Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi
Atashasta Nditiye tarehe 21 Agosti 2018 amekutana na Katibu Mkuu wa WMO Prof Petteri Taalas
katika ofisi za Wizara ya Uchukuzi ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi
ambapo atashiriki katika uzinduzi wa mfumo wa taifa wa huduma za hali ya hewa
na kutembelea ofisi za TMA tarehe 22 Agosti 2018.
Akizungumza na vyombo vya habari, Mhe. Nditiye amesema
ni heshima kubwa kwa Tanzania kupata ugeni huu kwa vile WMO wamekuwa wakitoa
miongozo mbalimbali katika utekelezaji wa huduma za hali ya hewa kwenye nchi
wanachama ikiwemo Tanzania. Aidha wamekuwa wakiwajengea uwezo TMA kupitia
mafunzo ya wataalam na upatikanaji wa baadhi ya vifaa vya hali ya hewa.
Kwa upande wa Katibu Mkuu huyo wa WMO alisema, amekuwa
akishuhudia mazuri mengi kuhusiana na Tanzania hususani kupitia TMA ambayo ni
moja ya taasis bora za hali ya hewa barani Afrika. Aidha alifafanua kwamba
mafanikio hayo yametokana na juhudi za
serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuboresha miundombinu ya hali ya
hewa ikiwemo kupatikana kwa rada za hali ya hewa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi alisema
katibu mkuu huyo atakuwepo nchini kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa
na TMA katika kutekeleza makubaliano ya kimataifa yaliyofikiwa kupitia Shirika
la Hali ya Hewa Duniani.
Katika mkutano huo alikuwepo pia Katibu Mkuu wa Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Leonard Chamuriho ambapo alifurahishwa na maelezo aliyoyatoa katibu mkuu huyo kwamba
WMO itaendelea kushirikisha taasis za hali ya hewa za Afrika ikiwemo TMA.
No comments:
Post a Comment