|
Kaimu Mkurugenzi
mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) Bw. Samwel Mbuya, mbele ya
waandishi wa habari akielezea mwenendo
wa hali ya hewa hususan mvua za mfululizo zinazoendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo hapa nchini |
Taarifa hii inatoa mwenendo wa hali ya hewa hususan
mvua za mfululizo zinazoendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo hapa nchini.
Mvua
zinazoendelea kunyesha hapa nchini hususan katika maeneo ya pwani ya kaskazini, nyanda za juu kaskazini
mashariki na kanda ya ziwa Victoria ni
sehemu ya mvua za Masika. Mvua hizi zinatokana na kuimarika kwa ukanda wa mvua
(ITCZ). Mvua za mfululizo katika
baadhi ya maeneo ya pwani ya kaskazini (mikoa ya Tanga, Dar es salaam na Pwani
pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba) zinatarajiwa kuendelea kwa kipindi cha siku
mbili zijazo (mpaka siku ya jumapili tarehe 12 Mei 2019). Aidha vipindi vya
mvua za mfululizo vinatarajiwa kujirudia kuanzia katikati ya mwezi Mei, 2019.
Mamlaka itatoa taarifa za mara kwa mara za mwenendo wa mvua hizo katika taarifa
zake za utabiri.
ANGALIZO: Pamoja na kwamba mvua za masika zinatarajiwa
kupungua katika maeneo mengi mwishoni mwa mwezi Mei, 2019; athari za mvua kubwa
zilizonyesha katika kipindi cha wiki moja mfululizo katika ukanda wa pwani ya
kaskazini pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba zimesababisha kutuama kwa maji
na mafuriko. Hivyo kutokana na ardhi kuwa na unyevunyevu mwingi, ongezeko
kidogo la mvua linaweza kuendelea kusababisha athari kama zilizokwisha
jitokeza.
USHAURI: Wananchi wanashauriwa
kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
na kuzingatia tahadhari zilizotolewa na mirejeo yake pamoja na kupata na
kuzingatia ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza
athari zinazoweza kujitokeza.
No comments:
Post a Comment