Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imetoa mwelekeo wa hali ya hewa nchini
kwa kipindi cha mwezi Juni hadi Agosti mwaka 2018. Taarifa hiyo imetoa uchambuzi
wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa, joto, upepo na mvua,
ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali
ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mamlaka imeeleza kuwa uwepo kwa hali ya joto la wastani hadi chini ya wastani inatarajiwa
katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo, hali ya baridi inatarajiwa katika
maeneo ya miinuko ya nyanda za juu Kaskazini mashariki (Arusha, Kilimanjaro na
Manyara), Nyanda za juu kusini Magharibi (hususani mkoa wa Njombe) pamoja na
maeneo ya miinuko ya mkoa wa Tanga (hususan wilaya za Lushoto na Bumbuli).
Kuhusu hali ya mvua na upepo taarifa hiyo imeeleza
kuwa maeneo mengi yanatarajiwa kuwa makavu kwa ujumla,pamoja na vipindi vifupi
vya upepo mkali vinatarajiwa kujitokeza katika baadhi ya maeneo. Aidha, vipindi
vya mvua za nje ya msimu vinatarajiwa katika maeneo ya pwani hususan katika
wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Juni, 2018 na vipindi kadhaa kwa mwezi Julai,
2018.
Wananchi wameendelea kushauriwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa ili
kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kama vile hali ya baridi
inayotarajiwa katika maeneo mengi ya nchi hususan maeneo ya miinuko nakuweza
kusababisha kudumaa kwa mazao kama vile ndizi pamoja na mazao ya nje ya msimu,
na kuathiri mifugo. Vile
vile, kutokana na hali ya joto katika bahari ya Hindi kuwa juu ya
wastani kiasi, ongezeko la siku zenye tija katika shughuli za uvuvi katika
kipindi cha msimu wa JJA zinatarajiwa.
Kwa taarifa zaidi tembelea: http://www.meteo.go.tz/news/135
No comments:
Post a Comment