Sunday, August 18, 2019

MCHANGO NA USHIRIKI WA MAMLAKA YA HALI YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA) KATIKA JUMUIYA YA MAENDELEO KUSINI MWA AFRIKA (SADC) NA FAIDA ZINAZOPATIKANA KWA TAIFA KUPITIA SADC



Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ni miongoni mwa taasisi za serikali zinazowakilisha Tanzania kikanda na kimataifa katika masuala ya hali ya hewa. Aidha Tanzania kupitia TMA inashiriki katika kutekeleza itifaki ya SADC ya Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa na mpango mkakati wake kama ifuatavyo:
        i.            Ushiriki katika Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa za nchi za Kusini mwa Afrika “Meteorological Association of Southern Africa (MASA)”

Tanzania kupitia TMA ni mwanachama wa MASA. MASA ni Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa za nchi za Kusini mwa Afrika ulioanzishwa mwaka 1999. Umoja huu ulianzishwa kwa lengo la kushirikiana na kuratibu utekelezaji wa programu mbalimbali za hali ya hewa zinazotekelezwa katika ukanda wa SADC. Katika kutimiza jukumu hilo, wanachama wa MASA hufanya mikutano kila mwaka ili kujadili utekelezaji na kutoa mapendekezo kwa ngazi mbalimbali za maamuzi za  SADC. Katika Umoja huu, Tanzania kupitia TMA imechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa za nchi za SADC “SADC Meteorological Association of Southern Africa (SADC-MASA)” kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka huu wa 2019, kabla ya hapo Tanzania ilikuwa ikishika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa MASA tangu mwaka 2016.

Sambamba na nafasi hiyo, wataalamu wa TMA wamekuwa wakishiriki katika shughuli mbalimbali zenye lengo la kuimarisha ushirikiano na utengamano uliopo kati ya wanachama wa SADC ambazo ni pamoja na ukaguzi wa hesabu za fedha za MASA, kujengea uwezo kwa baadhi ya Taasisi za Hali ya hewa za nchi wanachama wa SADC katika eneo la utoaji wa huduma bora za hali ya hewa “ Quality Management System (QMS)” na mfumo wa utoaji wa tahadhari kutokana na hali mbaya ya hewa “ Common Alerting Protocol (CAP)”.

     ii.            Ushiriki katika Kamati ya Sekta ya Hali ya Hewa kwa nchi wanachama  wa SADC “Sub-Sectoral Committee on Meteorology (SCOM)”

Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekabidhiwa Uenyekiti wa Kamati ndogo ya Sekta ya Hali ya Hewa ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) “Sub-Sectoral Committee on Meteorology (SCOM) kwa kipindi cha mwaka mmoja. Kupitia mikutano inayofanyika kila mwaka ya SCOM, Mamlaka hushirikiana na Taasisi zingine za Hali ya Hewa za nchi wanachama wa SADC kujadili utekelezaji wa masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya hali ya hewa ambapo hutoa mapendekezo kwa ngazi za juu za SADC hivyo kuchangia katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa katika nchi wanachama wa SADC.

   iii.            Kongamano la nchi za kusini mwa Afrika la kuandaa utabiri wa msimu wa hali ya hewa“Southern Africa Regional Climate Outlook Forum (SARCOF)”

Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) hushiriki kongamano la wataalamu ili kuandaa utabiri wa kikanda wa msimu wa mvua kwa nchi wanachama wa SADC “Southern Africa Regional Climate Outlook Forum (SARCOF)”. Utabiri huu wa hali ya hewa huandaliwa kwa ushirikiano wa wataalamu wa taasisi za hali ya hewa na wadau wengine kutoka nchi wanachama wa SADC.

   iv.            Programu maalumu ya kuangalia hali mbaya ya hewa “Severe Weather Forecasting Demonstration Project SWFDP - Southern Africa”

Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inashiriki katika programu maalumu ya kufuatilia na kutoa taarifa za hali mbaya ya hewa (vimbunga, mafuriko, joto kali n.k) kwa nchi wanachama wa SADC hivyo kusaidia nchi kujipanga katika kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.


Faida zinazopatikana kwa Taifa kutokana na ushiriki wa TMA katika SADC
        i.            Kuboresha huduma za hali ya hewa kupitia mafunzo ya hali ya hewa yanayotolewa kwa nchi wanachama wa SADC kupitia programu mbalimbali za hali ya hewa.
     ii.            Kupatikana kwa baadhi ya miundombinu ya hali ya hewa inayotolewa kupitia programu na miradi ya hali ya hewa inayotekelezwa kwa nchi wanachama wa SADC.
   iii.            Kupata utabiri wa misimu ya mvua kwa ukanda wa SADC unaoandaliwa kwa ushirikiano wa wataalamu wa taasisi za hali ya hewa na wadau wengine kutoka nchi wanachama.
   iv.            Kupata taarifa za hali mbaya ya hewa kwa nchi wananchama ikiwemo Tanzania
      v.            Kupata ujuzi unaotokana na ushirikiano na kubadilishana uzoefu baina ya Taasisi za hali ya hewa za nchi wanachama wa SADC.
   vi.            Kuimarisha ushiriki na ushawishi wa Tanzania katika masuala ya hali ya hewa kikanda na kimataifa.

TMA IMEJIPANGAJE KUFIKIA AZMA YA MWENYEKITI YA UCHUMI WA VIWANDA KATIKA SADC?
i.                    Kutoa huduma bora za hali ya hewa zitakazosaidia upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda kama vile mazao.
ii.                 Kutoa huduma bora za hali ya hewa zitakazosaidia kuongeza ufanisi na tija katika ujenzi wa miundo mbinu ya viwanda na uendeshaji wa viwanda vyenyewe.
iii.               Tanzania kupitia TMA itaendelea kusaidia nchi zingine wanachama wa SADC katika kuboresha huduma za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na kuanzisha mifumo ya kiutendaji.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...