Dar
es Salaam; Tarehe 03/02/2021.
Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa
Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi, ameongoza mkutano wa pili
wa Jopo la Kamati Kuu ya WMO ya Kujenga Uwezo “Second Meeting of the WMO Executive
Council Capacity Development Panel (CDP-2)”.
Akizungumza
wakati akifungua rasmi mkutano huo, Dkt. Kijazi aliwataka wajumbe wa mkutano
huo, kuzingatia lengo lililokasimiwa kwa jopo la kushauri namna bora ya kujenga
uwezo katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa Duniani.
“Mkutano
huu umelenga kujadili taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Vikosi kazi
vinavyounda Jopo hili, na kuandaa mapendekezo ya kuwasilisha kwenye Kamati Kuu
ya WMO (WMO Executive Coincil (EC), na mapendekezo ya maeneo ya vipaumbele kwa
ajili ya kuandaa Mpango Mkakati wa kujenga uwezo (WMO Capacity Development
Strategy) katika utoaji huduma Kimataifa”. Alizungumza Dkt. Kijazi.
Katika
hatua nyingine, Dkt. Kijazi alimpongeza Katibu Mkuu wa WMO, Prof. Petteri
Taalas, kwa kupewa tuzo na jarida la “Reader’s
Digest Magazine” kama Mtu Mashuhuri wa Bara la Ulaya wa mwaka 2020 (European
of the Year), ikiwa ni kutambua mchango
wake wa kuongoza jitihada za WMO kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na
tabianchi.
Naye,
Prof. Taalas alimshukuru Dkt. Kijazi na kusema kuwa tuzo hiyo ni maalum kwa
wadau wote wa WMO na huduma za hali ya hewa kwa ujumla na alimpongeza Dkt. Kijazi kwa uongozi wake mahiri unaosaidia
kufanikisha utekelezaji wa malengo ya
WMO.
Mkutano huo ulifanyika kwa njia ya mtandao (teleconference)
Tarehe 3 na 4 Februari, 2021 chini ya Mwenyekiti wa Jopo hilo, Dkt. Kijazi na
kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa WMO, Prof. Petteri Taalas na watendaji wengine waandamizi
wa WMO. Mkutano ulijadili taarifa za Vikosi
kazi vinavyounda jopo hilo na kuandaa mapendekezo mbalimbali ya kujenga uwezo
katika huduma za hali ya hewa. Miongoni mwa mapendekezo hayo ni pamoja na yatakayowasilishwa
katika mkutano wa 73 wa Kamati Kuu ya WMO na
mapendekezo ya maeneo ya vipaumbele vitakavyotumika kuandaa Mpango
Mkakati wa WMO wa kujenga uwezo. Mjadala ulijielekeza kutambua kwamba hali ya
hewa haina mipaka hivyo katika kipindi hiki cha kuongezeka majanga
yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa jopo hilo lihakikishe vipaombele katika
kujenga uwezo vinaelekezwa kuzisadia nchi zinazoendelea pamoja na za Bara la
Afrika ili kuhakikisha maendeleo katika sekta ya hali ya hewa hayamuachi mtu yoyote
nyuma (no one should be left behind).
No comments:
Post a Comment