Meneja Kituo Kikuu cha Utabiri, Bw. Samuel Mbuya akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuelezea ongezeko la joto,pembeni ni Bi. Monica Mutoni kutoka ofisi ya Uhusiano-TMA |
Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa na ufafanuzi kwa jamii juu ya hali
ya ongezekeo la joto katika baadhi ya maeneo hapa nchini.
Kwa
kawaida kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Machi kila mwaka jua la utosi linakuwa
katika maeneo ya kizio cha kusini mwa dunia. Tanzania ikiwa ni moja ya nchi
zilizopo katika kizio cha kusini, huwa na hali ya joto kali katika maeneo mengi
ikilinganishwa na miezi mingine. Hapa nchini, vipindi vya jua la utosi vinafikia
kilele kati ya mwishoni mwa mwezi
Novemba na mwezi Disemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki
ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia
tena mwezi Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya
Kansa). Jua la utosi huambatana na hali ya Joto kali kwa sababu kipindi hicho
ndipo uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo
mengine. Hali hii hushuhudiwa zaidi kunapokuwepo na upungufu wa mvua ambazo zingesaidia
katika kupunguza hali ya joto katika
kipindi husika.
Wastani
wa joto katika mwezi Novemba na Disemba ni
nyuzi joto 31.5 kwa mikoa ya Dar
es Salaam, Tanga na visiwa vya Unguja na
Pemba. Hata hivyo, mpaka kufika mwishoni
mwa Novemba 2018 joto limeshafika nyuzi joto 34. Katika baadhi ya maeneo hapa
nchini ikiwemo mikoa ya Kilimanjaro, Arusha,
Manyara, Morogoro, Dar es salaam, Pwani pamoja na visiwa vya Unguja na
Pemba ambapo msimu wa mvua za Vuli unaendelea
kukumbwa na mtawanyiko hafifu wa mvua hali ya fukuto inachangia katika hali ya joto japo vipimo vya nyuzi joto katika
baadhi ya maeneo hayo ni vya wastani.
Vipindi
hivi vya joto kali vinatarajiwa kupungua
kadiri mtawanyiko wa mvua za vuli utakavyoimarika katika mwezi Disemba 2018. Hata hivyo ikizingatiwa
kuwa hali ya joto inatarajiwa kujirudia tena mnamo mwezi Februari 2019,
wakati wa kipindi cha pili cha jua la utosi.
Aidha, taarifa za mwenendo wa joto, zinaendelea kutolewa katika utabiri
wa kila siku na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Hivyo tunatoa wito kwa wananchi kuendelea
kufuatilia taarifa hizo na kuchukua hatua stahiki kila inapobidi.
No comments:
Post a Comment