Dar es Salaam; Tarehe
04/06/2020
Wakuu wa Taasisi za Hali
ya Hewa za Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
wamefanya mkutano wa kuwianisha shughuli za utoaji wa huduma za hali ya hewa
katika Ukanda wa SADC (Harmonizing SADC Strategy and Action Plan on
Meteorology).
Mkutano huo ulifanyika
tarehe 4 Juni 2020 kwa njia ya mtandao (videoconference) chini ya Uenyekiti wa
Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ambapo Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la
Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi aliongoza mkutano huo.
Akiwasilisha
hotuba yake fupi ya ufunguzi, Dkt. Kijazi alisema kuwa dhumuni kuu la mkutano huo
ni kuwianisha shughuli za utoaji wa huduma za hali ya hewa katika
Ukanda wa SADC ili zichangie ipasavyo katika kutatua changamoto za sekta ya hali ya hewa katika Ukanda wa SADC
kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii katika Nchi Wanachama. Dkt.
Kijazi alizitaja baadhi ya changamoto zinazokabili sekta ya hali ya hewa kuwa
ni pamoja na uhaba wa miundombinu ya kupima hali ya hewa; kuchakata takwimu za
hali ya hewa; na kubadilishana takwimu za hali ya hewa.
Dkt.
Kijazi aliendelea kueleza kwamba, licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na Nchi
Wanachama kuboresha huduma za hali ya hewa, utatuzi wa changamoto hizo
unahitaji pia juhudi za pamoja za wadau na taasisi zote husika ili kuwianisha
shughuli za huduma ya hali ya hewa za Kikanda.
“Licha
ya jitihada zilizofanywa na Nchi wanachama katika uboreshaji wa huduma za hali
ya hewa, bado kuna changamoto nyingi.
Kama sehemu ya utatuzi wa
changamoto hizi, mkutano huu utajadili namna ya kuwianisha shughuli za huduma
za hali ya hewa za Kikanda” alisema Dkt. Kijazi na kuwaomba wajumbe kushiriki
kikamilifu na kutoa maoni
yatakayofanikisha uwianishaji wa
shughuli hizo.
Akitoa
maelezo ya awali kuhusiana na mkutano huo, Afisa Mwandamizi wa Programu ya Hali
ya Hewa katika Secretarieti ya SADC, Dkt. Prithiviraj Booneeady, alisema hatua ya kuwianisha
shughuli za huduma za hali ya hewa ni takwa la
Itifaki ya SADC ya Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa (SADC Protocol
on Transport, Communication and Meteorology) unaozitaka Nchi Wanachama kuwianisha
shughuli za huduma za hali ya hewa ili kuwezesha ushirikiano wa Kikanda na
kuimarisha uwezo wa Nchi Wanachama katika utoaji wa huduma za hali ya hewa. Kwa mujibu wa Dkt. Booneeady, hatua hiyo
itasaidia juhudi za pamoja katika kuimarisha uwezo wa Nchi Wanachama katika
kukabiliana na majanga yanayotokana na hali mbaya ya hewa.
Mada
zilizowasilisha katika mkutano huo ni pamoja na zinazohusiana na programu za Shirika
la Hali ya Hewa Duniani (WMO) katika ukanda wa SADC; Programu za Secretarieti
ya SADC zinazohusiana na sekta ya hali ya hewa; Programu za Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa
Kusini mwa Afrika (SADC MASA). Mkutano ulijadili shughuli hizo na kutoa
mapendekezo. Mapendekezo yaliyotolewa ni pamoja na kurejewa upya kwa Itifaki ya
Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa (SADC Protocol on Transport,
Communication and Meteorology) ili ukidhi mahitaji ya sasa ya sekta ya hali ya
hewa.
No comments:
Post a Comment