Thursday, March 12, 2020

KATIBU MKUU UCHUKUZI AITAKA TMA KATIKA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE YA UDHIBITI WA HUDUMA ZA HALI YA HEWA NCHINI IHAKIKISHE INAONGEZA MAPATO.

Menejiment ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika picha ya pamoja na mgeni rasmi ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi. Leonard Chamuriho wakati wa mafunzo ya udhibiti na ukusanyaji wa mapato, Dodoma.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Agnes Kijazi akitoa maelezo ya awali kwa mgeni rasmi wakati wa mafunzo ya udhibiti na ukusanyaji wa mapato, Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Uchukuzi) Mhandisi. Leonard Chamuriho, akizungumza na Menejiment ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) wakati wa mafunzo ya udhibiti na ukusanyaji wa mapato, Dodoma.

Meneja Mafunzo kutoka Wakala wa Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA) Bw. Brown Hasunga akitoa maelezo ya mafunzo wakati wa mafunzo ya udhibiti na ukusanyaji wa mapato, Dodoma.


Mwezeshaji kutoka Wakala wa Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA) Bw. Felix Ngamlagosi akielezea jambo wakati wa mafunzo ya udhibiti na ukusanyaji wa mapato, Dodoma.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya udhibiti na ukusanyaji wa mapato, Dodoma.

Dodoma, Tarehe: 09/03/2020;
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Uchukuzi) Mhandisi. Leonard Chamuriho ameagiza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuongeza kasi ya udhibiti na ukusanyaji wa mapato. Hayo yalizungumzwa wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Udhibiti na Ukusanyaji wa Mapato, Dodoma, Tarehe 9 Machi 2020.

Mhandisi Chamuriho aliipoongeza TMA kwa kazi nzuri ya kutoa taarifa sahihi na kwa wakati na kuwatendea haki watanzania, hivyo kuwataka jitihada hizo ziwekwe pia katika majukumu mapya ya TMA ya kudhibiti huduma za hali ya hewa hapa nchini.

Nachukua fursa hii kuwapongeza na kutoa maelekezo kwamba jitihada hizo zihamie pia katika ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa utoaji wa huduma za hali ya hewa hapa nchini”. Alisema Mhandisi Chamuriho.

Aliendelea kwa kusema kuwa jukumu la udhibiti linagaharama, gharama hizo ni kuwa na mapato ya Taasis au kupata ruzuku serikalini lakini kwa hili naona TMA imejipanga kwa kuongeza vyanzo vya mapato kwa maeneo ambayo huduma zinatolewa kibiashara. 
“Mimi ni mhandisi, na tunatambua ujenzi wa majengo marefu unategemea taarifa za hali ya hewa, kwahiyo itakuwa vizuri kwa wahusika kulipia gharama hizo ili kuweza kurudisha gharama zinazotumika katika kuziandaa taarifa za hali ya hewa mahususi kwa  ajili ya ujenzi”. Aliongezea Mhandisi. Chamuriho
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi alielezea lengo la mafunzo hayo kwa mgeni rasmi, ambayo yameandaliwa mahususi kwaajili ya menejimenti ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
“Lengo  la mafunzo haya ni kuongeza uelewa kwa menejimenti wa jukumu la udhibiti wa huduma za hali ya hewa hapa nchini na pia ukusanyaji wa mapato yatokanayo na huduma za kibiashara zinazotolewa na TMA”. Alieleza Dkt. Kijazi
Aliendelea kufafanua kuwa mafunzo haya yamekuja kwa wakati muafaka na yana lengo la kuweka msingi imara kwa TMA kuhusu udhibiti wa shughuli za hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa mapato kulingana na matakwa ya sheria ya TMA Na. 2 ya mwaka 2019.
Awali, Meneja Mafunzo kutoka Wakala wa Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA), Ndugu, Brown Hasunga alieleza kwa kifupi kinachoenda kufanyika katika wiki hiyo ya mafunzo kuwa ni kutoa mafunzo ya kuangalia suala zima la udhibiti kwa kufuata sheria na taratibu, masuala ya msingi ya jukumu la TMA kwa kutambua nyenzo za kutumika na utendaji wake, vilevile washiriki wataangalia suala la upangaji bei na tozo zake.
Mafunzo hayo yameandaliwa na TMA kwa kushirikiana na TaGLA, yamejumuisha viongozi kutoka katika ofisi za TMA zilizoko kwenye kanda nane za Mamlaka ikiwa pamoja na Ofisi ya Zanzibar na yanatarajiwa kuwaongezea uwezo viongozi hao kwa kuendelea kutoa huduma bora zaidi ambazo zinakidhi mahitaji ya wadau mbalimbali wanaotumia huduma za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...