Dodoma, Tanzania, 9 Juni 2026.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imepokea wataalamu wa hali ya hewa na uratibu wa maafa kutoka Uganda na Kenya, na pia kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Hatari za Maafa (UNDRR) kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu mifumo ya tahadhari za mapema.
Ziara hiyo ililenga kupata uzoefu kutoka Tanzania, ambayo ni miongoni mwa nchi kinara katika utekelezaji wa mifumo ya tahadhari za mapema ili kusaidia juhudi za kuanzisha na kuimarisha mifumo kama hiyo nchini Kenya na Uganda.
Aidha ziara hiyo iliongozwa na Dr. Agnes Kijazi, Mkurugenzi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Kanda ya Afrika pamoja na Dkt. Martin Brown Munene, Mtaalamu wa Tahadhari za Mapema kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Hatari za Maafa (UNDRR).
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang'a, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kujenga jamii zitakazoweza kukabiliana na hatari zinazohusiana na matukio ya hali mbaya ya hewa.
"Mifumo ya tahadhari za mapema ni muhimu sana kwa ajili ya kulinda maisha na mali kutokana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa, hususan matukio ya hali mbaya ya hewa, yanayoendelea kuongezeka kwa idadi na ukubwa wake. Kupitia ziara hii wenzetu watajifunza na kupata uzoefu wa namna bora ya kujenga, kutumia na kuratibu mifumo ya tahadhari. Lengo kubwa ni kuimarisha ushirikiano ili kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika kanda yetu na Afrika kwa ujumla," alisema Dkt. Chang'a
Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Kanda ya Afrika alipongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema na uratibu wa maafa. Nawapongeza sana Tanzania kwa ushirikiano mzuri na hatua kubwa ya kuimarisha huduma za hali ya hewa na uratibu wa maafa.
"Ziara ya kubadilishana uzoefu inatoa fursa muhimu kwa nchi za Afrika kujifunza kutokana na uzoefu wa kila mmoja katika kuimarisha mifumo ya tahadhari ya mapema na usimamizi wa hatari za majanga ya hali ya hewa. Nawapongeza kwa uratibu madhubuti katika kuhakikisha tahadhari za mapema zinafika kwa jamii zilizo hatarini na kuchukua hatua za haraka," alisema Dkt. Kijazi.
Akiwakilisha Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupunguza Hatari za Maafa (UNDRR), Dkt. Martin Brown Munene, alishukuru kwa kupata fursa ya kuja kujifunza Tanzania na alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kwa nchi zote za Afrika Mashariki.














No comments:
Post a Comment