Leo ni siku ya Hali ya Hewa Duniani (the World Meteorological
Day-WMD), siku ambayo Jumuiya ya Hali ya Hewa duniani kote inaadhimisha
kumbukizi la siku ambayo Mkataba wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani
(WMO) ulisainiwa mnamo tarehe 23 Machi, 1950. Kwa kawaida siku hii
huadhimishwa na kila Nchi mwanachama wa WMO na kuratibiwa na Taasisi za
Hali ya Hewa za nchi husika. Taasisi hizo hutumia siku hii kuonyesha na
kueleza huduma wanazotoa katika kuhakikisha usalama wa watu na mali zao
dhidi ya athari zitokanazo na hali mbaya ya hewa.
Kwa hapa nchini
kwetu Tanzania, shughuli zote zinazohusiana na masuala ya hali ya hewa
husimamiwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA). TMA ni taasisi ya
Serikali iliyoanzishwa mwaka 2019 kwa mujibu wa sheria ya Mamlaka ya
Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019 kabla ya hapo taasisi hii
ilikuwa ni wakala wa serikali.
Katika kusisitiza na kuhamasisha
umuhimu wa huduma za hali ya hewa katika mipango na maamuzi kwenye sekta
mbali mbali za kiuchumi na kijamii, sherehe za WMD zimekuwa
zikiadhimishwa kwa kaulimbiu maalumu, ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni
“Hali ya Hewa na Maji (Climate and Water)”. Kaulimbiu hii
inaenda sambamba na kaulimbiu ya Siku ya Maji Duniani kwa mwaka 2020,
ambayo imejikita katika athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye
sekta ya maji.
Kwa kawaida maji yapo katika hali mbalimbali
ambazo ni yabisi (barafu), kimiminiko (maji ya kawaida) na gesi (mvuke).
Hali hizo zinatokana na mzunguko ambao maji hupitia ujulikanao kama hydrological cycle
unaohusisha ardhi, anga, bahari, maziwa, misitu na mazingira mengine.
Ongezeko la joto duniani (global warming) linasababisha changamoto ya
mabadiliko ya hali ya hewa na limeathiri kwa kiasi kikubwa mifumo ya
mzunguko wa maji kutokana na kubadilika kwa mifumo ya mikondobahari,
mvukizo wa anga, ufanyikaji wa mawingu na mtiririko wa maji kwenye uso
wa dunia. Athari hizo zinatokana na uhusiano uliopo wa moja kwa moja wa
mifumo ya hali ya hewa na mzunguko wa maji. Changamoto ya mabadiliko ya
hali ya hewa imeathiri pia upatikanaji na ubora wa maji na kupelekea
upungufu wa maji yanayohitajika kwa matumizi katika sekta mbali mbali za
kiuchumi na kijamii.
Aidha, miongoni mwa athari za mabadiliko ya
hali ya hewa ni ongezeko la kina cha bahari Duniani kote. Hii
husababishwa na mambo makubwa mawili: kwanza, ni kutanuka kwa maji ya
bahari kutokana na kuongezeka kwa joto la maji, na pili ni kuyeyuka kwa
barafu katika maeneo yenye barafu, hususan katika uzio wa actic na antaktika.
Ongezeko hilo la kina cha bahari linahatarisha miundombinu, mazingira
na maisha ya jamii zinazoishi maeneo ya fukwe za bahari na visiwa, na
kuathiri ubora wa maji kwa kusababisha mwingiliano wa majichumvi na
vyanzo vya maji baridi hali inayopelekea hitaji la kutumia teknolojia
yenye gharama kubwa kusafisha maji hayo ili kuyafanya bora na yanayofaa
kwa matumizi ya binadamu.
Inatazamiwa kuwa, kutokana na
mabadiliko ya hali ya hewa, matukio ya mafuriko na ukame yataongezeka
kwa wingi (frequency) na ukubwa (intensity) na hivyo kusababisha athari
katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo sekta ya maji,
nishati, usafirishaji na kilimo.
Pamoja na changamoto za
mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, na athari zake katika mfumo wa
mzunguko na upatikanaji wa maji, taarifa za hali ya hewa za sehemu
husika zitasaidia katika kupanga shughuli za kiuchumi na kijamii
zinazotegemea upatikanaji wa maji.
Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA) inatekeleza Programu ya Kitaifa ya Huduma za Hali ya Hewa
“the National Framework for Climate Services (NFCS)”, ambayo ina
malengo ya kuboresha huduma za hali ya hewa katika sekta zilizoathiriwa
zaidi na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa (climate sensitive
sectors) ikiwemo sekta ya maji.
Katika kutimiza mahitaji ya wadau
na matakwa ya program ya NFCS pamoja na sheria iliyoanzisha TMA,
Mamlaka ya Hali ya Hewa hufanya shughuli za uangazi wa masuala ya hali
ya hewa. TMA hufanya uangazi kupitia mtandao wake wa vituo vya hali ya
hewa vilivyopo nchi nzima, ambavyo vinajumuisha vituo vilivyopo kwenye
uso wa dunia nchi kavu (ground weather stations), vilivyopo bandarini
(marine weather stations) na vilivyopo katika anga la juu ambavyo
vinajumuisha mtando wa RADAR (upper air stations).
Aidha, TMA
hutoa utabiri wa hali ya hewa unaotumika katika mipango kwaajili ya
shughuli za kijamii na kiuchumi. Utabiri unaotolewa na TMA ni pamoja na
utabiri wa kila siku (saa 24), siku tano, siku kumi (dekadal forecast),
mwezi, msimu na tahadhari za hali mbaya ya hewa (severe weather warnings
and alerts). Tabiri hizi za hali ya hewa ni kwa jamii yote kwa ujumla,
zikiwa na ushauri unaolenga sekta ambazo shughuli zake hutegemea zaidi
hali ya hewa na maji. Aidha, TMA hutoa taarifa mahsusi kwa sekta mahsusi
kama vile sekta ya usafiri wa anga na usafiri wa kwenye maji. Utabiri
huu husambazwa kwa njia mbalimbali zikiwemo tovuti ya TMA (www.meteo.go.tz),
radio, runinga, mitandao ya kijamii (facebook, twitter, Youtube, na
WhatsApp), magazeti na mfumo wa kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa
njia ya simu za mkononi (FarmSMS).
TMA imeendelea kupata mafanikio
zaidi katika kutekeleza mpango mkakati wake. Mafanikio hayo ni pamoja
na kutekeleza kikamilifu Mpango wa Huduma Bora “Quality Management
System (QMS) na kuendelea kumiliki cheti cha ubora wa huduma kutoka
Shirika la Viwango Duniani (ISO 9001:2015 Certification) katika huduma
za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga.
Katika eneo la vifaa
vya hali ya hewa, TMA imeendelea na mkakati wake wa kuboresha vifaa kwa
kununua vifaa vya kisasa na kuondoa vifaa vinavyotumia zebaki. Mkakati
huu umelenga kuboresha vituo vyote vya hali ya hewa nchini ili kuendana
na ukuaji wa teknolojia ya hali ya hewa duniani, na pia kutekeleza
mkataba wa Minamata (Minamata Convention) unaozitaka nchi zote wanachama
wa Umoja wa Mataifa kusitisha matumizi ya zebaki kabla ya kumalizika
mwaka huu wa 2020.
Hata hivyo pamoja na mafanikio yaliyofikiwa, bado kuna changamoto
mbalimbali ambazo zinahitaji jitihada za wadau wote wa huduma za hali ya
hewa, wakiwemo wadau wa maendeleo “Development Partners (DPs)” ili
kuunga mkono na kuendeleza jitihada za Serikali. Changamoto hizo ni
pamoja na uhaba wa vituo vya uangazi wa hali ya hewa, mabadiliko ya
matumizi ya teknolojia katika huduma za hali ya hewa, mahitaji ya
taarifa za sekta maalumu na maeneo madogomadogo (downcaled information)
na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi katika misimu ya
mvua ambayo husababisha ongezeko la matukio ya hali mbaya ya hewa.
Katika
kuadhimisha siku ya Hali ya Hewa Duniani Kwa mwaka huu wa 2020, napenda
kutoa wito kwa wadau wote wa huduma za hali ya hewa kutoka katika sekta
zote za kiuchumi na kijamii kuhakikisha wanazielewa na kuzitumia
ipasavyo huduma za hali ya hewa katika kupanga mipango ya kiuchumi na
kijamii kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Taifa letu. Napenda pia
kuwaomba wadau wote kutuunga mkono katika utekelezaji wa Programu ya
Kitaifa ya Huduma za Hali ya Hewa (NFCS) ili kuboresha zaidi huduma za
hali ya hewa hapa nchini na kupunguza athari kwa jamii na sekta ambazo
zinaathiriwa moja kwa moja na mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo sekta
ya maji.
Mwisho, nawatakia maadhimisho mema ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani “World Meteorological Day” (WMD) 2020 yenye kauli mbiu “Hali ya Hewa na Maji (Climate and Water)”