Tanzania kupitia
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeshiriki katika Mkutano wa Sabini wa
Kamati Kuu ya Utendaji ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological
Organization Executive Council WMO-EC 70) uliofanyika makao makuu ya Shirika
hilo, Geneva nchini Uswisi kuanzia tarehe 20 hadi 29 Juni, 2018. Kupitia
mkutano huo Tanzania imepata nafasi ya kushiriki katika kujadili masuala mbalimbali
ya uboreshaji wa huduma za hali ya hewa Duniani sambamba na kutimiza makubaliano
ya Kikanda na Kimataifa katika kukabiliana na athari zinazosababishwa na
mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.
Akielezea manufaa yaliyopatikana katika mkutano huo, Dkt.
Agnes Kijazi mjumbe wa kamati kuu akiwa miongoni mwa wajumbe 37 (wanaowakilisha
Dunia nzima) ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa
TMA alisema masuala
yanayojadiliwa ni sehemu ya Mpango Mkakati wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani na
vipaumbele vyake katika kipindi cha mwaka 2015-2019 unaojumuisha utekelezaji wa
programu za utoaji wa huduma bora zaidi za hali ya hewa kwa jamii “Global
Framework for Climate Services (GFCS)”, uboreshaji wa huduma za hali ya hewa
kwa maeneo ya Dunia yenye barafu ya asili ikiwa ni pamoja na milima mirefu kama
Kilimanjaro (Polar and High mountain regions)., utoaji wa tahadhari za mapema
ili kukabiliana na maafa (Disaster Risk Reduction, Resilience and Prevention), uboreshaji wa huduma za usalama na usafiri wa anga (Aviation
meteorological services), sambamba na kujenga uwezo wa rasilimali watu na vitendea
kazi hasa kwa nchi zinazoendelea na kuweka msisitizo katika tafiti za hali ya
hewa. Vile vile Mkutano huu umejadili namna ya kushirikiana na mashirika
mengine ya kimataifa kama njia ya kuboresha huduma za hali ya hewa kote duniani
na kutatua changamoto za athari zitokanazo na matukio ya hali mbaya ya hewa
hususani yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.
‘Tanzania imeweza kunufaika mojamoja kupitia programu za
utoaji wa huduma bora zaidi za hali ya hewa kwa jamii (Global Framework for Climate Services (GFCS)) ambapo Tanzania na
Malawi ni miongoni mwa nchi mbili barani
Afrika zinazotekeleza program hiyo, Aidha
mlima Kilimanjaro kwa mara ya kwanza umejumuishwa katika program ya kuboresha
huduma za hali ya hewa kwa maeneo ya Dunia yenye barafu ya asili (Polar and High mountain regions)’, Alisema
Dkt. Kijazi.
Aidha, Dkt. Kijazi katika Mkutano huu amewasilisha ripoti ya
Mkutano wa Jopo la Wataalamu wa Kamati Kuu ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani wanaoshughulikia
mafunzo (WMO EC Panel of Experts on
Education and Training) uliofanyika Nairobi, Kenya mwezi Aprili 2018.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo ni Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO),
hivyo Dkt. Kijazi alimwakilisha Rais wa Shirika la Hali ya hewa Duniani akiwa
Mwenyekiti wa Mkutano huo. Katika hotuba yake ya ufunguzi Rais wa Shirika la
Hali ya hewa Duniani alimshukuru Dkt. Kijazi kwa kumuwakilisha vema katika
Mkutano huo.
Kupitia Mkutano huo
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu, Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa,
Geneva, Mhe. Dkt. James Msekela alipata fursa ya kukutana na Katibu Mkuu wa
WMO, Prof. Petteri Taalas na kufanya mazungumzo mafupi kuhusiana na masuala
mbalimbali yanayohusiana na uwakilishi wa Tanzania katika masuala ya hali ya
hewa katika Shirika hilo na namna ya kuendelea kusaidia nchi zinazoendelea kama
Tanzania katika kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa kwa manufaa ya wananchi
wote.
No comments:
Post a Comment