Monday, August 7, 2023

MHE. DKT.JAFO ASISITIZA TAARIFA ZA HALI YA HEWA NI UFUNGUO WA SEKTA YA KILIMO






Morogoro 07/08/2023; 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema huduma za hali ya hewa ni ufunguo kwa sekta ya kilimo kwa vile taarifa hizo humsaidia mkulima kupanga ratiba ya kulima na kupanda. Mhe. Jaffo alisema hayo wakati alipotembelea Banda la Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwenye maonesho ya NaneNane 2023, Morogoro, tarehe 07/08/2023.

 

“Kilimo chetu bado tunategemea mvua kwa kiasi kikubwa, hali ya hewa ni ufunguo wa mkulima kujua anatakiwa kulima lini na kupanda nini, hivyo naomba sana uwekezaji huu mkubwa unaofanyika uweze kumsaidia mkulima na kuweza kufanya maamuzi sahihi ya kupanda mazao kulingana na hali ya hewa”.

 

Aidha, aliongezea kuwa uwekezaji wa miradi mbalimbali unaofanyika nchini lazima uzingatie data za hali ya hewa, ambazo zinatolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini,na kuwaagiza wataalamu kuongeza juhudi kwenye utendaji kazi ili taarifa zipatikane kwa wingi zaidi kila zinapohitajika.

 

Alisisitiza, uwekezaji wa rada za hali ya hewa nchini, utasaidia upatikanaji wa data za kutosha na hivyo kuchangia katika mipango na maendeleo endelevu ya nchi, huku akitoa wito kwa wananchi kufuata sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na.2 ya mwaka 2019 katika shughuli mbalimbali. 

 

Mhe. Jaffo aliambatana na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima na wakuu wa wilaya kutoka wilaya za kanda ya Mashariki. 

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...