Monday, March 23, 2020

KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI, MHE. MHANDISI ISACK KAMWELWE ATOA WITO KWA WADAU WOTE WA HALI YA HEWA.

Kila mwaka tarehe 23 Machi, Jumuiya ya kimataifa ya hali ya hewa duniani kote inaadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani. Siku hii ni kumbukumbu ya kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization-WMO) ambalo lilianzishwa tarehe 23 Machi, 1950. Tanzania pamoja na wanachama wengine 192 wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani inaungana na jumuiya ya kimataifa kusherehekea Siku ya Hali ya Hewa Duniani. Siku hii pia hutumika kuonesha mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za hali ya hewa ikiwemo Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika kuchangia maendeleo na kukuza ustawi wa jamii. Taasisi za Hali ya Hewa duniani kote hutoa tahadhari za hali mbaya ya hewa ambazo ni muhimu kwa usalama wa watu na mali zao.

Katika kusherehekea siku ya hali ya hewa duniani, ni desturi kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kutoa kaulimbiu ya maadhimisho ya kila mwaka. Kwa mwaka huu wa 2020 kaulimbiu ya maadhimisho haya ni “Hali ya Hewa na Maji” (Climate and Water). Kaulimbiu hii inaelezea ukweli kwamba, hali ya hewa ina mchango mkubwa katika mtawanyiko, mgawanyo, ubora na matumizi ya rasilimali maji katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii kama vile kilimo, nishati, mifugo na uvuvi. Pia kwa kuzingatia kuwa mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi pamoja na matukio ya hali mbaya ya hewa inayoambatana na mabadiliko hayo yanaathiri sana mzunguko wa maji wa Dunia pamoja na upatikanaji na ubora wa maji.

Kwa upande wa Tanzania, kama ilivyo kwa wanachama wengine wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ina jukumu la kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa utabiri wa hali ya hewa ambao huchangia kulinda vyanzo vya maji na hivyo kuboresha upatikanaji wa rasilimali maji. Upatikanaji wa rasilimali maji ni muhimu katika kuchangia maendeleo ya Taifa na malengo ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo endelevu (Sustainable Development Goals-SDGs). Huduma za hali ya hewa ni muhimu katika malengo hayo hususani lengo Na. 7 (SDG7) ambalo linahusiana na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.
Tanzania inaendelea kutekeleza maridhiano ya kimataifa katika sekta ya hali ya hewa kwa kuhakikisha Mamlaka ya Hali ya Hewa inatoahuduma za hali ya hewa katika viwango vinavyokubalika kimataifa. Hii ni pamoja na kuijengea uwezo Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa upande wa vifaa na wataalam ili kuhakikisha wanafuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazohitajika nchini, kikanda na kimataifa kwa matumizi ya sekta zote ikiwemo sekta ya maji. Mwaka 2019, Serikali ilipitisha sheria ya kuhuisha Wakala wa Hali ya Hewa nchini kuwa Mamlaka kwa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na. 2 ya 2019. Sheria hii inaiwezesha Mamlaka kutekeleza majukumu yake kitaifa, kikanda na kimataifa na kutoa huduma za hali ya hewa kwa jamii ambazo zina mchango mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi. Pia sheria iliyounda Mamlaka ya Hali ya Hewa inaipa nguvu za kisheria za kudhibiti huduma za hali ya hewa hapa nchini na kukusanya mapato yanayotokana na matumizi ya huduma za hali ya hewa zinazotumiwa kibiashara. Aidha, Sheria hiyo inaitambua Serikali kama mdau mkubwa wa huduma zinazotolewa kwa matumizi ya wananchi (Public Good) hususan tahadhari za hali mbaya ya hewa. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inatarajiwa kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa nchini, hivyo sheria hii imehakikisha uwakilishi, ushirikishwaji, mabadiliko ya kimtazamo na uwajibikaji wa wadau wote ikiwa ni pamoja na sekta binafsi na jumuiya za kijamii.
Katika kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi ili kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii hapa nchini, Serikali inaendelea kuijengea uwezo Mamlaka hii ili iweze kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kuboresha utabiri wa hali ya hewa kwa lengo la kufuatilia mabadiliko ya hali ya hewa ya muda mfupi na muda mrefu (climate variability and change). Taarifa za hali ya hewa ni za muhimu sana katika kutoa maamuzi na kuweka mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Taarifa na huduma za hali ya hewa husaidia na kuongeza uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na vilevile kuchangia katika maendeleo endelevu na hivyo kuliandaa taifa vizuri katika kukabiliana na maafa yanayosababishwa na vipindi vya ongezeko au upungufu wa maji kama vile mafuriko na ukame. Mfano wa uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na mafuriko ni pamoja na mvua kubwa zilizonyesha katika msimu huu na kuharibu miundominu ya usafiri ikiwemo miundombinu ya reli, barabara na madaraja. Hivyo, huduma za hali ya hewa zitolewazo husaidia watumiaji wa huduma hizo kupanga vyema shughuli zao ambazo ni pamoja na mipango ya utoaji wa huduma za maji mijini, kilimo, mifugo, maendeleo ya uvuvi, uzalishaji wa nishati, ujenzi wa miundombinu ya barabara na reli yakiwemo madaraja na uratibu wa maafa miongoni mwa sekta nyingine. Aidha, katika jitihada za kuboresha huduma za hali ya hewa nchini, Serikali imeendelea kuongeza uwezo wa TMA kwa kuboresha mtandao wa Taifa wa vituo vya upimaji wa hali ya hewa ili kuboresha upatikanaji wa data na usahihi wa utabiri wa hali ya hewa kwa matumizi katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii pamoja na kufanya maamuzi ya mipango ya maendeleo katika sekta hizo.

Kwa kuzingatia hatua kubwa ya maendeleo iliyopigwa katika nyanja ya teknolojia na mahitaji yake katika sayansi ya hali ya hewa, Serikali inaipongeza TMA kwa kuendeleza ubunifu na matumizi ya teknolojia katika kuboresha huduma wanazotoa hapa nchini. Kwa kutambua juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Juamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambapo imeboresha utendaji wa TMA katika utoaji wa huduma bora za hali ya hewa, hatuna budi kutumia huduma hizi ili kuboresha shughuli zetu za kila siku na vilevile kufanya kazi kwa pamoja ili kuendelea kuboresha huduma hizi kwa siku zijazo.
Uwekezaji wa Serikali katika utoaji wa huduma za hali ya hewa hususani katika kuboresha miundombinu ni pamoja na ununuzi wa Rada za hali ya hewa kwa lengo hilo hilo la kuboresha upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa nchini. Rada hizo zimefungwa Mwanza na Dar es Salaam na zingine tatu ziko katika hatua ya ununuzi ambazo zitafungwaMtwara, Mbeya na Kigoma. Aidha, ili kukamilisha mtandao wa Rada zitahitajika Rada zingine mbili ambazo zitafungwa Dodoma na Kilimanjaro. Pia kwa kutambua ongezeko la uhitaji wa huduma za hali ya hewa na changamoto zinazotukabili ambazo zinahitaji kutatuliwa, Serikali itaendelea kuwekeza ili kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa na maji kwa kuongeza uwezo wa wataalamu na miundombinu huku tukihimiza ushirikiano baina ya sekta mbalimbali zinazohusiana na zinazotumia huduma za hali ya hewa na rasilimali maji kwa lengo la kuendelea kuboresha maisha na ustawi wa jamii. Vilevile kwa kuzingatia maboresho yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika katika utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini, ni vyema kuongeza juhudi katika kutumia huduma hizi katika mipango ya sekta zote za kiuchumi na kijamii na utekelezaji wa miradi ya kitaifa kama vile ujenzi wa miundombinu, uendelezaji na uzalishaji wa nishati inayotokana na maji, kilimo na rasilimali maji.

Katika kuadhimisha Siku hii ya hali ya hewa Duniani yenye kauli mbiu “Hali ya Hewa na Maji” (Climate and Water), ninatoa wito kwa wadau wote wa huduma za hali ya hewa kutoka sekta zote za kiuchumi na kijamii zinazotumia au kuathiriwa na hali ya hewa pamoja na wananchi kwa ujumla kuhakikisha wanazitumia huduma za hali ya Hewa kwa maendeleo ya Taifa letu. Sekta ya maji izitumie huduma za hali ya hewa katika kupanga mipango yao ili kwenda sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu. Aidha, tuendelee kuunga mkono juhudi za TMA katika utekelezaji wa majukumu yao ya utoaji wa huduma za hali ya hewa pamoja na udhibiti kwa kuendelea kuwapa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wote wenye vituo vya hali ya hewa wanavinasajili TMA ili kwenda sambamba na matakwa ya sheria. Ushirikiano huo utaiwezesha TMA kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa hapa nchini.

Mwisho nachukua fursa hii kuwatakia wananchi wote pamoja na jumuia yote ya kimataifa maadhimisho mema na yenye mafanikio ya siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka huu wa 2020.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...