Monday, March 23, 2020

UJUMBE WA DKT. AGNES KIJAZI MKURUGENZI MKUU WA TMA NA MAKAMU WA TATU WA RAIS WA WMO KATIKA WMD 2020.

Leo ni siku ya Hali ya Hewa Duniani (the World Meteorological Day-WMD), siku ambayo Jumuiya ya Hali ya Hewa duniani kote inaadhimisha kumbukizi la siku ambayo Mkataba wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ulisainiwa mnamo tarehe 23 Machi, 1950. Kwa kawaida siku hii huadhimishwa na kila Nchi mwanachama wa WMO na kuratibiwa na Taasisi za Hali ya Hewa za nchi husika. Taasisi hizo hutumia siku hii kuonyesha na kueleza huduma wanazotoa katika kuhakikisha usalama wa watu na mali zao dhidi ya athari zitokanazo na hali mbaya ya hewa.
Kwa hapa nchini kwetu Tanzania, shughuli zote zinazohusiana na masuala ya hali ya hewa husimamiwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA). TMA ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 2019 kwa mujibu wa sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019 kabla ya hapo taasisi hii ilikuwa ni wakala wa serikali.

Katika kusisitiza na kuhamasisha umuhimu wa huduma za hali ya hewa katika mipango na maamuzi kwenye sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii, sherehe za WMD zimekuwa zikiadhimishwa kwa kaulimbiu maalumu, ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni “Hali ya Hewa na Maji (Climate and Water)”. Kaulimbiu hii inaenda sambamba na kaulimbiu ya Siku ya Maji Duniani kwa mwaka 2020, ambayo imejikita katika athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye sekta ya maji.
Kwa kawaida maji yapo katika hali mbalimbali ambazo ni yabisi (barafu), kimiminiko (maji ya kawaida) na gesi (mvuke). Hali hizo zinatokana na mzunguko ambao maji hupitia ujulikanao kama hydrological cycle unaohusisha ardhi, anga, bahari, maziwa, misitu na mazingira mengine. Ongezeko la joto duniani (global warming) linasababisha changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na limeathiri kwa kiasi kikubwa mifumo ya mzunguko wa maji kutokana na kubadilika kwa mifumo ya mikondobahari, mvukizo wa anga, ufanyikaji wa mawingu na mtiririko wa maji kwenye uso wa dunia. Athari hizo zinatokana na uhusiano uliopo wa moja kwa moja wa mifumo ya hali ya hewa na mzunguko wa maji. Changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa imeathiri pia upatikanaji na ubora wa maji na kupelekea upungufu wa maji yanayohitajika kwa matumizi katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii.

Aidha, miongoni mwa athari za mabadiliko ya hali ya hewa ni ongezeko la kina cha bahari Duniani kote. Hii husababishwa na mambo makubwa mawili: kwanza, ni kutanuka kwa maji ya bahari kutokana na kuongezeka kwa joto la maji, na pili ni kuyeyuka kwa barafu katika maeneo yenye barafu, hususan katika uzio wa actic na antaktika. Ongezeko hilo la kina cha bahari linahatarisha miundombinu, mazingira na maisha ya jamii zinazoishi maeneo ya fukwe za bahari na visiwa, na kuathiri ubora wa maji kwa kusababisha mwingiliano wa majichumvi na vyanzo vya maji baridi hali inayopelekea hitaji la kutumia teknolojia yenye gharama kubwa kusafisha maji hayo ili kuyafanya bora na yanayofaa kwa matumizi ya binadamu.

Inatazamiwa kuwa, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, matukio ya mafuriko na ukame yataongezeka kwa wingi (frequency) na ukubwa (intensity) na hivyo kusababisha athari katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo sekta ya maji, nishati, usafirishaji na kilimo.
Pamoja na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, na athari zake katika mfumo wa mzunguko na upatikanaji wa maji, taarifa za hali ya hewa za sehemu husika zitasaidia katika kupanga shughuli za kiuchumi na kijamii zinazotegemea upatikanaji wa maji.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatekeleza Programu ya Kitaifa ya Huduma za Hali ya Hewa “the National Framework for Climate Services (NFCS)”, ambayo ina malengo ya kuboresha huduma za hali ya hewa katika sekta zilizoathiriwa zaidi na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa (climate sensitive sectors) ikiwemo sekta ya maji.

Katika kutimiza mahitaji ya wadau na matakwa ya program ya NFCS pamoja na sheria iliyoanzisha TMA, Mamlaka ya Hali ya Hewa hufanya shughuli za uangazi wa masuala ya hali ya hewa. TMA hufanya uangazi kupitia mtandao wake wa vituo vya hali ya hewa vilivyopo nchi nzima, ambavyo vinajumuisha vituo vilivyopo kwenye uso wa dunia nchi kavu (ground weather stations), vilivyopo bandarini (marine weather stations) na vilivyopo katika anga la juu ambavyo vinajumuisha mtando wa RADAR (upper air stations).

Aidha, TMA hutoa utabiri wa hali ya hewa unaotumika katika mipango kwaajili ya shughuli za kijamii na kiuchumi. Utabiri unaotolewa na TMA ni pamoja na utabiri wa kila siku (saa 24), siku tano, siku kumi (dekadal forecast), mwezi, msimu na tahadhari za hali mbaya ya hewa (severe weather warnings and alerts). Tabiri hizi za hali ya hewa ni kwa jamii yote kwa ujumla, zikiwa na ushauri unaolenga sekta ambazo shughuli zake hutegemea zaidi hali ya hewa na maji. Aidha, TMA hutoa taarifa mahsusi kwa sekta mahsusi kama vile sekta ya usafiri wa anga na usafiri wa kwenye maji. Utabiri huu husambazwa kwa njia mbalimbali zikiwemo tovuti ya TMA (www.meteo.go.tz), radio, runinga, mitandao ya kijamii (facebook, twitter, Youtube, na WhatsApp), magazeti na mfumo wa kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa njia ya simu za mkononi (FarmSMS).

TMA imeendelea kupata mafanikio zaidi katika kutekeleza mpango mkakati wake. Mafanikio hayo ni pamoja na kutekeleza kikamilifu Mpango wa Huduma Bora “Quality Management System (QMS) na kuendelea kumiliki cheti cha ubora wa huduma kutoka Shirika la Viwango Duniani (ISO 9001:2015 Certification) katika huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga.

Katika eneo la vifaa vya hali ya hewa, TMA imeendelea na mkakati wake wa kuboresha vifaa kwa kununua vifaa vya kisasa na kuondoa vifaa vinavyotumia zebaki. Mkakati huu umelenga kuboresha vituo vyote vya hali ya hewa nchini ili kuendana na ukuaji wa teknolojia ya hali ya hewa duniani, na pia kutekeleza mkataba wa Minamata (Minamata Convention) unaozitaka nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa kusitisha matumizi ya zebaki kabla ya kumalizika mwaka huu wa 2020.

Hata hivyo pamoja na mafanikio yaliyofikiwa, bado kuna changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji jitihada za wadau wote wa huduma za hali ya hewa, wakiwemo wadau wa maendeleo “Development Partners (DPs)” ili kuunga mkono na kuendeleza jitihada za Serikali. Changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa vituo vya uangazi wa hali ya hewa, mabadiliko ya matumizi ya teknolojia katika huduma za hali ya hewa, mahitaji ya taarifa za sekta maalumu na maeneo madogomadogo (downcaled information) na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi katika misimu ya mvua ambayo husababisha ongezeko la matukio ya hali mbaya ya hewa.

Katika kuadhimisha siku ya Hali ya Hewa Duniani Kwa mwaka huu wa 2020, napenda kutoa wito kwa wadau wote wa huduma za hali ya hewa kutoka katika sekta zote za kiuchumi na kijamii kuhakikisha wanazielewa na kuzitumia ipasavyo huduma za hali ya hewa katika kupanga mipango ya kiuchumi na kijamii kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Taifa letu. Napenda pia kuwaomba wadau wote kutuunga mkono katika utekelezaji wa Programu ya Kitaifa ya Huduma za Hali ya Hewa (NFCS) ili kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa hapa nchini na kupunguza athari kwa jamii na sekta ambazo zinaathiriwa moja kwa moja na mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo sekta ya maji.

Mwisho, nawatakia maadhimisho mema ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani “World Meteorological Day” (WMD) 2020 yenye kauli mbiu “Hali ya Hewa na Maji (Climate and Water)”

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...