Saturday, June 13, 2015

MATUKIO KATIKA PICHA MKUTANO WA BARAZA KUU LA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO)




Ujumbe wa Tanzania unaendelea kushiriki katika kikao cha Mkutano Mkuu wa Kumi na saba wa Shirikia la Hali ya Hewa Duniani (WMO-Congress 17), mijini Geneva, nchini Uswisi. Ujumbe huo umeshiriki katika matukio mbalimbali ya mkutano huo ikiwa ni pamoja na Dkt. Agnes Kijazi kushiriki katika siku ya Jinsia ya WMO (WMO Gender Day), kutoa mada zilizotoa uzoefu wa Tanzania wa utekelezaji wa program za utekelezaji wa programu ya utoaji wa huduma bora za hali ya hewa kwa jamii “Global Framework for Climate Services (GFCS) na programu ya uendelezaji wa mitandao ya upimaji wa hali ya hewa na mawasiliano (WMO Integrated Observation System and WMO Information System-WIGOS/WIS). Kwa habari zaidi angalia picha za matukio mbalimbali ya Mkutano huo hapa. 


Mh. Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Geneva na Murugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Dkt. Agnes Kijazi na Ujumbe wa Tanzania wakishiriki katika Mkutano Mkuu wa Kumi na Saba wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO- Congress-17), Geneva, Uswisi


“WMO Gender Day”, Siku ya Ijumaa, Tarehe 5 Juni 2015 ilikuwa siku ya Jinsia (WMO Gender Day) ya Mkutano wa Kumi na saba wa Shirika la hali ya hewa Duniani (WMO-Congress 17). Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) alikuwa miongoni mwa zaidi ya wajumbe 50 na wafanyakazi wa WMO walioshiriki katika ufunguzi wa siku hii na kujadili masuala mbalimbali katika nyanja ya usawa na uwezeshaji wa wanawake katika taasisi za hali ya hewa na WMO. Maoni yaliyotokana na majadiliano ya siku hii yatajumuishwa na kutengeneza Mpango Mkakati wa WMO utakaolenga masuala ya jinsia (WMO Gender Action Plan)

Vile vile siku ya tarehe 6 Juni 2015, Dr. Kijazi alishiriki katika warsha ya Uongozi ya viongozi wanawake ikiwa na lengo kuwajengea uwezo zaidi wa uongozi wajumbe waliohudhuria katika mkutano mkuu wa kumi na saba wa WMO.


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Dr Agnes Kijazi akiwasilisha mada ya uzoefu wa Tanzania katika utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa jamii (Global Framework for Climate Services (GFCS)) katika Mkutano Mkuu wa Kumi na Saba wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO Congress-17), Geneva, Uswisi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dr. Agnes Kijazi akiwasilisha mada ya uzoefu wa Tanzania katika utekelezaji wa Programu ya "WMO Intergrated Global Observation Systems (WIGOS)" katika Mkutano Mkuu wa kumi na saba wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Geneva, Uswisi.


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dr. Agnes Kijazi na Mkurugenzi wa utabiri Dr. Hamza Kabelwa wakiwa katika majadiliano na maafisa wa Shirika la Hali ya hewa Duniani (WMO) na Marekani wakati wa majadiliano yanayohusu namna ya kuboresha huduma za hali ya hewa kwa jamii hususan utoaji wa tahadhari “ Early Warning” katika Mkutano Mkuu wa kumi na saba wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Geneva, Uswisi.


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dr. Agnes Kijazi na Mtabiri Mwandamizi katika Ofisi ya Mahusiano ya Kimataifa ya TMA, Ndugu. Wilbert Timiza wakifuatili mwenendo wa Mkutano Mkuu wa kumi na saba wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Geneva, nchini Uswisi.


Saturday, June 6, 2015

TANZANIA IMECHAGULIWA KUWA MJUMBE KATIKA BARAZA LA UTENDAJI (EXECUTIVE COUNCIL) LA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI–WORLD METEOROLOGICAL ORGANIZATION (WMO), GENEVA, USWISI, 4 JUNI 2015



Dr. Kijazi amechaguliwa tarehe 4 June 2015 bila kupingwa wakati Mkutano Mkuu wa kumi na saba wa Shirika la hali ya Hewa Duniani(WMO-Congress wa 17) ulioanza tarehe 25 Mei ambao unatarajiwa kumalizika tarehe 12 June,2015 jijini Geneva, Uswis

Dr. Kijazi amechaguliwa tarehe 4 June 2015 bila kupingwa wakati wa Mkutano Mkuu wa kumi na saba wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO­ Congress wa 17) ulioanza tarehe 25 Mei ambao unatarajiwa kumalizika tarehe 12 Juni, 2015 jijini Geneva, Uswisi


Kuchaguliwa kwa Dr. Agnes Kijazi kumetokana na jitihada kubwa za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kupitia Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Ubalozi wetu wa Kudumu Umoja wa Mataifa, Geneva,

 Dr. Kijazi anaongoza ujumbe wa Tanzania katika ushiriki Mkutano huo ambao una washiriki kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Maji na Ubalozi wa Tanzania, Geneva.

WMO ni Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya hali ya hewa duniani na mabadiliko ya tabia nchi. WMO inatekeleza majukumu na maamuzi kuhusu maendeleo ya sayansi ya hali ya hewa na uboreshaji wake ikiwa ni pamoja na kusimamia viwango katika upimaji na utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa nchi wanachama.

Hadi wakati wa Mkutano huu unaoendelea nchini Uswisi, WMO ilikuwa na nchi wanachama 191. Katika Mkutano huu nchi za Sudani ya Kusini na Tuvalu zilikaribishwa rasmi kama wanachama wapya wa WMO. Kati ya nchi hizi 191 Wanachama wa WMO ni nchi 37 tu ambazo zina wajumbe katika Baraza hilo kuu. Hivyo hii ni nafasi adhimu na heshima kwa Tanzania, TMA na Dr Kijazi ambaye ni msomi mwenye utaalamu wa kutosha akiwa na shahada ya Uzamivu (Ph.D) katika sayansi ya Hali ya hewa.

Kazi kuu ya Baraza la Utendaji la WMO, ambalo Tanzania imefanikiwa kuwa mjumbe ni kuchukua hatua zinazostahili, kwa kushirikiana na Katibu Mkuu wa Shirika hilo kutekeleza maamuzi yanayotolewa na Mkutano Mkuu (WMO-Congress) ambao hukutana mara moja kila baada ya miaka minne.

Akizungumza baada ya uchaguzi huo Balozi Celestine Mushy, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alielezea sababu ya Tanzania kugombea nafasi hiyo muhimu ni kutaka kuwa ndani ya chombo cha maamuzi na hivyo kushawishi maamuzi yatakayoinufaisha jamii nzima ya kimataifa ikiwemo Tanzania katika masuala ya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na kutoa mwelekeo wa kisayansi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa yanayoendelea maeneo mengi Duniani. Aidha, Dkt. Kijazi alieleza kuridhishwa kwake na jinsi ambavyo nchi wanachama 190 walivyoridhishwa na utendaji wa Tanzania katika kipindi cha miaka mitatu (2012­-2015) ambacho alikuwa mjumbe wa Baraza hili na
hivyo kumchagua tena katika kipindi kingine cha miaka minne.
 “Hii ni heshima kubwa kwa nchi yangu ya Tanzania na ninaahidi kutumia uwezo wangu wote kutekeleza majukumu ya nafasi hii” alisema Dkt. Kijazi.



Dr. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ndiye aliyechaguliwa kuwa mjumbe katika Baraza la Utendaji (Executive Council) la Shirika la Hali ya Hewa Duniani–World Meteorological Organization (WMO) kwa kipindi cha miaka minne kuanzia 2015 hadi 2019.


Imetolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa

Monday, June 1, 2015

TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO MKUU WA 17 WA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO) NCHINI USWISI TAREHE: 25 MEI HADI 12 JUNE 2015.




Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Agnes Kijazi akiwa kwenye picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania na wajumbe toka nchi wanachama wa WMO.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Agnes Kijazi pamoja na ujumbe wa Tanzania akiwemo Bwana Mohamed Ngwali, Mkurugenzi wa TMA – Ofisi ya Zanzibar, wanashiriki mkutano mkuu wa 17 wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) unaofanyika Uswisi, makao makuu ya Shirika hilo kuanzia tarehe 25 Mei hadi 12 Juni 2015. 

Akizungumzia umuhimu wa mkutano huyo, katika mahojiano yaliyofanyika kabla ya kuanza safari  Dkt. Kijazi alisema ni muhimu kwa Tanzania kushiriki mkutano huo ili kutekeleza makubaliano ya kimataifa.  Aliongeza kusema mkutano huo ni wa 17 na utahusisha uchaguzi na uthibitisho wa Katibu Mkuu wa WMO, uchaguzi wa Rais wa WMO na makamu wake watatu pamoja na uchaguzi wa wajumbe wa Baraza kuu (Executive Council). Aidha Dkt. Kijazi alisema mkutano huo utapitia na kupitisha mipango ya muda mrefu na bajeti ya shirika hilo. ‘ Tanzania itahusika moja kwa moja katika uchaguzi wa Katibu Mkuu, Rais, Makamu wa Rais na wajumbe wa baraza  kuu pamoja na kupitisha bajeti na mpango mkakati wa muda mrefu kwa ajili ya shirika hilo’ Alisema Dkt. Kijazi.

Shirika hilo limekuwa likifanya mkutano mkuu kila baada ya miaka minne (4) na kushirikisha nchi wanachama ambao kwa sasa idadi yake ni 191.
Kwa kipindi cha hivi karibuni dunia imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa, hivyo moja ya agenda ni kuhakikisha mkutano huo unaweka mikakati yenye tija katika kupambana na changamoto hizo sambamba na ajenda nyingine mbalimbali zitakazojadiliwa.

Tunawatakia Dkt. Kijazi na Ujumbe wote wa Tanzania majadiliano yenye tija katika mkutano huo muhimu.

IMETOLEWA NA: MONICA MUTONI, OFISA MAHUSIANO MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...