Thursday, August 29, 2019

TMA YAONGEZA NGUVU KATIKA UTOAJI HUDUMA KUWAFIKIA WANANCHI

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi wakati akifungua rasmi uzinduzi wa programu ya Huduma za Hali ya Hewa kwa Afrika (Weather Information and Services for Africa (WISER) Kitaifa “WISER National Project” katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, Tanzania.
Mratibu wa programu ya WISER kwa Nchi za Afrika Mashariki, Ndugu. John Mungai akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu ya Huduma za Hali ya Hewa kwa Afrika (Weather Information and Services for Africa (WISER) Kitaifa “WISER National Project” katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, Tanzania.
Rais wa TMS Dkt. Burhani Nyenzi akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu ya Huduma za Hali ya Hewa kwa Afrika (Weather Information and Services for Africa (WISER) Kitaifa “WISER National Project” katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, Tanzania.


Wadau mbalimbali wakizungumza wakati wa uzinduzi wa programu ya Huduma za Hali ya Hewa kwa Afrika (Weather Information and Services for Africa (WISER) Kitaifa “WISER National Project” katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, Tanzania.
Baadhi ya washiriki katika picha kwenye uzinduzi wa programu ya Huduma za Hali ya Hewa kwa Afrika (Weather Information and Services for Africa (WISER) Kitaifa “WISER National Project” katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, Tanzania.
Mgeni rasmi Dkt. Agnes Kijazi (katikati ya waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa mkutano wakati wa uzinduzi wa programu ya Huduma za Hali ya Hewa kwa Afrika (Weather Information and Services for Africa (WISER) Kitaifa “WISER National Project” katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, Tanzania.

Tarehe 29/08/2019 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Chama cha Wataalam wa Hali ya Hewa Tanzania (TMS) kupitia programu ya “Weather and Climate Information Services” (WISER), imejipanga katika kuongeza nguvu ya utoaji hudumza za hali ya hewa ili kufikia wananchi wengi zaidi.

Hayo yalizungumzwa na mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi wakati akifungua rasmi uzinduzi wa programu ya Huduma za Hali ya Hewa kwa Afrika (Weather Information and Services for Africa (WISER) Kitaifa “WISER National Project” katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, Tanzania.

‘Programu hiyo itaiwezesha Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kusambaza taarifa za hali ya hewa pamoja na kuelimisha wadau mbalimbali juu ya matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa hususan katika sekta za Kilimo, Usafiri majini, Udhibiti wa majanga, Maji na Nishati hivyo itaongeza nguvu katika kuwafikia wananchi wengi’,alizungumza Dkt. Kijazi.

Aidha, aliendelea kueleza kuwa madhumuni makubwa ya program ya WISER Kitaifa ni kuhakikisha kunakuwa na matumizi sahihi ya tarifa za hali ya hewa katika sekta mbali mbali za maendeleo kwa lengo la kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Kwa upande wa mratibu wa programu ya WISER kwa Nchi za Afrika Mashariki, Ndugu. John Mungai alieleza kuwa lengo la warsha ya uzinduzi huo ni kuwakutanisha wadau na kuwa na uelewa wa pamoja wa programu hii pia kutoa taarifa ya kuanza kwa utekelezaji wake kwa wadau wanaohusika katika program hii.

Awali Rais wa TMS Dkt. Burhani Nyenzi aliwajulisha washiriki kuwa tayari utekelezaji wa awali umeanza kufanyika kwa kuwajengea uwezo wadau wa sekta husika pamoja na wanahabari katika mikoa ya Dodoma, Simiyu, Tanga na Manyara.

Programu hii inafadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia Shirika lake la Kimataifa la maendeleo (DFID) na ulijumuisha wadau mbalimbali wakiwemo wizara na taasisi za serikali, taasisi zisizo za kiserikali (NGO), mashuleni, watendaji wa vijiji na wanahabari.

Monday, August 26, 2019

WAZIRI KAMWELWE AHIMIZA MIPANGO MADHUBUTU YA KUKABILIA NA ATHARI ZA MABADILIKO YA HALI YA HEWA

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaack Kamwelwe akifungua  mkutano wa 53 wa utabiri wa msimu wa vuli kwa nchi 11 za pembe ya Afrika unaofanyika kwenye hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi akizungumza katika mkutano huo unaofanyika kwenye hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es salaam leo.
Meza Kuu




‘Tarehe 26/08/2019: Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mh. Mhandisi Isaack Kamwelwe amehimiza wanasayansi na wataalam wa sekta mbalimbali kuhakikisha wanafanikisha upatikanaji wa mipango madhubuti ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Alizungumza hayo wakati akifungua rasmi mkutano wa 53 wa utoaji wa utabiri wa Hali ya Hewa wa Msimu wa Mvua za Vuli 2019 "Fifty Third Greater Horn of Africa Climate Outlook Forum" (GHACOF 53) unaofanyika katika Hotel ya Kilimanjaro (Hyatt Regency) kuanzia tarehe 26 hadi 28 Agosti 2019 Dar es Salaam.

'Naamini baada ya mkutano huu wataalamu mliopo kwenye mkutano huu mtakuja na mpango madhubuti wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa ili kuweza kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko hayo’, alizungumza Mhe. Kamwelwe. 
 
Aidha, Mheshimiwa Kamwele aliwakumbusha wataalam hao kutoka nchi kumi na moja za pembe ya Afrika umuhimu wa kuhusisha utabiri wa jadi (Indigenous knowledge) katika kuboresha utabiri. Alisema kuna wadudu ambao wakionekana inaashiria kuanza kwa mvua na kuna ambao wakionekana inaashiria mvua si za kuridhisha, aliwataka wanasayansi hao kufanya uchambuzi wa kina. 
 
Sambamba na maelekezo hayo, Mheshimiwa Kamwele aliwakaribisha washiriki wa kongamano hilo kutembelea sehemu za vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini na aliwataka kujifunza maneno machache ya Kiswahili. 
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani, Dkt.Agnes Kijazi alimweleza mhe. Waziri kuwa kupitia mikutano hiyo kumekuwa na maboresho makubwa kwenye mfumo wa mawasiliano kati ya wanasayansi na wataalamu kutoka sekta mbalimbali hivyo kusaidia matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa zitolewazo na taasisi za hali ya hewa za nchi za Pembe ya Afrika. 
 
Pia, Dkt. Kijazi aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais John Joseph Pombe Magufuli kwa kutoa kipaombele katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa hapa nchini. 
 
Aliendelea kwa kusema kuwa uwekezaji unaofanywa na Serikali katika miundombinu ya hali ya hewa ukiwemo mtandao wa rada za hali ya hewa ni kielelezo tosha cha umakini wa serikali kuboresha sekta ya hali ya hewa ambayo ni ya muhimu sana katika kufikia maendeleo endelevu. 
 
Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa taasis za hali ya hewa katika nchi za pembe ya Afrika Dkt. Kijazi aliziomba serikali za nchi hizo kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa na pia aliwashukuru ICPAC kwa kuendelea kuendesha makongamano hayo ambayo alisema yameendelea kuwa chachu ya uboreshaji wa utabiri wa msimu katika nchi za pembe ya Afrika. 
 
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Taasis inayosimamia Masuala ya Hali ya Hewa kwa Nchi za Pembe ya Afrika (IGAD Climate Prediction and Application Centre (ICPAC)) Dkt. Guleid Artan alielezea lengo la kongamano hilo kuwa ni kujadili na kuandaa kwa pamoja utabiri wa msimu wa mvua za vuli za mwezi Oktoba hadi Desemba 2019, pamoja na kuandaa mikakati ya kukubaliana na hali mbaya ya hewa kwa msimu huo kwa kulenga sekta muhimu za kijamii na kiuchumi ambazo ni pamoja na afya, kilimo na usalama wa chakula, maji, nishati n.k. 
 
Mwakilishi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani, Dkt. Afiesimama aliwajulisha washiriki wa kongamano hilo kwamba katika mkutano wa WMO Congress uliomalizika hivi karibuni Afrika ilifanikiwa kuwa na mwakilishi katika ngazi za juu za uongozi wa Shirika hilo kupitia Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ambaye alichaguliwa katika nafasi ya Makamu wa tatu wa Rais wa WMO. Aidha, aliahidi kwamba WMO itaendelea kuzisaidia nchi wanachama kuboresha huduma zikiwemo nchi za pembe ya Afrika. 
 
Wengine waliozungumza katika ufunguzi wa Kongamano hilo ni mwakilishi wa Bank ya maendeleo ya Afrika Dkt. Solomon Ngoze ambae alielezea misaada mbali mbali iliyotolewa na Bank hiyo katika kuboresha huduma za hali ya hewa kwenye nchi za pembe ya Afrika.  Mwakilishi wa programu ya WISER Mr. Adam Curtis alielezea mafanikio yaliyofikiwa katika kutekeleza programu hiyo. Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Dkt. Buruhani Nyenzi aliwakumbusha washiriki hao kwamba kongamano la kwanza lilifanyika nchini Zimbabwe mwaka 1996 ambapo yeye binafsi alikuwa kiongozi wa taasisi iliyohusika na ukame kusini mwa Afrika ambayo ndiyo iliendesha kongamano hilo. Alionyesha furaha yake kuona kwamba makongamano hayo yanaendelea kwa ufanisi mkubwa. 
 

GHACOF ni Mkutano unaojumuisha nchi za Pembe ya Afrika ambazo ni Tanzania, Kenya, Somalia, Ethiopia, Sudan, Sudan ya Kusini, Uganda, Burundi, Rwanda, Djibouti na Eritrea pamoja na mashirika ya Kimataifa ikiwemo Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO). 
 

Friday, August 23, 2019

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA 53 WA UTOAJI WA UTABIRI WA HALI YA HEWA WA MSIMU WA MVUA ZA VULI 2019 KATIKA NCHI ZA PEMBE YA AFRIKA




Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano wa 53 wa Utoaji wa Utabiri wa Hali ya Hewa wa Msimu wa Mvua za Vuli 2019 “Fifty Third Greater Horn of Africa Climate Outlook Forum” (GHACOF 53) utakao fanyika katika  Hotel ya Kilimanjaro (Hyatt Regency) kuanzia tarehe 26 hadi 28 Agosti 2019 Dar es Salaam.

Lengo la mkutano huo ni kujadili na kuandaa kwa pamoja utabiri wa msimu wa mvua za vuli za mwezi Oktoba hadi Desemba 2019, pamoja na kuandaa mikakati ya kukabiliana na hali mbaya ya hewa kwa msimu huo kwa kulenga sekta muhimu za kijamii na kiuchumi ambazo ni pamoja na afya, kilimo na usalama wa chakula, maji, nishati n.k.

Mkutano huo utajumuisha nchi za Pembe ya Afrika ambazo ni Tanzania, Kenya, Somalia, Ethiopia, Sudan, Sudan ya Kusini, Uganda, Burundi, Rwanda, Djibouti na Eritrea

Sunday, August 18, 2019

MCHANGO NA USHIRIKI WA MAMLAKA YA HALI YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA) KATIKA JUMUIYA YA MAENDELEO KUSINI MWA AFRIKA (SADC) NA FAIDA ZINAZOPATIKANA KWA TAIFA KUPITIA SADC



Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ni miongoni mwa taasisi za serikali zinazowakilisha Tanzania kikanda na kimataifa katika masuala ya hali ya hewa. Aidha Tanzania kupitia TMA inashiriki katika kutekeleza itifaki ya SADC ya Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa na mpango mkakati wake kama ifuatavyo:
        i.            Ushiriki katika Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa za nchi za Kusini mwa Afrika “Meteorological Association of Southern Africa (MASA)”

Tanzania kupitia TMA ni mwanachama wa MASA. MASA ni Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa za nchi za Kusini mwa Afrika ulioanzishwa mwaka 1999. Umoja huu ulianzishwa kwa lengo la kushirikiana na kuratibu utekelezaji wa programu mbalimbali za hali ya hewa zinazotekelezwa katika ukanda wa SADC. Katika kutimiza jukumu hilo, wanachama wa MASA hufanya mikutano kila mwaka ili kujadili utekelezaji na kutoa mapendekezo kwa ngazi mbalimbali za maamuzi za  SADC. Katika Umoja huu, Tanzania kupitia TMA imechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa za nchi za SADC “SADC Meteorological Association of Southern Africa (SADC-MASA)” kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka huu wa 2019, kabla ya hapo Tanzania ilikuwa ikishika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa MASA tangu mwaka 2016.

Sambamba na nafasi hiyo, wataalamu wa TMA wamekuwa wakishiriki katika shughuli mbalimbali zenye lengo la kuimarisha ushirikiano na utengamano uliopo kati ya wanachama wa SADC ambazo ni pamoja na ukaguzi wa hesabu za fedha za MASA, kujengea uwezo kwa baadhi ya Taasisi za Hali ya hewa za nchi wanachama wa SADC katika eneo la utoaji wa huduma bora za hali ya hewa “ Quality Management System (QMS)” na mfumo wa utoaji wa tahadhari kutokana na hali mbaya ya hewa “ Common Alerting Protocol (CAP)”.

     ii.            Ushiriki katika Kamati ya Sekta ya Hali ya Hewa kwa nchi wanachama  wa SADC “Sub-Sectoral Committee on Meteorology (SCOM)”

Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekabidhiwa Uenyekiti wa Kamati ndogo ya Sekta ya Hali ya Hewa ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) “Sub-Sectoral Committee on Meteorology (SCOM) kwa kipindi cha mwaka mmoja. Kupitia mikutano inayofanyika kila mwaka ya SCOM, Mamlaka hushirikiana na Taasisi zingine za Hali ya Hewa za nchi wanachama wa SADC kujadili utekelezaji wa masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya hali ya hewa ambapo hutoa mapendekezo kwa ngazi za juu za SADC hivyo kuchangia katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa katika nchi wanachama wa SADC.

   iii.            Kongamano la nchi za kusini mwa Afrika la kuandaa utabiri wa msimu wa hali ya hewa“Southern Africa Regional Climate Outlook Forum (SARCOF)”

Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) hushiriki kongamano la wataalamu ili kuandaa utabiri wa kikanda wa msimu wa mvua kwa nchi wanachama wa SADC “Southern Africa Regional Climate Outlook Forum (SARCOF)”. Utabiri huu wa hali ya hewa huandaliwa kwa ushirikiano wa wataalamu wa taasisi za hali ya hewa na wadau wengine kutoka nchi wanachama wa SADC.

   iv.            Programu maalumu ya kuangalia hali mbaya ya hewa “Severe Weather Forecasting Demonstration Project SWFDP - Southern Africa”

Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inashiriki katika programu maalumu ya kufuatilia na kutoa taarifa za hali mbaya ya hewa (vimbunga, mafuriko, joto kali n.k) kwa nchi wanachama wa SADC hivyo kusaidia nchi kujipanga katika kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.


Faida zinazopatikana kwa Taifa kutokana na ushiriki wa TMA katika SADC
        i.            Kuboresha huduma za hali ya hewa kupitia mafunzo ya hali ya hewa yanayotolewa kwa nchi wanachama wa SADC kupitia programu mbalimbali za hali ya hewa.
     ii.            Kupatikana kwa baadhi ya miundombinu ya hali ya hewa inayotolewa kupitia programu na miradi ya hali ya hewa inayotekelezwa kwa nchi wanachama wa SADC.
   iii.            Kupata utabiri wa misimu ya mvua kwa ukanda wa SADC unaoandaliwa kwa ushirikiano wa wataalamu wa taasisi za hali ya hewa na wadau wengine kutoka nchi wanachama.
   iv.            Kupata taarifa za hali mbaya ya hewa kwa nchi wananchama ikiwemo Tanzania
      v.            Kupata ujuzi unaotokana na ushirikiano na kubadilishana uzoefu baina ya Taasisi za hali ya hewa za nchi wanachama wa SADC.
   vi.            Kuimarisha ushiriki na ushawishi wa Tanzania katika masuala ya hali ya hewa kikanda na kimataifa.

TMA IMEJIPANGAJE KUFIKIA AZMA YA MWENYEKITI YA UCHUMI WA VIWANDA KATIKA SADC?
i.                    Kutoa huduma bora za hali ya hewa zitakazosaidia upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda kama vile mazao.
ii.                 Kutoa huduma bora za hali ya hewa zitakazosaidia kuongeza ufanisi na tija katika ujenzi wa miundo mbinu ya viwanda na uendeshaji wa viwanda vyenyewe.
iii.               Tanzania kupitia TMA itaendelea kusaidia nchi zingine wanachama wa SADC katika kuboresha huduma za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na kuanzisha mifumo ya kiutendaji.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...