Wednesday, June 24, 2026

UNDP YAIKABIDHI TMA MAGARI MATANO KATIKA KUIMARISHA MIFUMO YA UANGALIZI WA HALI YA HEWA NA TAHADHARI ZA MAPEMA KUPITIA MRADI WA SOFF

 

Uploading: 522163 of 522163 bytes uploaded.









Dar es Salaam, 23 Juni 2026:


Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)  limekabidhi rasmi magari matano kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kupitia Mradi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa kuimarisha Uangazi wa Hali ya Hewa (SOFF), hatua inayolenga kuimarisha uwezo wa Tanzania katika uendeshaji na matengenezo ya miundombinu muhimu ya uangalizi wa hali ya hewa nchini.

 

Makabidhiano hayo yalifanyika katika Ofisi za TMA, Ubungo Plaza , Dar es Salaam, tarehe 23 Juni 2026 yakiashiria hatua nyingine muhimu ya ushirikiano kati ya UNDP na TMA katika kuimarisha mifumo ya uangazi na kuboresha huduma za utabiri wa hali ya hewa pamoja na kuongeza ustahimilivu katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa nchini.

 

Magari hayo yatawezesha timu za kiufundi za TMA kufikia vituo vya uangazi wa hali ya hewa vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya ufungaji, matengenezo, ukaguzi na ufuatiliaji wa vifaa vya hali ya hewa. Hatua hii itasaidia kuhakikisha kunakuwa na ukusanyaji na usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

 

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara alisema kuwa uwekezaji huo unaenda mbali zaidi ya kukabidhi magari.

Kwa mtazamo wa kwanza, makabidhiano ya leo yanaweza kuonekana kama kukabidhi magari. Hata hivyo, kwa hakika ni uwekezaji unaowezesha ukusanyaji wa taarifa bora za hali ya hewa ambazo ni msingi wa utabiri sahihi wa hali ya hewa, mifumo ya tahadhari za mapema na kupunguza madhara ya majanga,” alisema.

 

Makabidhiano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa SOFF, ambao ni miongoni mwa uwekezaji mkubwa zaidi unaoendelea nchini Tanzania katika sekta ya miundombinu ya hali ya hewa. Mradi huo una thamani ya takribani Dola za Marekani milioni 13.5, ikijumuisha Dola milioni 9 kutoka Mfuko wa SOFF Multi-Partner Trust Fund na Dola milioni 4.5 kama mchango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Kupitia uwekezaji katika vituo vya uangazi wa hali ya hewa ardhini na angani, mafunzo ya kitaalamu, mradi huo unalenga kuimarisha mchango wa Tanzania katika Mtandao wa Kimataifa wa Uangazi wa Hali ya Hewa (‘Global Basic Observing Network’ - GBON) na kuongeza uwezo wa nchi katika kutoa utabiri sahihi wa hali ya hewa pamoja na huduma madhubuti za tahadhari za mapema.

 

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus B. Chang’a, amepongeza ushirikiano unaoendelea kati ya TMA na UNDP pamoja na msaada unaotolewa kupitia Mradi wa SOFF, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha uwezo wa kiutendaji wa taasisi katika kusimamia mtandao wa kisasa wa uangazi wa hali ya hewa nchini.

 

Wakati ambapo matukio ya hali mbaya ya hewa na athari za mabadiliko ya hali ya hewa yanaongezeka kwa kasi, umuhimu wa mifumo imara ya uangazi wa hali ya hewa na huduma za tahadhari za mapema hauwezi kupuuzwa.

 

Kuhusu UNDP

Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) linafanya kazi katika takribani nchi na maeneo 170 duniani, likisaidia kuondoa umaskini, kupunguza ukosefu wa usawa na kujenga ustahimilivu ili nchi ziweze kufikia maendeleo endelevu. Nchini Tanzania, UNDP inashirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali katika maeneo ya utawala bora, ukuaji shirikishi wa uchumi, mabadiliko ya tabianchi, mazingira na maendeleo endelevu.

 

Kuhusu TMA

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ni taasis ya Serikali iliyoanzishwa kwa sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na.2 ya mwaka 2019 ikiwa na jukumu la kuratibu, kudhibiti na kutoa huduma za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...