Monday, March 22, 2021

SIMANZI YATANDA TANZANIA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI, 2021


 

“Mchango wa bahari katika hali ya hewa”-(The Ocean, Our Climate and Weather)


Dar es Salaam, Tarehe 23/03/2021

Leo, tarehe 23 Machi, 2021 ni Siku ya Hali ya Hewa Duniani ikiwa ni kumbukizi ya kusainiwa kwa Mkataba wa kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) mnamo tarehe 23 Machi, 1950. Siku hii imefikiwa wakati Tanzania ikiwa katika maombolezo ya Kitaifa kufuatia kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyefariki tarehe 17 Machi, 2021. Hivyo kwa upande wa Tanzania maadhimisho haya hayatafanyika Kitaifa kama ilivyo kawaida bali siku hii inatumika kukumbuka mchango wa Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika kuboresha sekta na huduma za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bodi, menejimenti na watumishi wa TMA tunatoa salamu za pole kwa Watanzania wote kwa kuondekewa na Kiongozi wetu Mahiri, Mchapakazi na Mzalendo wa kweli.

Miongoni mwa michango muhimu katika sekta ya hali ya hewa katika kipindi cha Uongozi wa Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ni;

1.    Kutungwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Namba 2 ya mwaka 2019 iliyoibadili TMA kutoka Wakala wa Hali ya Hewa Tanzania na kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Mabadiliko hayo yameipa TMA mamlaka ya kisheria ya kuendelea kutekeleza jukumu la kutoa huduma za hali ya hewa na kuongezewa jukumu la kudhibiti na kuratibu shughuli za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, sheria hiyo inaipa TMA mamlaka ya kisheria ya kukusanya mapato yanayotokana na matumizi ya huduma za hali ya hewa kwa shughuli za kibiashara. Hivyo, kuiwezesha sekta ya hali ya hewa kuwa bora zaidi na kuongeza mchango wake katika  kuinua uchumi wa Nchi katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

2.    Mchango mwingine muhimu uliofanywa na Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika sekta ya Hali ya Hewa ni uboreshaji wa miundombinu ya ufuatiliaji na upimaji wa hali ya hewa ikiwa ni pamoja na mtandao wa RADA saba za hali ya hewa ili kuona hali ya hewa ya eneo lote la nchi yetu. RADA tatu zilizofungwa Dar es Salaam, Mtwara na Mwanza tayari zinafanya kazi. RADA nyingine nne ambazo ziko katika mpango huu  na tayari ziko katika hatua za matengenezo na ununuzi zitafungwa katika mikoa ya Kigoma, Dodoma, Kilimanjaro na Songwe.  RADA tano kati ya saba zitahusika katika uangazi wa eneo la bahari na maziwa makuu yanayozunguka nchi yetu. Maeneo hayo ni pamoja na pwani ya Bahari ya Hindi (Dar es Salaam na Mtwara), Ziwa Viktoria (Mwanza), Ziwa Tanganyika (Kigoma) na Ziwa Nyasa (Songwe).

3.    Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameboresha miundombinu ya vifaa vya hali ya hewa kuwa vya kisasa zaidi.  Vifaa vinavyotumia zebaki vimeondolewa na kufungwa vifaa vya kisasa visivyotumia zebaki ikiwa ni utekelezaji wa mkataba wa Minamata unaoelekeza kusitisha matumizi ya zebaki duniani.

4.    Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pia aliweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa programu za Kidunia na Kikanda za masuala ya hali ya hewa. Programu hizo ni pamoja na programu ya WMO ya Kidunia ya utoaji wa huduma za hali ya hewa “Global Framework for Climate Services Adaptation Programme in Africa (GFCS APA)”; na programu ya “Weather and Climate Information Services for Africa (WISER)”, pamoja na uandaaji wa Mfumo wa Kitaifa wa Huduma za Hali ya Hewa “National Framework for Climate Services(NFCS)”. Utekelezaji wa programu hizi umechangia kuboresha huduma za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na huduma kwa watumiaji wa bahari na maziwa makuu. Kwa mfano, program ya “WISER” ilisaidia kuundwa kwa mfumo wa utoaji huduma za hali mbaya ya hewa “Multi-Hazard Early Warning System (MHEWS)”, ambao umejumuisha wadau wote muhimu, ikiwa ni pamoja na Mfumo wa Kitaifa wa Utoaji wa Taarifa “National Early Warning System (NEWS)” ukihusisha Ofisi ya Taifa ya Uratibu wa Maafa “National Disaster Management Office (DMO)”. Mfumo huo ulifanyiwa majaribio katika tukio la kimbunga Kenneth kilichotokea mwezi Aprili, 2019 ambapo ulionekana kuwa ni mfumo wenye ufanisi mkubwa katika uratibu wa matukio ya vimbunga.

5.    Aidha, Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameweka kipaombele katika kujenga uwezo wa rasilimali watu katika sekta ya hali ya hewa kwa kuongeza wataalam bingwa wa hali ya hewa (Meteorologists) ambapo mwaka 2015 alipoingia madarakani TMA ilikuwa na wataalam bingwa sitini na saba (67) na mwaka huu 2021 wapo wataalam bingwa 131. Aidha, wataalam hao wamepatiwa mafunzo mbali mbali ya kuwaongezea weledi na hivyo kuongeza umahiri wao katika kutoa utabiri wa hali ya hewa.

6.    Uboreshaji huo alioufanya Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wa miundo mbinu ya hali ya hewa pamoja na ongezeko la wataalam bingwa umeiwezesha TMA kupata cheti cha kimataifa cha ubora  katika utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa usalama wa usafiri wa anga yaani ISO 9001:2015 certification. Aidha, uboreshaji huo umewezesha kuongezeka kwa viwango vya usahihi wa utabiri wa hali ya hewa kutoka asilimia 78 mwaka 2015 hadi kufikia kati ya asilimia 82 na 96 mwaka 2020.

7.    Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameweka mazingira wezeshi yaliyoiwezesha TMA  kutekeleza jukumu lake la kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika masuala ya hali ya hewa kikanda na kimataifa kwa ufanisi na mafanikio makubwa. Aidha, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliidhinisha jina la Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi kugombea nafasi ya makamu wa tatu wa  Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ambapo alichaguliwa katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka minne kuanzia 2019 hadi 2023. Dkt. Agnes Kijazi ni mwanamke wa kwanza kutoka Bara la Afrika na nchi zinazoendelea kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo kubwa ya uongozi wa juu kabisa katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).

8.    Aidha, kipindi cha utawala wa Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli taarifa za kisayansi za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa nchini zimeboreshwa ambapo TMA inatoa jarida la mwenendo wa hali ya hewa nchini (Statement on the Status of Tanzania Climate). Jarida hili limesheheni taarifa muhimu ambazo zinasaidia katika mipango ya muda mrefu sambamba na utekelezaji wa dira ya nchi ya uchumi wa viwanda.

9.  Uboreshaji wa huduma za hali ya hewa zitolewazo na TMA alioufanya Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli umeimarisha uwezo wa Serikali katika kupunguza madhara ya majanga yanayosababishwa  na  matukio ya hali mbaya ya hewa. Aidha, uboresha wa huduma za hali ya hewa umeimarisha uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Kutokana na mafanikio haya na mengine mengi katika sekta ya hali ya hewa, matumizi ya taarifa za hali ya hewa zitolewazo na TMA yameongezeka katika kupanga shughuli za kiuchumi na kijamii hapa nchini.

10. Sambamba na mafanikio yaliyofikiwa, maboresho zaidi yanahitajika hususan kuongeza na kuboresha miundombinu ya vifaa vya upimaji na uchambuzi wa data za hali ya hewa; ufungashaji na elimu juu ya matumizi sahihi ya taarifa.  Katika kutekeleza hilo, TMA itaendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha matumizi sahihi ya huduma za hali ya hewa. Aidha, jitihada za Serikali pekee haziwezi kutatua changamoto zote za masuala ya hali ya hewa zinazoikabili jamii. Hivyo, jitihada zinahitajika pia kutoka kwa watumiaji na washirika wa huduma za hali ya hewa katika kuziboresha na kuhakikisha zinatumika ipasavyo.

Katika Siku hii ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka 2021, TMA inauenzi mchango mkubwa wa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alioutoa katika sekta ya hali ya hewa hapa nchini, na pia kikanda na kimataifa. Aidha, TMA itaendelea kuchapa kazi kwa bidii na kuwahudumia Watanzania wote ili kumuenzi shujaa wa uboreshaji wa sekta ya hali ya hewa Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuhakikisha uboreshaji alioufanya unakuwa endelevu. Pia, tunatoa wito kwa wadau wote wa huduma za hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na watumiaji wa bahari, wavuvi, wakazi wa maeneo ya fukwe na Mamlaka zinazohusika kuendelea kuzifuatilia na kuzitumia ipasavyo taarifa zitolewazo na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika mipango ya shughuli za kiuchumi na kijamii, na kuchukua hatua stahiki ambazo zitasaidia kupunguza madhara ya majanga na hatimaye kuongeza kasi ya ujenzi na maendeleo ya Taifa letu. TMA inakaribisha mashirikiano katika utekelezaji wa Mfumo wa Kitaifa wa Huduma za Hali ya Hewa (National Framework for Climate Services) na programu zingine za kuboresha huduma za hali ya hewa nchini ambazo Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ametuachia, wadau wote tuzitekeleze kwa ufanisi ikiwa ni sehemu ya kumuenzi shujaa huyu wa uboreshaji wa sekta ya hali ya hewa hapa nchini.

Maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani (WMD) kwa mwaka 2021 yanaongozwa na kaulimbiu ya “Mchango wa bahari katika hali ya hewa”-(The Ocean, Our Climate and Weather).  Kaulimbiu hii inalenga kufafanua umuhimu na uhusiano kati ya bahari, hali ya hewa, na athari zake kwa shughuli za kichumi na kijamii za kila siku.

Mchango wa bahari katika hali ya hewa umetokana na uhusiano mkubwa uliopo kati ya bahari na anga ambapo umesababisha kuona ulazima wa kuelewa kwa kina tabia na mwenendo wa bahari ili kutoa utabiri wa hali ya hewa kwa usahihi. Moja ya uhusiano muhimu kati ya bahari na anga, ni uwezo wa bahari kusharabu nishati ya jua inayofanikiwa kufika katika uso wa Dunia kwa kiasi kikubwa sana ambapo sehemu ya nishati hii huvukiza maji ya bahari na kutengeneza mawingu mengi na mazito, vimbunga na kusababisha mvua baharini na nchi kavu.

Utekelezaji wa programu mbalimbali za huduma za uangazi katika bahari umerahisisha upatikanaji wa data za hali ya bahari. Hivyo, uboreshaji wa miundombinu ya upimaji na ufuatiliaji wa hali ya anga na bahari, pamoja na uelewa wa kutosha wa mahusiano yaliyopo, unasaidia wanasayansi kutambua na kutabiri kwa urahisi zaidi viashiria muhimu vya bahari kwa hali ya hewa kama vile “El Niño” na “La Niña” hali ambazo huathiri hali ya hewa ya maeneo mengi na makubwa duniani ikiwa ni pamoja na Tanzania.  

Tanzania ni miongoni mwa Nchi 193 Wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ambao leo duniani kote wanaikumbuka siku hii muhimu ya kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Dunia mwaka 1950. Aidha, Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Prof. Petteri Taalas ametuma Salaam za Pole kwa Serikali, wana TMA na wananchi wote wa Tanzania kufuatia kifo cha Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambapo alisema Jumuia ya kimataifa imempoteza kiongozi mahiri aliyesimamia Amani na Maendeleo ya nchi yake. Wana TMA tuna ikumbuka siku hii tukiwa tumejawa na majonzi na simanzi kwa kuondokewa na shujaa wa uboreshaji wa huduma za hali ya hewa hapa nchini.

Maono ya Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa Sekta ya Hali ya Hewa Nchini yataendelea kuishi na Mchango wake Tutauenzi Daima.

PUMZIKA KWA AMANI SHUJAAWA UBORESHAJI WA HUDUMA ZA HALI YA HEWA.

“Mchango wa bahari katika hali ya hewa”-(The Ocean, Our Climate and Weather)”

 

Tuesday, March 16, 2021

HALI YA MWENENDO WA MVUA ZA MASIKA, 2021


 Dar es Salaam, 16 Machi, 2021:

Taarifa kuhusu mwenendo wa mvua za Masika (Machi–Mei, 2021) kwa maeneo ya kaskazini mwa nchi ambayo hupata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

Utabiri wa mvua za Masika, 2021 ulionesha kuwa mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Viktoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma - wilaya za Kakonko na Kibondo) na nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro); na wastani hadi chini ya wastani katika maeneo ya pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba). Mvua hizi zilitarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya mwezi Februari, 2021 (nyanda za juu kaskazini mashariki na pwani ya kaskazini) na wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2021 (ukanda wa Ziwa Viktoria). 

Mvua zimeanza kunyesha wiki ya nne ya mwezi Februari katika maeneo machache ya Pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki. Aidha mvua hizo zimekuwa na mtawanyiko hafifu katika maeneo mengi kama ilivyotabiriwa. Kwa ukanda wa Ziwa Viktoria mvua zimeanza kunyesha wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2021 katika baadhi ya maeneo kama ilivyotarajiwa. 

Uwepo wa mgandamizo mkubwa wa hewa nchini pamoja na kujitokeza kwa migandamizo midogo ya hewa katika eneo la kusini magharibi mwa bahari ya Hindi kumesababisha Ukandamvua wa kitropiki kuendelea kusalia maeneo ya kusini na hivyo kusababisha vipindi vya ukavu katika maeneo mengi hususan maeneo ya kaskazini mwa nchi.  Hata hivyo, mvua za Masika zinatarajiwa kuendelea kunyesha wiki ya nne ya mwezi Machi, 2021 katika baadhi ya maeneo ya Ukanda wa ziwa Victoria pamoja na maeneo machache ya nyanda za juu kaskazini mashariki na pwani ya kaskazini.

Kwa taarifa hii wananchi wanashauriwa kuendelea kuzingatia taarifa na tahadhari za hali ya hewa zilizotolewa na zitakazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania sambamba na kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazotokana na hali mbaya ya hewa.

Thursday, February 18, 2021

MASIKA 2021: MAENEO MENGI KUPATA MVUA ZA WASTANI.



Dar es Salaam, Tarehe 18/02/2021

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2021 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ikiwa ni mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani ikijumuisha kisiwa cha Mafia, Tanga na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na  visiwa vya Unguja na Pemba, Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara  pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

 

Akizungumzia utabiri huo Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri wa TMA, Dkt. Hamza Kabelwa kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi, alisema utabiri unaonesha mvua zitakuwa za wastani kwa maeneo mengi na uwepo wa mvua za juu ya wastani na chini ya wastani katika vipindi tofauti tofuati wakati wa msimu.

 

“Mvua za Masika zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara pamoja na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Kigoma (wilaya za Kakonko na Kibondo). Aidha, mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba”. Alisema Dkt. Kabelwa.

 

Aliendelea kwa kueleza kuwa mvua za Masika zinatarajiwa kuanza mapema katika wiki ya nne ya mwezi Februari, 2021 hususan katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki na pwani ya kaskazini na vipindi vya ukavu vinatarajiwa kujitokeza hususan katika mwezi Mei, 2021. Hivyo, unyevunyevu wa kutosha kwenye udongo unatarajiwa kuimarisha uzalishaji wa mazao mbalimbali ukiwemo mpunga na uwepo wa malisho na maji ya kutosha kwa ajili ya mifugo na wanyamapori unatarajiwa kupunguza migogoro baina ya wanyama na binadamu

Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Kabelwa alisema vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza na kuambatana na mafuriko, hivyo jamii inashauriwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa mara kwa mara na kuchukua hatua stahiki ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kama vile uharibifu wa miundombinu, shughuli za kijamii kuathirika, upotevu wa maisha na mali.

 

 Kwa taarifa zaidi tembelea tovuti yetu www.meteo.go.tz

 

Tuesday, February 16, 2021

WADAU WATAKIWA KUTUMIA TAARIFA ZA HALI YA HEWA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA HALI YA HEWA.




Mgeni rasmi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya TMA Dkt. Buruhani Nyenzi akizungumza kwa kusisitiza wakati akifungua warsha ya wadau ya kujadili utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2021 unaotarajiwa kutolewa rasmi Tarehe 18 februari, 2021 katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza - Dar es Salaam, Tanzania


Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi  akifafanua jambo kwa wadau katika warsha ya kujadili utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2021 unaotarajiwa kutolewa rasmi Tarehe 18 februari 2021 katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza - Dar es Salaam, Tanzania


Wadau kutoka sekta mbalimbali katika picha ya pamoja na mgeni rasmi kwenye warsha ya wadau ya kujadili utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2021 unaotarajiwa kutolewa rasmi Tarehe 18 februari, 2021 katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza - Dar es Salaam, Tanzania




Matukio katika picha wakati wadau wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika warsha ya wadau ya kujadili utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2021 unaotarajiwa kutolewa rasmi Tarehe 18 februari, 2021 katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza - Dar es Salaam, Tanzania







Wadau kutoka sekta mbalimbali wakiwasilisha athari na ushauri katika sekta zao kwenye warsha ya wadau ya kujadili utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2021 unaotarajiwa kutolewa rasmi Tarehe 18 februari, 2021 katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza - Dar es Salaam, Tanzania





 Dar es Salaam; Tarehe 15 - 16 Februari, 2021;

Wadau wa hali ya hewa kutoka sekta mbalimbali wametakiwa kutumia taarifa za hali ya hewa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Hayo yalizungumzwa na Mgeni Rasmi na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Buruhani Nyenzi, wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Utabiri wa Mvua za Msimu wa Masika (Machi -Mei 2021), uliofanyika katika Ukumbi wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (The Law School of Tanzania), Dar es Salaam.

“Nichuke fursa hii kuwasihi wadau wote wa hali ya hewa katika sekta mbalimbali kujihusisha zaidi katika kuelewa na kufuatilia masuala ya hali ya hewa na mabadiliko yake ili kuweza kuchukua hatua stahiki za kujikinga na kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa. Kwa kufanya hivyo tutasababisha mazingira tunayoishi yaendelee kubaki salama na kuwa katika asili yake na yenye kuvutia kwa shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo”. Alizungumza Dkt. Nyenzi.

Aidha, Dkt. Nyenzi aliendelea kwa kusema kuwa ni jukumu letu kuendelea kuelimishana kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na namna ya kukabiliana nayo na wakati huo huo tukiendelea kutekeleza sera na mikakati ambayo itatusaidia kutumia vyema huduma za hali ya hewa katika kuinua uchumi wa nchi yetu, kutoka uchumi wa kati tuliofikia sasa kwenda uchumi wa juu zaidi.

“Mabadiliko ya tabia nchi  ni halisi ambapo tumeshuhudia athari mbalimbali zinazotokana na mabadiliko haya ikiwa ni pamoja na kuwa na vipindi vya mvua kubwa, kubadilika kwa misimu ya mvua hasa tarehe za kuanza na kuisha kwa mvua, wote tumeshuhudia mvua zilizo nje ya msimu kwa mwaka huu wa 2021 katika maeneo ambayo kwa kawaida huwa ni makavu kwa miezi ya Januari na Februari, hali hii inasababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa (climate change)”. Alifafanua Dkt. Nyenzi.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi alieleza kuwa mkutano huo unalenga kujadiliana na kupata maoni ya wadau jinsi utabiri wa mvua za Masika utakavyoweza kutumika kwa tija katika sekta mbalimbali hapa nchini na hivyo kuendeleza na kuimarisha utoaji wa huduma za hali ya hewa na matumizi yake kwa jamii. 

“Ipo haja ya kutambua uwezo wa utabiri wa hali ya hewa na  hususan utabiri wa msimu kama zana yenye nguvu katika  kusaidia watoa maamuzi kukabiliana na changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa. Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Tumia taarifa za utabiri kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa”. Alisema Dkt. Kijazi.

Dkt. Kijazi aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa jitihada za kuboresha miundombinu na huduma za hali ya hewa hapa nchini na kufanya huduma zinazotolewa na TMA kuendelea kuwa bora na kukidhi viwango vya kimataifa.

Kwa upande wake, mdau kutoka Wizara ya Kilimo Bw. Robert Dimoso alisema katika kipindi cha msimu wa mvua za vuli ulioanza oktoba mpaka Disemba 2020, maeneo mengi yalipata mvua za chini ya wastani hivyo kupelekea kupata unyevunyevu mzuri kwenye udongo ambao ulisaidia kustawi vizuri kwa mazao, hata hivyo kuna maeneo machache yalipata mvua za juu ya wastani hasa mikoa ya kanda ya ziwa ambayo ilichangia kuharibika kwa zao la maharage, lakini kwa ujumla utabiri uliendana na uhalisia kama ulivyotabiriwa.

Naye, mdau kutoka sekta ya Makazi Mijini Bw. Tim Ndezi alitoa pongezi zilizotolewa na wakazi wanaoishi katika makazi holela akisema wakazi hao wamefurahishwa sana na utabiri uliotolewa katika msimu uliopita kwani umekuwa sahihi sana na hata idadi ya watu wanaoathirika na mafuriko katika msimu uliopita imekuwa ni kidogo sana kama rekodi zinavyoonesha kwasababu watu walipata taarifa mapema na kuchukuwa tahadhari.

Bw. Simon Kadogosa kutoka Redcross alisema utabiri uliwasaidia katika kuboresha akiba ya vifaa vya uokozi na vilevile ulichangia katika kufanikisha  miradi mbalimbali ambayo inafanyika kwa ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu hususan kwenye mikoa ya Iringa, Songwe na Arusha.





Tuesday, February 9, 2021

DKT. KIJAZI AONGOZA MKUTANO WA KUJADILI VIPAUMBELE KATIKA MPANGO MKAKATI WA WMO WA KUJENGA UWEZO.

 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi akimsikiliza Katibu Mkuu wa WMO, Prof. Petteri Taalas alipomkaribisha kutoa neno katika ufunguzi wa mkutano wa pili wa Jopo la Kamati Kuu ya WMO ya Kujenga Uwezo “Second Meeting of the Executive Council Capacity Development Panel (CDP-2)”, Tarehe 3 Februari, 2021.


 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi akitoa hotuba ya kufungua mkutano wa pili wa Jopo la Kamati Kuu ya WMO ya Kujenga Uwezo “Second Meeting of the Executive Council Capacity Development Panel (CDP-2)”, Tarehe 3 Februari, 2021. Kulia kwake ni Meneja wa Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Wilbert Muruke  na kushoto kwake ni Mtaalamu wa Hali ya Hewa  katika Ofisi ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mathew Ndaki wakimsaidia Mwenyekiti katika kuongoza kikao.


Dar es Salaam; Tarehe 03/02/2021.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi, ameongoza mkutano wa pili wa Jopo la Kamati Kuu ya WMO ya Kujenga Uwezo “Second Meeting of the WMO Executive Council Capacity Development Panel (CDP-2)”.

Akizungumza wakati akifungua rasmi mkutano huo, Dkt. Kijazi aliwataka wajumbe wa mkutano huo, kuzingatia lengo lililokasimiwa kwa jopo la kushauri namna bora ya kujenga uwezo katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa Duniani.

“Mkutano huu umelenga kujadili taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Vikosi kazi vinavyounda Jopo hili, na kuandaa mapendekezo ya kuwasilisha kwenye Kamati Kuu ya WMO (WMO Executive Coincil (EC), na mapendekezo ya maeneo ya vipaumbele kwa ajili ya kuandaa Mpango Mkakati wa kujenga uwezo (WMO Capacity Development Strategy) katika utoaji huduma Kimataifa”. Alizungumza Dkt. Kijazi.

 Katika hatua nyingine, Dkt. Kijazi alimpongeza Katibu Mkuu wa WMO, Prof. Petteri Taalas, kwa kupewa tuzo na jarida la “Reader’s Digest Magazine” kama Mtu Mashuhuri wa Bara la Ulaya wa mwaka 2020 (European of the Year), ikiwa ni  kutambua mchango wake wa kuongoza jitihada za WMO kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Naye, Prof. Taalas alimshukuru Dkt. Kijazi na kusema kuwa tuzo hiyo ni maalum kwa wadau wote wa WMO na huduma za hali ya hewa kwa ujumla na alimpongeza  Dkt. Kijazi kwa uongozi wake mahiri unaosaidia  kufanikisha utekelezaji wa malengo ya WMO.

Mkutano huo ulifanyika kwa njia ya mtandao (teleconference) Tarehe 3 na 4 Februari, 2021 chini ya Mwenyekiti wa Jopo hilo, Dkt. Kijazi na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa WMO, Prof. Petteri Taalas na watendaji wengine waandamizi wa WMO. Mkutano ulijadili taarifa za Vikosi kazi vinavyounda jopo hilo na kuandaa mapendekezo mbalimbali ya kujenga uwezo katika huduma za hali ya hewa. Miongoni mwa mapendekezo hayo ni pamoja na yatakayowasilishwa katika mkutano wa 73 wa Kamati Kuu ya WMO na  mapendekezo ya maeneo ya vipaumbele vitakavyotumika kuandaa Mpango Mkakati wa WMO wa kujenga uwezo. Mjadala ulijielekeza kutambua kwamba hali ya hewa haina mipaka hivyo katika kipindi hiki cha kuongezeka majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa jopo hilo lihakikishe vipaombele katika kujenga uwezo vinaelekezwa kuzisadia nchi zinazoendelea pamoja na za Bara la Afrika ili kuhakikisha maendeleo katika sekta ya hali ya hewa hayamuachi mtu yoyote nyuma (no one should be left behind).


Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...