Dar es Salaam, Tarehe:
31/08/2021
“Ili taarifa hizi za
utabiri zilizoandaliwa kwa kila wilaya, ziwe na tija iliyokusudiwa tunahitaji
kuipatia Mamlaka ushirikiano mzuri katika kuhakikisha taarifa hizi
zinawafikia watumiaji wa mwisho kwenye sekta mbalimbali ili kuchangia ukuaji wa
uchumi hapa nchini”, Makamu Mwenyekiti
wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Makame O. Makame
alisisitiza hayo wakati akifungua rasmi mkutano wa wadau wa utabiri wa msimu wa
mvua za vuli (Oktoba hadi Disemba) 2021 uliofanyika katika ukumbi wa mikutano
wa ‘Law School’, Dar es Salaam.
Aidha, Dkt. Makame aliendelea kusisitiza kuwa taarifa za hali ya hewa
zinalenga kusaidia nchi kufikia malengo ya Mpango wa Taifa katika kujenga
uchumi wa viwanda katika eneo la uzalishaji mazao ya chakula na biashara,
nishati na maji. Alisema huduma za hali ya hewa zikitumika ipasavyo zitasaidia
upatikanaji wa malighafi na nishati kwa viwanda hapa nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Agnes Kijazi amesema kuwa Mkutano huu ni muhimu sana kwa wataalam wa hali ya
hewa katika kujifunza kwa undani na kuongeza uelewa wa matumizi sahihi ya
taarifa za hali ya hewa katika sekta mbalimbali na hivyo kuendelea kuboresha
taarifa zinazotolewa na Mamlaka.
Aidha Dkt. Kijazi aliwakumbusha wadau kuwa TMA inaendelea kufanya
utafiti kujua mwenendo wa mvua za mawe zilizojitokeza hivi karibuni katika
baadhi ya maeneo hapa nchini, ambapo utafiti huo utasaidia kuboresha utabiri ili
kupunguza au kuepusha athari zitokanazo na mvua hizo za mawe.
Sekta ambazo
zilipata fursa ya kuchangia jinsi walivyoutumia utabiri wa Masika (Machi hadi
Mei, 2021) ni pamoja na; Sekta ya Kilimo ambao walisema mazao ya mizizi yaliendelea
vizuri katika msimu husika. Sekta ya Maafa walielezea namna utabiri ulivyoleta
ufanisi katika njia za kukabiliana na maafa na hivyo kupunguza maafa, Sekta ya
afya ambao walisema utabiri ulitumika kwa manufaa katika sekta hiyo. Kwa upande
wa Sekta ya Mifugo walisema, miundo mbinu ya ufugaji iliboreshwa ili
kukabiliana na athari ambazo zingeweza kujitokeza na Sekta ya Nishati kwa
upande wa tafiti za mafuta walisema miradi ya tafiti hizo inaendelea kutumia
taarifa za hali ya hewa.
No comments:
Post a Comment