Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2021 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ikiwa ni mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani ikijumuisha kisiwa cha Mafia, Tanga na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
Akizungumzia utabiri huo Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri wa TMA, Dkt. Hamza Kabelwa kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi, alisema utabiri unaonesha mvua zitakuwa za wastani kwa maeneo mengi na uwepo wa mvua za juu ya wastani na chini ya wastani katika vipindi tofauti tofuati wakati wa msimu.
“Mvua za Masika zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara pamoja na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Kigoma (wilaya za Kakonko na Kibondo). Aidha, mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba”. Alisema Dkt. Kabelwa.
Aliendelea kwa kueleza kuwa mvua za Masika zinatarajiwa kuanza mapema katika wiki ya nne ya mwezi Februari, 2021 hususan katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki na pwani ya kaskazini na vipindi vya ukavu vinatarajiwa kujitokeza hususan katika mwezi Mei, 2021. Hivyo, unyevunyevu wa kutosha kwenye udongo unatarajiwa kuimarisha uzalishaji wa mazao mbalimbali ukiwemo mpunga na uwepo wa malisho na maji ya kutosha kwa ajili ya mifugo na wanyamapori unatarajiwa kupunguza migogoro baina ya wanyama na binadamu
Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Kabelwa alisema vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza na kuambatana na mafuriko, hivyo jamii inashauriwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa mara kwa mara na kuchukua hatua stahiki ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kama vile uharibifu wa miundombinu, shughuli za kijamii kuathirika, upotevu wa maisha na mali.
Kwa taarifa zaidi tembelea tovuti yetu www.meteo.go.tz
No comments:
Post a Comment