Na Monica Mutoni
WAKATI huu ambapo tunaadhimisha wiki
ya mazingira ni vyema tukakumbuka tulikotoka, wakati wazee wetu wakitumia
busara zao kutushauri kutunza mazingira ili yatutunze.
Moja ya msisitizo wao ulikuwa ni
pamoja na kutuaminisha kwamba utunzaji wa mazingira ni kupanda miti, lakini
umefika wakati na sisi tujiulize kupanda miti ndio utunzaji wenyewe wa
mazingira?
Kwa mujibu wa wataalamu wa mazingira,
ushauri wa wazee juu ya kupanda miti ni sahihi kabisa, nadharia ambayo pia
inaungwa mkono na wataalamu wa hali ya hewa kote duniani ambao wanaamini maeneo
yenye misitu mizito, ndiko kunapokuwa na mvua nyingi zaidi.
Wataalam hao wanatolea mfano wa
misitu mikubwa duniani ikiwemo misitu ya Congo ambapo wanasema pamoja na kupata
mvua nyingi maeneo hayo yanakuwa na hewa
safi kulinganisha na maeneo ambayo hayana misitu kwani miti ina tabia ya
kuondoa hewa chafu kwenye anga na kuongeza hewa safi.
Kwa maana hiyo, kama waaminivyo
wataalamu hatuna budi kufahamu kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya mazingira kwa
maana ya uwepo wa misitu na mabadiliko ya hali ya hewa.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
(TMA), ni taasisi inayoshughulikia masuala ya hali ya hewa nchini na kuiwakilisha
nchi kikanda na Kimataifa. Taasisi hii imepewa jukumu la kutoa huduma za hali
ya hewa kupitia sheria ya hali ya hewa Na. 6 ya mwaka 1977. Mamlaka hii pia
hutoa tahadhari ya hali mbaya ya hewa kila inapotarajiwa kuwepo na huwaelimisha
wananchi juu ya umuhimu wa kutumia taarifa za hali ya hewa.
Kwa kuzingatia matumizi sahihi ya huduma za hali ya hewa
tutaweza kupunguza athari za uharibifu wa mazingira.
TMA inasema takwimu za hali ya hewa
zilizokusanywa kwa kipindi cha miongo kadhaa iliyopita zinaonesha dhahiri kuwa
uharibifu wa mazingira umechangia kwa kiasi kikubwa kusababisha mabadiliko ya
hali ya hewa nchini na duniani kwa ujumla.
Mfano mkubwa wa viashirikia hivyo ni kuongezeka
kwa joto na kupungua kwa mvua katika
maeneo mbalimbali nchini kama ilivyooneshwa
kwenye mwenendo wa mvua wa kitaalamu katika vielelezo vya maeneo mbalimbali
nchini.
Kwa vielelezo hivi, ni wazi
kuwa joto limeendelea kuongezeka miaka
ya karibuni katika mkoa wa Dar es Salaam
na Kilimanjaro ukilinganisha na miaka iliyopita.
Aidha, kiwango cha mvua
kinapungua kwa kiasi fulani ukilinganisha na miaka ya nyuma kama inavyoonekana
kwa mkoa wa Kilimanjaro.
Picha
Na. 1: Kupungua kwa mvua katika mkoa wa Kilimanjaro
Picha Na;2: Ongezeko la joto kwa mkoa wa Kilimanjaro
kuanzia mwaka 1972 hadi 2016
Picha Na. 3: Ongezeko la joto kwa mkoa wa Dar es salaam kuanzia mwaka 1953-2015 |
Hata hivyo, pamoja na
kupungua kwa mvua, kumekuwa pia na vipindi vifupi vya vya mvua kubwa zenye athari kwa watu na mali
zao.
Wanasayansi ya hali ya hewa
wanasema kuwa uharibifu wa mazingira unaosababisha mabadiliko ya hali ya hewa
umeleta changamoto kubwa kwenye kuandaa utabiri wa hali ya hewa kwani hata vile
viashiria vya awali vinapotea.
Utafiti uliofanywa na
Mamlaka ya Hali ya Hewa katika baadhi ya maeneo hapa nchini unaonyesha kuwa
viashiria vinavyotumiwa na wazee wa jadi
kufanya utabiri wa msimu wa mvua vinapotea kutokana na uharibifu wa mazingira.
Viashiria hivyo ni pamoja na uwepo wa wadudu, ndege, mimea na vinginevyo.
Viashiria vinavyotumiwa na wazee wa jadi vimeonekana vikishabihiana kwa kiasi
kikubwa na sayansi na hivyo kuwepo maelezo ya kisayansi kuhusu utabiri wa jadi.
Picha Na. 4: Eneo la jangwani likiwa
limezungukwa na maji yaliyotokana na vipindi vifupi za mvua kubwa katika msimu
wa mvua za VULI 2017
Ni vyema tukatambua umuhimu
wa kutumia taarifa za hali ya hewa hasa zile zilizoandaliwa na wanasayansi wa
hali ya hewa, kwa maana ya TMA kwa kuwa kutokana na kuongezeka kwa vifaa vya
hali ya hewa, mafunzo kwa watumishi na kujitoa kwao kufanya kazi kwa bidii
wamefanikiwa kuboresha utabiri unaotolewa kwa kiasi kikubwa.
TMA hutoa taarifa, ushauri na
takwimu ili kumwezesha mwekezaji kuwekeza aina ya nishati katika eneo husika
ili kuepuka uharibifu wa mazingira mfano wa taarifa hizo ni kasi na mwelekeo wa
upepo, nguvu ya upepo, vipindi vya jua na hali ya mawingu.
Takwimu za upepo kutoka
vituo vya hali ya hewa nchi nzima zinaweza kusaidia uwekezaji wa faida wa
nishati ya umeme inayozalishwa kwa kutumia upepo ambayo ni nishati mbadala ,
nishati hii itasaidia kupunguza matumizi ya mkaa nchini, nishati hii pia ni
rafiki wa mazingira. Ni vyema ukajua takwimu za hali ya hewa zinasemaje ili
kuwekeza kwa faida, mfano mikoa wa Singida, Dodoma n.k
Kwa upande wa takwimu za jua,
ambazo zinapatikana katika vituo vya TMA nchi nzima, zitasaidia maamuzi sahihi
katika miradi mikubwa ya uwekezaji wa nishati ya jua, kama inavyoonekana kuenea
nchini kwa sasa, hii pia ni nishati mbadala na rafiki kwa mazingira yetu.
Takwimu za mvua
zinazopatikana katika vituo vya TMA nchi nzima, zitasaidia kutoa muongozo na
maamuzi ya kuongeza uwekezaji katika nishati inayozalishwa kutokana na nguvu za
maji katika maeneo mbalimbali nchini, hata kujipanga kwa kuweka mbadala pindi
unapotambua kiasi cha maji kinachopatikana kwa kipindi husika
Takwimu za mawimbi na upepo
wa bahari zitasaidia katika tafiti mbali mbali za uwekezaji katika eneo la mafuta na gesi
ambayo pia ni nishati mbadala na rafiki kwa mazingira.
Sote tunatambua mchango wa TMA katika
kutoa huduma za hali ya hewa nchini, tumeshuhudia utabiri na tahadhari za mara
kwa mara zikitolewa hivyo kupunguza athari zake.
Hapo nyuma ilikuwa si rahisi kutabiri
hali ya hewa na kutambua mabadiliko ya hali ya hewa kwa kipindi kirefu kama
vile wiki au mwezi kuachilia mbali utabiri wa mvua za msimu, lakini kutokana na
maboresho makubwa ya vifaa vya kiteknolojia watabiri wengi wameongezewa
ufanisi.
Shime kwa jamii na Mamlaka husika
kutumia huduma za TMA ili kuweza kuwekeza katika njia mbadala za kuiondoa nchi
kwenye janga la uharibifu wa mazingira.
Kwa hitimisho, ni dhahiri huwezi
kutenganisha mazingira na hali ya hewa. Ukubali, ukatae taarifa za hali ya hewa
ni mtambuka kama maji waswahili wanavyosema, maji usipoyanywa utayaoga hivyo
pale penye fursa ya kuzipata ng'ang'ania kwa sababu teknolojia ipo imetuwezesha
kuzipata tena kwa usahihi wake.
Namalizia kwa kuwaza tu kwa sauti
Kama akitokea mtu wa kuhoji, “kama
kupanda miti ndio kupata mvua au hewa safi, mbona Dodoma hakuna miti mingi
lakini kuna mvua na ikifika jioni hali ya hewa ni baridi?” Lipi litakuwa jibu
lako kwake? Usikose kufuatilia makala hizi ili kujifunza zaidi
Picha Na. 5: Wafanyakazi wa TMA wakishiriki
katika zoezi la kupanda miti wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Agnes Kijazi
|
No comments:
Post a Comment