Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Kangi Lugola akipata maelezo
kutoka kwa meneja wa TMA kanda ya kati Bw. Waziri Waziri katika banda
la TMA kwenye maadhimisho ya wiki ya zimamoto na uokoaji, mkoani Dodoma.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imejumuika na
taasisi zingine kuadhimisha wiki ya jeshi la zimamoto na uokoaji kitaifa
inayofanyika Jijini Dodoma tarehe 29 Agosti hadi 01 Septemba 2018. Kauli mbiu
ya maadhimisho hayo ni “Shiriki kukuza uchumi wa viwanda, funga king’amua moto
kwenye kiwanda chako.”
Maadhimisho hayo yalifunguliwa rasmi na Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Kangi Lugola (MB) ambaye alitembelea banda la TMA
na kuwapongeza kwa usahihi wa hali ya juu wa utabiri wa hali ya hewa unaotolewa
kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni na kuwataka waendelee kuboresha ili
kufikia viwango vya juu zaidi ya walipo kwa sasa. Mhe. Lugola
aliweza kupata maelezo mafupi kutoka kwa meneja wa TMA kanda ya kati Bw.
Waziri Omari Waziri ambapo alieleza kuwa taarifa za hali ya hewa ni muhimu kwa
shughuli za uokoaji na zimamoto, akitolea mfano taarifa za upepo mkali ambao
kwa kiasi kikubwa unaweza kusababisha moto kusambaa kwa kasi (eneo kubwa)
au hata kwa watumiaji wa bahari au ziwa kuathirika na mawimbi makubwa vile vile
taarifa ya mvua kubwa inayotarajiwa kunyesha katika eneo husika zinasaidia
vikosi vya uokoaji kujipanga na vifaa na njia ya uokoaji kutokana na hali ya
hewa ya eneo husika. Aliongezea kuwa mchango wa taaarifa za hali ya hewa katika
kukuza uchumi wa maendeleo ya viwanda ni pamoja na kutambua hali ya hewa ya
eneo husika ili kujua namna ya kuwekeza, mfano mwelekeo wa upepo hii inasaidia
kujua jinsi ya kuelekezea uchafu (moshi), kiasi cha uzalishaji kama vile
vinywaji baridi kwa kipindi cha baridi au joto, usafirishaji wa mazao ya
viwandani hutegemea hali ya hewa ya wakati huo sambamba na miundo mbinu mfano
kipindi cha mvua kubwa ambacho husababisha uharibifu wa miundo mbinu hivyo ni
vyema mwekezaji akatafuta njia mbadala ya usafirishaji na mengine mengi.
IMETOLEWA NA
KITENGO CHA UHUSIANO, MAMLAKA YA
HALI YA HEWA TANZANIA
|
No comments:
Post a Comment