Tuesday, March 16, 2021

HALI YA MWENENDO WA MVUA ZA MASIKA, 2021


 Dar es Salaam, 16 Machi, 2021:

Taarifa kuhusu mwenendo wa mvua za Masika (Machi–Mei, 2021) kwa maeneo ya kaskazini mwa nchi ambayo hupata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

Utabiri wa mvua za Masika, 2021 ulionesha kuwa mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Viktoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma - wilaya za Kakonko na Kibondo) na nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro); na wastani hadi chini ya wastani katika maeneo ya pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba). Mvua hizi zilitarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya mwezi Februari, 2021 (nyanda za juu kaskazini mashariki na pwani ya kaskazini) na wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2021 (ukanda wa Ziwa Viktoria). 

Mvua zimeanza kunyesha wiki ya nne ya mwezi Februari katika maeneo machache ya Pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki. Aidha mvua hizo zimekuwa na mtawanyiko hafifu katika maeneo mengi kama ilivyotabiriwa. Kwa ukanda wa Ziwa Viktoria mvua zimeanza kunyesha wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2021 katika baadhi ya maeneo kama ilivyotarajiwa. 

Uwepo wa mgandamizo mkubwa wa hewa nchini pamoja na kujitokeza kwa migandamizo midogo ya hewa katika eneo la kusini magharibi mwa bahari ya Hindi kumesababisha Ukandamvua wa kitropiki kuendelea kusalia maeneo ya kusini na hivyo kusababisha vipindi vya ukavu katika maeneo mengi hususan maeneo ya kaskazini mwa nchi.  Hata hivyo, mvua za Masika zinatarajiwa kuendelea kunyesha wiki ya nne ya mwezi Machi, 2021 katika baadhi ya maeneo ya Ukanda wa ziwa Victoria pamoja na maeneo machache ya nyanda za juu kaskazini mashariki na pwani ya kaskazini.

Kwa taarifa hii wananchi wanashauriwa kuendelea kuzingatia taarifa na tahadhari za hali ya hewa zilizotolewa na zitakazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania sambamba na kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazotokana na hali mbaya ya hewa.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...