Taarifa hii inatoa mrejeo wa mwenendo
wa mgandamizo mdogo wa hewa uliopewa jina la “Kenneth” katika bahari ya Hindi na athari zake kwa maeneo
mbalimbali hapa nchini.
Katika kipindi cha saa 24 zilizopita, mgandamizo mdogo wa hewa (Kenneth) umeendelea kuimarika kwa kasi hadi kufikia kiwango cha kimbunga kamili. Kimbunga Kenneth kwa sasa kipo umbali wa takribani kilometa 700 mashariki mwa Mtwara. Mifumo ya hali ya hewa inaonesha kimbunga Kenneth kilichopo eneo la kaskazini magharibi mwa kisiwa cha Madagascar kinaambatana na mvua kubwa na upepo mkali katika eneo hilo. Aidha, vipindi vya upepo mkali unaofikia na kuzidi kasi ya kilometa 80 kwa saa vinatarajiwa kujitokeza katika ukanda wa pwani ya kusini (Lindi na Mtwara). Kimbunga hicho kinaendelea kutawala mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini, hivyo kusababisha ongezeko la mvua zinazoambatana na ngurumo za radi pamoja na upepo mkali kadri kinavyokaribia maeneo ya ukanda wa pwani.
Kimbunga
hiki kitakapoingia nchi kavu kikiwa na nguvu inayotarajiwa kitakuwa na madhara
makubwa kwa maisha ya watu na mali zao. Madhara yanayotarajiwa ni pamoja na
mtawanyiko mkubwa wa mafuriko, uharibifu wa mali na makazi, kuezuliwa mapaa
kutokana na upepo mkali, uharibifu wa mazao mashambani, miundombinu kutokana na
mafuriko na upepo mkali, kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari katika kipindi
kifupi (storm surge), kuathirika kwa shughuli za usafirishaji kwa njia ya anga,
kwenye maji na nchi kavu inaweza kuathirika hasa katika mkoa wa Mtwara na
maeneo jirani (umbali wa kilometa 500).
Mamlaka
ya hali ya hewa Tanzania inaendelea kufuatilia mwenendo wa kujengeka kwa kimbunga
hicho kusini magharibi mwa bahari ya Hindi pamoja na mwenendo wa mifumo mingine
ya hali ya hewa kwa ujumla na itaendelea kutoa taarifa za mrejeo kila
itakapobidi.
USHAURI: Wananchi wanashauriwa
kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
na kuzingatia tahadhari zilizotolewa na mirejeo yake pamoja na kupata na
kuzingatia ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza
athari zinazoweza kujitokeza.
Imetolewa tarehe
24 Aprili 2019 na:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
No comments:
Post a Comment