Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa Mvua za Msimu kuanzia Novemba 2026 hadi Aprili 2027 ikibainisha mvua nyingi zaidi zinatarajiwa katika kipindi cha Novemba 2026 hadi Januari 2027, ikilinganishwa na kipindi cha Februari hadi Aprili 2027. Hali hii inahitaji maandalizi ya mapema ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua nyingi, ikiwemo mafuriko na kuongezeka kwa maji katika mito na mabwawa.
Akizungumza na vyombo vyahabari, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC, Dkt. Ladislaus Chang’a alisema mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zikitarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka. Mvua hizo zinatarajiwa kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na hali ya El Niño yenye Nguvu Kubwa, hususan katika nusu ya kwanza ya msimu, kuanzia Novemba 2026 hadi Januari 2027.
Kwa mujibu wa mwelekeo wa mvua za msimu huo, mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe na Rukwa, pamoja na maeneo ya kusini mwa Mkoa wa Morogoro. Aidha, mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi.
Mvua hizo zinatarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya Oktoba 2026 katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Tabora, Katavi, Kigoma, Lindi na Mtwara, kabla ya kusambaa katika maeneo mengine mwezi Novemba 2026. Katika maeneo mengi, mvua zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya tatu na ya nne ya Aprili 2027.
Dkt. Chang’a alisisitiza, wadau katika sekta mbalimbali kuchukua hatua za stahiki kujiandaa mapema ili kupunguza au kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.
Katika mkutano huo, TMA pia iliwasilisha tathmini ya unyeshaji wa Mvua za Vuli (Oktoba hadi Desemba 2026), ambapo utabiri wake uliotolewa tarehe 18 Agosti 2026 ikijumuisha mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Kaskazini mwa Kigoma, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Kaskazini mwa Morogoro na Visiwa vya Unguja na Pemba. Tathmini hiyo imeonesha kuwa katika baaadhi ya maeneo, ikiwemo Bukoba, mvua zilizonyesha mpaka sasa zimepita wastani wa Mwezi kwa Oktoba. Aidha Mvua zilizonyesha tarehe 22 na 23 Oktoba 2026 katika mikoa ya Tabora, Kigoma, na Shinyanga, pia zilikuwa kubwa na kuzidi wastani wa mwezi mzima. Kwa upande wa Bukoba , wastani wa mvua kwa mwezi Oktoba ni 165 mm, lakini mpaka zaidi 171 mm za mvua zimepimwa. Kwa upande wa Tabora na Shinyanga, wastani wa mwezi Oktoba ni 26 mm na 33 mm mtawaliwa, lakini mvua iliyonyesha tarehe 22 na 23 Oktoba 2026, katika vituo hivi viwili ni 51 mm na 47 mm mtawalia. Hii inaonesha mwelekeo wa kuendelea kuimarika kwa mvua kuelekea mwezi Novemba na Desemba 2026 kama ilivyo tabiriwa tarehe 18 Agostin 2026



No comments:
Post a Comment