Baadhi ya wananchi walishiriki katika uzindua vituo 51 vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe katika viwanja vya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dododma tarehe 27 Juni 2018.(Picha zote kwa hisani ya Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wataalamu wa sekta za kilimo, mifugo na maji watumie taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili waongeze ufanisi katika utendaji kazi wao.
Ametoa agizo hilo
leo (Jumatano, Juni 27, 2018) wakati akizindua vituo 51 vya
kufuatilia taarifa za hali ya hewa, vituo 15 vya haidrolojia, kanzidata ya
taarifa za hali ya hewa na kituo cha operesheni na mawasiliano ya
dharura wilayani Bahi, Dodoma.
Amesema kuwa kuongezeka kwa vituo vipya
vya kisasa vya ufuatiliaji wa mwenendo wa hali ya hewa kumeboresha uhakika wa
utabiri kutoka asilimia 81 hadi 87 kama inavyoshuhudiwa kwenye taarifa
zinazotolewa katika siku za hivi karibuni. “Hivi sasa tukiambiwa kwamba mvua
itanyesha katika maeneo fulani tunakuwa na uhakika kwa asilimia 87 ya utabiri
huo,”.
“Vituo hivi ni muhimu katika kuimarisha
uwezo wa nchi wa utoaji wa huduma za hali ya hewa na haidrolojia kwa ajili ya
shughuli za maendeleo na kuongeza ufanisi katika utoaji wa tahadhari za awali
za majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa na mabadiliko ya
tabianchi,”.
Amesema kupitia mradi huo uliofadhiliwa
na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Serikali imeweza kufungua
vituo 51 vya kisasa vya hali ya hewa katika maeneo mbalimbali nchini na vituo
15 vya kupima ujazo wa maji kwenye mito iliyopo kwenye mabonde ya Pangani,
Ruvuma na Pwani ya Kusini ambavyo vinajiendesha vyenyewe.
“Pia, mradi huu
umeiwezesha Serikali kuanzisha kanzidata ya takwimu na taarifa za
mafuriko na ukame na
taarifa za hali ya hewa na kuondoa ucheleweshwaji wa kupata takwimu au taarifa
kutoka Wizara moja kwenda Wizara nyingine,” amesema.
Hata hivyo, Waziri Mkuu ameziagiza
Wizara ya Maji na Umwagiliaji na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
zitenge fedha kwenye bajeti zao ili ziweze kufuatilia na kusimamia mradi huo
baada ya wafadhili kumaliza muda wao.
Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu
ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, itaendelea kushirikiana na
washirika wa maendeleo katika kuhakikisha kuwa vituo na mifumo iliyowekwa
inafanya kazi ipasavyo kwa usimamizi bora ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu,
Bibi Jenista Mhagama, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack
Kamwelwe na Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba.
Wengine ni Naibu Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, Naibu Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola, Wabunge na
Mwakilishi Mkaazi wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Bibi
Natalie Boucly.
No comments:
Post a Comment