kupelekea kuvuma kwa upepo hafifu kutoka mashariki na kusababisha upungufu wa mvua katika maeneo mengi nchini. Halikadhalika, joto la bahari la wastani hadi juu kidogo ya wastani linatarajiwa katika eneo la kusini mashariki mwa bahari ya Atlantic karibu na pwani ya Angola. Hali hii inatarajiwa kupunguza msukumo wa upepo kutoka magharibi na hivyo kupunguza uwepo wa unyevunyevu kutoka misitu ya Kongo.
III. USHAURI
Mamlaka ya Hali ya Hewa inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, Mamlaka za Wanyamapori, Mamlaka za Maji na Afya waendelee kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta husika.
Mwelekeo wa mvua uliotolewa hapa umezingatia zaidi kipindi cha msimu (miezi mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa. Hivyo, viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi katika maeneo madogo utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi. Watumiaji wa taarifa za utabiri huu wanashauriwa pia kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 pamoja na mwezi kama unavyotolewa na Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania.
Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa za mwelekeo wa mvua nchini.
No comments:
Post a Comment