Monday, August 7, 2023

MHE. DUGANGE (MB) AFURAHISHWA NA ELIMU YA KIFAA CHA KISASA KINACHOPIMA TAARIFA ZA HALI YA HEWA


 










Mbeya; Tarehe 05 Agosti, 2023;

“Nimefurahishwa sana kupata elimu hii ya mtambo huu ambao naweza kusema ni “Multi Purpose” kwa kupima “aspect” mbalimbali za hali ya hewa na kama tunavyofahamu shughuli kubwa katika maonesho haya ni kilimo, uvuvi na ufugaji, hivyo taarifa zenu ni muhimu sana kwa mkulima kujua aina gani ya mazao anaweza kulima”
Hayo yalizungumzwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Festo Dugange (MB) mara baada ya kupata elimu ya kifaa chenye teknolojia ya kisasa kinachotumika kupima taarifa za hali ya hewa alipokuwa ametembelea banda la TMA lililopo katika viwanja vya John Mwakangale, Uyole - Mbeya kupitia maonesho ya Nane Nane yanayoendelea kufanyika kuanzia tarehe 01 – 08 Agosti 2023.

Aidha, Mhe. Dugange amewapongeza TMA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kutoa mchango mkubwa katika sekta ya kilimo pamoja na kuwataka kuzifikisha taarifa zao kwa wakati katika maeneo ya kiutendaji kupitia mamlaka za Serikali zinazohusika ikiwemo Serikali za Mitaa, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Maafisa Tarafa, Maafisa Usalama ili kuepusha majanga yanayoweza kujitokeza kwa wananchi.

Kwa upande wake Meneja wa Huduma za Hali ya Hewa Kilimo, Ndg. Isack Yonah ameeleza kuwa shughuli kubwa inayofanywa na TMA ni kutoa utabiri wa hali ya hewa na hivi karibuni wametoa taarifa ya uwepo wa El Niño ambayo wadau wengi waliofika bandani hapo wamekuwa wakitaka kupata ufafanuzi wa hali hiyo na kubainisha kuwa El Niño ipo japo alieleza madhara yake yanaweza kujitokeza pale itakapoendelea kuwepo katika msimu wa mvua unaokuja na kuahidi TMA kuendelea kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa mrejeo kadri itakapohitajika.

Ndg. Isack Yonah aliongezea kuwa TMA imeshiriki katika maonesho hayo ya Nane Nane mwaka 2023 katika Mikoa ya Morogoro, Mbeya pamoja na Zanzibar ili kuwaonesha wadau vifaa vya hali ya hewa vinavyotumia teknolojia ya kisasa katika kupima taarifa mbalimbali za hali ya hewa pamoja na kuwakumbusha wadau wanaoshughulika na shughuli za hali ya hewa kuomba kibali na kusajili vituo vyao kwa ajili ya kutoa huduma hizo kama inavyoelekezwa kupitia Sheria No. 2 ya Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA ya Mwaka 2019.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...