Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
katika jitihada zake za kutambua umuhimu wa ushirikishwaji wa wadau wa huduma
za hali ya hewa ili kuhakikisha huduma zitolewazo zinakidhi matwaka ya
watumiaji, imekutana na wadau wa huduma za hali ya hewa baharini ili kupata
mrejesho wa huduma zinazotolewa na kuweza kuzifanyia maboresho kulingana vigezo
vya kitaifa na kimataifa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa
kikao hicho cha wadau
wanaotumia huduma za hali ya hewa kwa shughuli baharini kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa
Chuo cha Baharia (DMI), tarehe 08 Machi 2019, mkurugenzi mkuu wa TMA Dkt. Agnes
Kijazi aliwaeleza washiriki wa mkutano lengo ni kutoa uelewa wa huduma
zitolewazo na kupokea mrejesho pamoja na kuibua fursa za ushirikiano kati ya
TMA na wadau hao na kusaidia katika kuboresha huduma.
‘lengo la mkutano huu ni kuwapa uelewa wa huduma za
hali ya hewa zinazotolewa kwaajili ya watumiaji wa bahari na pia kupata
mrejesho kutoka kwenu kuhusu huduma hizo sambamba na kuibua fursa za
ushirikiano kati ya TMA na ninyi watumiaji wa huduma za hali ya hewa ili kuboresha
huduma zinazotolewa katika sekta hii ya bahari ‘Alizungamza Dkt. Kijazi’.
Aidha, aliongezea kwa kueleza kuwa mkutano huo
unasaidia kuibua fursa na changamoto zilizopo ili kwa pamoja tuweze kufanikiwa
katika utoaji na utumiaji wa huduma za hali ya hewa kwa shughuli za bahari na
maziwa makuu kwa kuzingatia miongozo ya ndani na miongozo inayotolewa na
Mashirika ya kimataifa ikiwemo Shirika
la Hali ya Hewa Duniani - (WMO); Shirika
la Kimataifa la Bahari – (IMO) na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la
Umoja wa Mataifa kupitia kamisheni inayohusu masuala ya bahari ya Hindi -
(UNESCO-IOC).
Vile vile, wadau walipata fursa ya kupitia mfumo
mpya wa mawasiliano unaoitwa Mfumo wa Mawasiliano wa Taarifa za za Hali ya Hewa
Baharini – Marine Meteorological Information System (MMIS) unaoundwa na kuweza
kutoa michango yao ya maboresho kabla ya kuzinduliwa rasmi.
Kwa upande wa wadau waliipongeza TMA kwa kuandaa
warsha/mkutano kama huo wenye lengo la kukidhi mahitaji ya wadau na kushauri
kuwa endelevu ili kufika malengo ikiwa ni pamoja na mafunzo ya mfumo,
kufanikisha huduma za baharini zinapata cheti cha ubora kama zilivyo huduma za
usafiri wa anga.
Mkutano huo wa wadau uliwakutanisha wadau kutoka
Mamlaka ya Bandari za Tanzania Bara na Visiwani (TPA na ZPC), Shirika la
Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Chuo
cha Bahari (DMI), Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA),
Chama cha Maafisa wa Meli Tanzania (MNOAT), Shirika la Maendeleo ya Mafuta
(TPDC), wakala wa makampuni ya meli kama
vile PIL, MESSINA, Chama cha Mabaharia (TSC), Flyinghorse na wengine wengi
IMETOLEWA NA
OFISI YA UHUSIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA
TANZANIA
No comments:
Post a Comment