Thursday, September 2, 2021

MVUA ZA VULI 2021 ZINATARAJIWA KUANZA KWA KUSUASUA.

Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri - TMA, Dkt. Hamza Kabelwa mbele ya waandishi wa habari  akichambua  mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za Msimu wa Vuli Oktoba - Desemba 2021


Bw. Ramadhan Omary akitoa tathmini ya mvua za msimu wa Masika 2021, kabla ya kutolewa rasmi mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2021.


Washiriki mbalimbali wakiwa kwenye mkutano wa wanahabari wa kutoa mwelekeo wa mvua za Msimu wa Vuli Oktoba - Desemba 2021.

 

Dar es Salaam, 02/09/2021;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za VULI 2021 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka. Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Huduma za utabiri Dkn. Hamza Kabelwa alisema Utabiri huu ni mahsusi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Nyanda za juu kaskazini mashariki, Pwani ya kaskazini, Ukanda wa Ziwa Viktoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma).

Dkt Kabelwa alisema, Msimu wa mvua za Vuli unatarajiwa kuanza kwa kusuasua katika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Oktoba 2021 ukiwa na mtawanyiko na muendelezo usioridhisha katika maeneo mengi. Aidha, Mvua za Vuli zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani na zinatarajiwa kuambatana na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo mengi yanayopata mvua za Vuli.

Akizungumza kuhusu athari zinazotarajiwa kujitokeza, Dkt. Kabelwa  alisema upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi, magonjwa ya mlipuko kutokana upungufu wa maji safi na salama, upungufu wa malisho na maji unaweza kujitokeza hali ambayo inaweza kuleta uwezekano wa kutokea migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

“Matukio ya moto katika mapori na misitu yanategemewa kutokea, hivyo mamlaka husika zinashauriwa kupanga mikakati mahsusi ya kukabiliana na hali hiyo kutokana na maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani, japo izingatiwe kuwa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanaweza yakajitokeza katika maeneo machache”. Aliongezea Dkt. Kabelwa

Utabiri wa msimu wa mvua za vuli 2021 unapatikana katika ofisi zote za TMA nchini pamoja na mitandao ya mawasiliano kama vile TMA online TV, tovuti, blog, facebook na Instagram. 

Kwa taarifa zaidi tembele: https://www.meteo.go.tz/news/mvua-za-vuli-2021-zinatarajiwa-kuanza-kwa-kusuasua

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...