Monday, March 22, 2021

SIMANZI YATANDA TANZANIA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI, 2021


 

“Mchango wa bahari katika hali ya hewa”-(The Ocean, Our Climate and Weather)


Dar es Salaam, Tarehe 23/03/2021

Leo, tarehe 23 Machi, 2021 ni Siku ya Hali ya Hewa Duniani ikiwa ni kumbukizi ya kusainiwa kwa Mkataba wa kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) mnamo tarehe 23 Machi, 1950. Siku hii imefikiwa wakati Tanzania ikiwa katika maombolezo ya Kitaifa kufuatia kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyefariki tarehe 17 Machi, 2021. Hivyo kwa upande wa Tanzania maadhimisho haya hayatafanyika Kitaifa kama ilivyo kawaida bali siku hii inatumika kukumbuka mchango wa Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika kuboresha sekta na huduma za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bodi, menejimenti na watumishi wa TMA tunatoa salamu za pole kwa Watanzania wote kwa kuondekewa na Kiongozi wetu Mahiri, Mchapakazi na Mzalendo wa kweli.

Miongoni mwa michango muhimu katika sekta ya hali ya hewa katika kipindi cha Uongozi wa Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ni;

1.    Kutungwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Namba 2 ya mwaka 2019 iliyoibadili TMA kutoka Wakala wa Hali ya Hewa Tanzania na kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Mabadiliko hayo yameipa TMA mamlaka ya kisheria ya kuendelea kutekeleza jukumu la kutoa huduma za hali ya hewa na kuongezewa jukumu la kudhibiti na kuratibu shughuli za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, sheria hiyo inaipa TMA mamlaka ya kisheria ya kukusanya mapato yanayotokana na matumizi ya huduma za hali ya hewa kwa shughuli za kibiashara. Hivyo, kuiwezesha sekta ya hali ya hewa kuwa bora zaidi na kuongeza mchango wake katika  kuinua uchumi wa Nchi katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

2.    Mchango mwingine muhimu uliofanywa na Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika sekta ya Hali ya Hewa ni uboreshaji wa miundombinu ya ufuatiliaji na upimaji wa hali ya hewa ikiwa ni pamoja na mtandao wa RADA saba za hali ya hewa ili kuona hali ya hewa ya eneo lote la nchi yetu. RADA tatu zilizofungwa Dar es Salaam, Mtwara na Mwanza tayari zinafanya kazi. RADA nyingine nne ambazo ziko katika mpango huu  na tayari ziko katika hatua za matengenezo na ununuzi zitafungwa katika mikoa ya Kigoma, Dodoma, Kilimanjaro na Songwe.  RADA tano kati ya saba zitahusika katika uangazi wa eneo la bahari na maziwa makuu yanayozunguka nchi yetu. Maeneo hayo ni pamoja na pwani ya Bahari ya Hindi (Dar es Salaam na Mtwara), Ziwa Viktoria (Mwanza), Ziwa Tanganyika (Kigoma) na Ziwa Nyasa (Songwe).

3.    Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameboresha miundombinu ya vifaa vya hali ya hewa kuwa vya kisasa zaidi.  Vifaa vinavyotumia zebaki vimeondolewa na kufungwa vifaa vya kisasa visivyotumia zebaki ikiwa ni utekelezaji wa mkataba wa Minamata unaoelekeza kusitisha matumizi ya zebaki duniani.

4.    Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pia aliweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa programu za Kidunia na Kikanda za masuala ya hali ya hewa. Programu hizo ni pamoja na programu ya WMO ya Kidunia ya utoaji wa huduma za hali ya hewa “Global Framework for Climate Services Adaptation Programme in Africa (GFCS APA)”; na programu ya “Weather and Climate Information Services for Africa (WISER)”, pamoja na uandaaji wa Mfumo wa Kitaifa wa Huduma za Hali ya Hewa “National Framework for Climate Services(NFCS)”. Utekelezaji wa programu hizi umechangia kuboresha huduma za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na huduma kwa watumiaji wa bahari na maziwa makuu. Kwa mfano, program ya “WISER” ilisaidia kuundwa kwa mfumo wa utoaji huduma za hali mbaya ya hewa “Multi-Hazard Early Warning System (MHEWS)”, ambao umejumuisha wadau wote muhimu, ikiwa ni pamoja na Mfumo wa Kitaifa wa Utoaji wa Taarifa “National Early Warning System (NEWS)” ukihusisha Ofisi ya Taifa ya Uratibu wa Maafa “National Disaster Management Office (DMO)”. Mfumo huo ulifanyiwa majaribio katika tukio la kimbunga Kenneth kilichotokea mwezi Aprili, 2019 ambapo ulionekana kuwa ni mfumo wenye ufanisi mkubwa katika uratibu wa matukio ya vimbunga.

5.    Aidha, Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameweka kipaombele katika kujenga uwezo wa rasilimali watu katika sekta ya hali ya hewa kwa kuongeza wataalam bingwa wa hali ya hewa (Meteorologists) ambapo mwaka 2015 alipoingia madarakani TMA ilikuwa na wataalam bingwa sitini na saba (67) na mwaka huu 2021 wapo wataalam bingwa 131. Aidha, wataalam hao wamepatiwa mafunzo mbali mbali ya kuwaongezea weledi na hivyo kuongeza umahiri wao katika kutoa utabiri wa hali ya hewa.

6.    Uboreshaji huo alioufanya Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wa miundo mbinu ya hali ya hewa pamoja na ongezeko la wataalam bingwa umeiwezesha TMA kupata cheti cha kimataifa cha ubora  katika utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa usalama wa usafiri wa anga yaani ISO 9001:2015 certification. Aidha, uboreshaji huo umewezesha kuongezeka kwa viwango vya usahihi wa utabiri wa hali ya hewa kutoka asilimia 78 mwaka 2015 hadi kufikia kati ya asilimia 82 na 96 mwaka 2020.

7.    Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameweka mazingira wezeshi yaliyoiwezesha TMA  kutekeleza jukumu lake la kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika masuala ya hali ya hewa kikanda na kimataifa kwa ufanisi na mafanikio makubwa. Aidha, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliidhinisha jina la Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi kugombea nafasi ya makamu wa tatu wa  Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ambapo alichaguliwa katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka minne kuanzia 2019 hadi 2023. Dkt. Agnes Kijazi ni mwanamke wa kwanza kutoka Bara la Afrika na nchi zinazoendelea kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo kubwa ya uongozi wa juu kabisa katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).

8.    Aidha, kipindi cha utawala wa Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli taarifa za kisayansi za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa nchini zimeboreshwa ambapo TMA inatoa jarida la mwenendo wa hali ya hewa nchini (Statement on the Status of Tanzania Climate). Jarida hili limesheheni taarifa muhimu ambazo zinasaidia katika mipango ya muda mrefu sambamba na utekelezaji wa dira ya nchi ya uchumi wa viwanda.

9.  Uboreshaji wa huduma za hali ya hewa zitolewazo na TMA alioufanya Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli umeimarisha uwezo wa Serikali katika kupunguza madhara ya majanga yanayosababishwa  na  matukio ya hali mbaya ya hewa. Aidha, uboresha wa huduma za hali ya hewa umeimarisha uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Kutokana na mafanikio haya na mengine mengi katika sekta ya hali ya hewa, matumizi ya taarifa za hali ya hewa zitolewazo na TMA yameongezeka katika kupanga shughuli za kiuchumi na kijamii hapa nchini.

10. Sambamba na mafanikio yaliyofikiwa, maboresho zaidi yanahitajika hususan kuongeza na kuboresha miundombinu ya vifaa vya upimaji na uchambuzi wa data za hali ya hewa; ufungashaji na elimu juu ya matumizi sahihi ya taarifa.  Katika kutekeleza hilo, TMA itaendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha matumizi sahihi ya huduma za hali ya hewa. Aidha, jitihada za Serikali pekee haziwezi kutatua changamoto zote za masuala ya hali ya hewa zinazoikabili jamii. Hivyo, jitihada zinahitajika pia kutoka kwa watumiaji na washirika wa huduma za hali ya hewa katika kuziboresha na kuhakikisha zinatumika ipasavyo.

Katika Siku hii ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka 2021, TMA inauenzi mchango mkubwa wa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alioutoa katika sekta ya hali ya hewa hapa nchini, na pia kikanda na kimataifa. Aidha, TMA itaendelea kuchapa kazi kwa bidii na kuwahudumia Watanzania wote ili kumuenzi shujaa wa uboreshaji wa sekta ya hali ya hewa Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuhakikisha uboreshaji alioufanya unakuwa endelevu. Pia, tunatoa wito kwa wadau wote wa huduma za hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na watumiaji wa bahari, wavuvi, wakazi wa maeneo ya fukwe na Mamlaka zinazohusika kuendelea kuzifuatilia na kuzitumia ipasavyo taarifa zitolewazo na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika mipango ya shughuli za kiuchumi na kijamii, na kuchukua hatua stahiki ambazo zitasaidia kupunguza madhara ya majanga na hatimaye kuongeza kasi ya ujenzi na maendeleo ya Taifa letu. TMA inakaribisha mashirikiano katika utekelezaji wa Mfumo wa Kitaifa wa Huduma za Hali ya Hewa (National Framework for Climate Services) na programu zingine za kuboresha huduma za hali ya hewa nchini ambazo Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ametuachia, wadau wote tuzitekeleze kwa ufanisi ikiwa ni sehemu ya kumuenzi shujaa huyu wa uboreshaji wa sekta ya hali ya hewa hapa nchini.

Maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani (WMD) kwa mwaka 2021 yanaongozwa na kaulimbiu ya “Mchango wa bahari katika hali ya hewa”-(The Ocean, Our Climate and Weather).  Kaulimbiu hii inalenga kufafanua umuhimu na uhusiano kati ya bahari, hali ya hewa, na athari zake kwa shughuli za kichumi na kijamii za kila siku.

Mchango wa bahari katika hali ya hewa umetokana na uhusiano mkubwa uliopo kati ya bahari na anga ambapo umesababisha kuona ulazima wa kuelewa kwa kina tabia na mwenendo wa bahari ili kutoa utabiri wa hali ya hewa kwa usahihi. Moja ya uhusiano muhimu kati ya bahari na anga, ni uwezo wa bahari kusharabu nishati ya jua inayofanikiwa kufika katika uso wa Dunia kwa kiasi kikubwa sana ambapo sehemu ya nishati hii huvukiza maji ya bahari na kutengeneza mawingu mengi na mazito, vimbunga na kusababisha mvua baharini na nchi kavu.

Utekelezaji wa programu mbalimbali za huduma za uangazi katika bahari umerahisisha upatikanaji wa data za hali ya bahari. Hivyo, uboreshaji wa miundombinu ya upimaji na ufuatiliaji wa hali ya anga na bahari, pamoja na uelewa wa kutosha wa mahusiano yaliyopo, unasaidia wanasayansi kutambua na kutabiri kwa urahisi zaidi viashiria muhimu vya bahari kwa hali ya hewa kama vile “El Niño” na “La Niña” hali ambazo huathiri hali ya hewa ya maeneo mengi na makubwa duniani ikiwa ni pamoja na Tanzania.  

Tanzania ni miongoni mwa Nchi 193 Wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ambao leo duniani kote wanaikumbuka siku hii muhimu ya kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Dunia mwaka 1950. Aidha, Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Prof. Petteri Taalas ametuma Salaam za Pole kwa Serikali, wana TMA na wananchi wote wa Tanzania kufuatia kifo cha Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambapo alisema Jumuia ya kimataifa imempoteza kiongozi mahiri aliyesimamia Amani na Maendeleo ya nchi yake. Wana TMA tuna ikumbuka siku hii tukiwa tumejawa na majonzi na simanzi kwa kuondokewa na shujaa wa uboreshaji wa huduma za hali ya hewa hapa nchini.

Maono ya Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa Sekta ya Hali ya Hewa Nchini yataendelea kuishi na Mchango wake Tutauenzi Daima.

PUMZIKA KWA AMANI SHUJAAWA UBORESHAJI WA HUDUMA ZA HALI YA HEWA.

“Mchango wa bahari katika hali ya hewa”-(The Ocean, Our Climate and Weather)”

 

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...