Tuesday, June 9, 2020

TANZANIA YAONGOZA MKUTANO WA KUWIANISHA SHUGHULI ZA UTOAJI HUDUMA ZA HALI YA HEWA KATIKA UKANDA WA SADC.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO, Dkt. Agnes Kijazi akiongoza Mkutano wa SADC Sekta ya Hali ya Hewa uliofanyika kwa njia ya mtandao katika katika kituo cha kimataifa cha mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), Jijini, Dar es Salaam. Aliyekaa kulia kwake ni Meneja Ushirikiano wa Hali ya Hewa Kimataifa wa TMA, Bw. Wibert Muruke akifuatilia majadiliano ya kikao.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO, Dkt. Agnes Kijazi akijibu hoja za wajumbe wa mkutano wa SADC Sekta ya Hali ya Hewa. Aliyekaa kulia kwake  ni Meneja Ushirikiano wa Hali ya Hewa Kimataifa wa TMA, Bw. Wibert Muruke akiandika muhtasari wa kikao.


Dar es Salaam; Tarehe 04/06/2020
Wakuu wa Taasisi za Hali ya Hewa za Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamefanya mkutano wa kuwianisha shughuli za utoaji wa huduma za hali ya hewa katika Ukanda wa SADC (Harmonizing SADC Strategy and Action Plan on Meteorology).

Mkutano huo ulifanyika tarehe 4 Juni 2020 kwa njia ya mtandao (videoconference) chini ya Uenyekiti wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ambapo  Mkurugenzi Mkuu wa  TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi aliongoza mkutano huo.

Akiwasilisha hotuba yake fupi ya ufunguzi, Dkt. Kijazi alisema kuwa dhumuni kuu la mkutano huo ni kuwianisha shughuli  za  utoaji wa huduma za hali ya hewa katika Ukanda wa SADC ili zichangie ipasavyo katika kutatua changamoto za  sekta ya hali ya hewa katika Ukanda wa SADC kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii katika Nchi Wanachama. Dkt. Kijazi alizitaja baadhi ya changamoto zinazokabili sekta ya hali ya hewa kuwa ni pamoja na uhaba wa miundombinu ya kupima hali ya hewa; kuchakata takwimu za hali ya hewa; na kubadilishana takwimu za hali ya hewa.
Dkt. Kijazi aliendelea kueleza kwamba, licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na Nchi Wanachama kuboresha huduma za hali ya hewa, utatuzi wa changamoto hizo unahitaji pia juhudi za pamoja za wadau na taasisi zote husika ili kuwianisha shughuli za huduma ya hali ya hewa za Kikanda.
 “Licha ya jitihada zilizofanywa na Nchi wanachama katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa, bado kuna changamoto nyingi.  Kama sehemu ya utatuzi  wa changamoto hizi, mkutano huu utajadili namna ya kuwianisha shughuli za huduma za hali ya hewa za Kikanda” alisema Dkt. Kijazi na kuwaomba wajumbe kushiriki kikamilifu na kutoa maoni  yatakayofanikisha  uwianishaji wa shughuli hizo.

Akitoa maelezo ya awali kuhusiana na mkutano huo, Afisa Mwandamizi wa Programu ya Hali ya Hewa katika Secretarieti ya SADC, Dkt. Prithiviraj Booneeady, alisema hatua ya kuwianisha shughuli za huduma za hali ya hewa ni takwa la  Itifaki ya SADC ya Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa (SADC Protocol on Transport, Communication and Meteorology) unaozitaka Nchi Wanachama kuwianisha shughuli za huduma za hali ya hewa ili kuwezesha ushirikiano wa Kikanda na kuimarisha uwezo wa Nchi Wanachama katika utoaji wa huduma za hali ya hewa.  Kwa mujibu wa Dkt. Booneeady, hatua hiyo itasaidia juhudi za pamoja katika kuimarisha uwezo wa Nchi Wanachama katika kukabiliana na majanga yanayotokana na hali mbaya ya hewa.
Mada zilizowasilisha katika mkutano huo ni pamoja na zinazohusiana na programu za Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) katika ukanda wa SADC; Programu za Secretarieti ya SADC zinazohusiana na sekta ya hali ya hewa;  Programu za Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa Kusini mwa Afrika (SADC MASA). Mkutano ulijadili shughuli hizo na kutoa mapendekezo. Mapendekezo yaliyotolewa ni pamoja na kurejewa upya kwa Itifaki ya Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa (SADC Protocol on Transport, Communication and Meteorology) ili ukidhi mahitaji ya sasa ya sekta ya hali ya hewa.

Monday, June 8, 2020

DKT KIJAZI: MSIMU WA KIPUPWE WANANCHI WACHUKUE TAHADHARI ZA VIPINDI VYA UPEPO MKALI NA BARIDI


Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi akitoa mwelekeo wa Hali  ya Hewa, Msimu wa Kipupwe unaoanza mwezi Juni hadi Agost (JJA), 2020

Dar es Salaam,Tarehe 04/06/2020:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi mwelekeo wa hali ya hewa wa msimu wa kipupwe hapa nchini, unaoanzia Mwezi Juni – Agosti 2020, taarifa hiyo imeelezea athari zinazoweza kujitokeza pamoja na ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumzia msimu huo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi aliwataka wananchi kufuatilia utabiri huo wa msimu wa kipupwe kwa kipindi cha Juni-Agosti (JJA) 2020, ambapo mvua za msimu wa Machi hadi Mei ambazo zilileta athari hapa nchini zimeisha.

“Msimu huu wa kipupwe unatarajiwa kuwa na vipindi vifupi vya upepo mkali wa kusi na hali ya ukavu katika maeneo mengi ya nchi hata hivyo, vipindi vya baridi kali vinatarajiwa katika maeneo ya miinuko ya nyanda za juu kusini-magharibi hususan nyakati za usiku na asubuhi”. Alisema Dkt. Kijazi
“Vipindi vya baridi kali vinatarajiwa hasa katika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Juni na kupungua kuelekea mwishoni mwa msimu yaani mwezi Agosti kwa maeneo ya mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe na Rukwa pamoja na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Ruvuma, maeneo haya yanatarajiwa yatakuwa na joto la kawaida kati ya nyuzi joto 6 na 12, hata hivyo baadhi ya maeneo hususan katika mikoa ya Njombe na Mbeya yanatarajiwa kuwa na joto la chini ya nyuzi joto 6”. Aliongezea Dkt. Kijazi
“Nawakumbusha wananchi kuchukua tahadhari na kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 pamoja na mwezi kama unavyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania”, alisisitiza Dkt. Kijazi
                                                                                                                         
Akitoa ufafanuzi zaidi, Dkt. Kijazi alielezea hali ya joto katika maeneo mengi hapa nchini, huku akibainisha kuwa joto la kawaida linatarajiwa katika maeneo mengi ya ukanda wa Pwani na kuashiria uwepo wa vipindi vichache vya baridi ikilinganishwa na hali ya wastani wa muda mrefu (1981-2010) kwa miezi ya Juni-Agosti katika maeneo hayo.

Akizungumzia kuhusu mvua, Dkt. Kijazi alisema, vipindi vya Upepo unaovuma kutoka mashariki na kusini mashariki (Matlai) vinatarajiwa kuleta unyevunyevu kutoka katika bahari ya Hindi na kusababisha kuwepo na matarajio ya vipindi vifupi vya mvua nyepesi katika maeneo machache.

Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Kijazi alisema, hali ya ukavu na upepo inaweza kuongeza upotevu wa maji kwa njia ya mvukizo na kuathiri upatikanaji wa maji kwa mazao, mifugo na matumizi mengine. Jamii inashauriwa kuzingatia matumizi endelevu ya maji ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

“Jamii inashauriwa kuzingatia matumizi endelevu ya maji ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza, wakati huohuo wakizingatia tahadhari za upepo mkali ambazo zitaendelea kutolewa na TMA kila upepo mkali utakapojitokeza”. Alimalizia Dkt. Kijazi

Kwa maelezo kamili tembelea; http://www.meteo.go.tz/weather_forecasts/seasonal-weather-forecast

Monday, May 11, 2020

SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI LAENDELEA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE KWA NJIA YA MTANDAO KATIKA KIPINDI HIKI AMBACHO DUNIA INAKABILIWA NA JANGA LA COVID-19.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO, Dkt. Agnes Kijazi akichangia mada katika mkutano wa WMO (TCC-1), tarehe 27 Aprili, 2020

Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO, Dkt. Agnes Kijazi akiwasilisha mada katika mkutano wa WMO (TCC-1), tarehe 28 Aprili, 2020

 Dar -es -Salaam; Tarehe 29 Aprili 2020.

Wakati Dunia inakabiliwa na janga la COVID-19, Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), linaendelea kutekeleza majukumu yake kwa njia ya mtandao. Akizungumzia utendaji wa Shirika hilo Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt Agnes Kijazi ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) amesema uongozi wa WMO umekuwa na vikao vya mara kwa mara kwa njia ya mtandao ambavyo pamoja na mambo mengine umewekwa utaratibu wa kuhakikisha huduma za hali ya hewa duniani zinaendelea kutolewa katika kipindi hiki cha janga la COVID-19.

Mkutano wa Kwanza wa Kamati ya Uratibu ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) First Session of the WMO Technical Coordination Committee (TCC-1), ulifanyika kwa njia ya mtandao (Telecoference) kuanzia tarehe 27 hadi 29 Aprili 2020 na Dkt. Agnes Kijazi  alishiriki mkutano huo. Akichangia mada inayohusu Bodi ya Utafiti ya Shirika hilo (WMO Research Board), Dkt. Kijazi aliishauri Bodi hiyo kuhakikisha kwamba mojawapo ya vipaumbele vyake iwe kuzisaidia Nchi Wanachama hususan nchi zinazoendelea katika utafiti wa mifumo mipya inayoibuka siku hizi kutokana na mabadiliko ya tabia nchi (unusual systems) ambayo imeonekana kuleta athari kubwa kwa jamii.

Dkt Kijazi aliongeza kusema kwamba utafiti ni muhimu katika kuboresha huduma za hali ya hewa hata hivyo nchi wanachama wa WMO zina uwezo tofauti wa kufanya utafiti katika masuala ya hali ya hewa, hivyo ni muhimu Bodi ya utafiti ya WMO ikaweka katika vipaumbele vyake namna itakavyosaidia masuala ya utafiti katika ngazi ya nchi na kanda, hususan mambo yanayoibuka kama vile mifumo inayosababisha vipindi vya mvua kubwa, upepo mkali, joto kali, baridi kali, kubadilika kwa misimu ya hali ya hewa, jambo ambalo liliungwa mkono na wajumbe wa mkutano huo.

Awali, akifungua Mkutano huo, Mwenyekiti wa mkutano huo Dkt. Albert Martis ambaye ni Makamu wa Pili wa Rais wa WMO, alitoa salamu za pole kwa familia zilizopoteza ndugu na jamaa zao kutokana na janga la ugonjwa wa COVID-19, na kuziomba Taasisi za Hali ya Hewa kuendelea kutoa huduma za hali ya hewa kwa vile zina mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi hususan kuchangia katika kuimarisha usalama wa watu na mali zao.

Bodi ya Utafiti ya WMO ni miongoni mwa vyombo vipya (WMO Bodies) vilivyoundwa na Mkutano Mkuu wa 18 wa WMO uliofanyika Juni 2019, ikiwa ni mpango mkakati wa WMO wa mwaka 2020 hadi 2023 wa kuimarisha mchango wa tafiti za hali ya hewa katika kuboresha huduma za hali ya hewa ili zichangie ipasavyo katika maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii. Bodi hiyo inayoongozwa na Makamuwa Kwanza wa Rais wa WMO iliwasilisha utaratibu wa namna itakavyotekeleza majukumu yake na vipaumbele ilivyojiwekea, ikiwa ni pamoja na kuimarisha masuala ya ubunifu na kufanya tathmini ya athari za ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) katika utoaji wa huduma za hali ya hewa duniani.

Katika siku ya pili ya mkutano huo, Dkt Kijazi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jopo la WMO la kujenga uwezo (Capacity Development Panel), aliwasilisha mada mbili katika kikao hicho kuhusiana na namna jopo hilo litakavyotekeleza majukumu yake (Rule of Procedures) na litakavyoshirikiana na vyombo vingine vya WMO na Taasisi nyingine kote duniani (Coordinated Approach to Capacity Development). Wajumbe walichangia mada hizo na kusisitiza umuhimu wa kuzisaidia nchi wanachama ili kuhakikisha zinatoa huduma bora kwa maendeleo endelevu. Ilifafanuliwa kwamba jopo hilo la kujenga uwezo ni suala mtambuka katika WMO hivyo liweke vipaombele vyake vitakavyowezesha kuzijengea uwezo sekta mbali mbali hasa katika nchi zinazoendelea.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe takribani 38 kutoka kote Duniani wakiwemo viongozi wote wandamizi wa WMO ikiwa ni pamoja na Rais wa WMO, Prof. Gerhard Adrian (Ujerumani); Makamu wa Kwanza wa Rais, Prof. Celeste Saulo (Argentina); Makamu wa Pili wa Rais Dkt. Albert Martis (Curaçao); Makamu wa Tatu wa Rais, Dkt. Agnes Kijazi  (Tanzania); na Katibu Mkuu wa WMO, Prof. Petteri Taalas (Finland). Viongozi hao ni miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Uratibu ya WMO.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...