Dar
es Salaam, 12 Machi 2020:
Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa kuhusu mvua za msimu wa masika
(Machi – Mei) zinazoendelea hususan katika maeneo yanayopata misimu miwili ya
mvua kwa mwaka, yaani (Ukanda wa Ziwa Viktoria, nyanda za juu kaskazini
mashariki pamoja na pwani ya kaskazini). Mvua katika maeneo haya zimeanza vizuri
kama ilivyotarajiwa katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Machi, 2020.
Katika
hatua nyingine, mvua kubwa zilizojitokeza zimesababishwa na uwepo wa joto la
bahari kuwa juu ya wastani mfululizo kuanzia mwezi Oktoba, 2019 hadi sasa na
pia kuimarika kwa ukanda mvua (ITCZ) sambamba na kujitokeza kwa migandamizo
midogo ya hewa katika Bahari ya Hindi na hivyo kumeongeza viwango vya mvua zinazonyesha
katika muda mfupi.
Aidha,
hali hiyo ya kuimarika kwa ukanda mvua (ITCZ) pamoja na uwepo wa mgandamizo mdogo
wa hewa (Depression) Kaskazini Mashariki mwa kisiwa cha Madagascar inaendelea
kusababisha ongezeko la mvua katika maeneo mengi nchini katika kipindi hiki. Sambamba
na hayo, ongezeko la mvua linatarajiwa kwa kiwango cha juu katika mwezi Machi
na Aprili 2020, na kutarajiwa kupungua katika mwezi Mei kwa maeneo yanayopata misimu
miwili ya mvua kwa mwaka (maeneo ya kaskazini mwa nchi).
Kwa
upande mwingine, mvua za MSIMU zilizoanza mwezi Novemba, 2019 katika maeneo
yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka(maeneo ya kusini, kati na magharibi
mwa nchi) zinatarajiwa kuendelea hadi mwezi Aprili, 2020.
TMA
inaendelea kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa mrejesho kadri mabadiliko
yatakavyokuwa yanajitokeza.
ATHARI: Wakati
wa kuandaa utabiri wa msimu wa mvua za Masika, 2020, TMA iliwashirikisha wadau
kwa kiasi kikubwa. Wadau hao walionesha kwamba mvua zinazoendelea kunyesha
zitakuwa na athari katika sekta nyingi za kiuchumi na kijamii. Baadhi
ya athari zinazotarajiwa kutokana na vipindi vya mvua kubwa vinavyoambatana na
upepo mkali ni pamoja na uharibifu wa mazao, milipuko ya magonjwa ya binadamu,
wanyama na mimea, mafuriko, uharibifu wa miundo mbinu n.k. Aidha, wataalam
katika sekta husika wana utaalam wa kutosha kutathmini kwa weledi zaidi athari
zinazoweza kujitokeza kutokana na vipindi vya mvua kubwa vinavyoendelea
kujitokeza katika msimu huu wa mvua.
USHAURI:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inawashauri watumiaji wa taarifa hii ikiwa
ni pamoja na wakulima, wafugaji, Mamlaka za Wanyamapori, Wasafirishaji, Mamlaka
za Maji na Afya kuendelea kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam
katika sekta husika. Pia kuendelea kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi
pamoja na tahadhari kila zinapotolewa na kuchukua hatua.
No comments:
Post a Comment