Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
imetoa utabiri wa msimu wa mvua za Masika kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili
kwa mwaka. Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari, Mkurugenzi Mkuu
Dkt. Agnes Kijazi alisema maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ni Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, Mikoa
ya Dar es Salaam, Pwani ikijumuisha
kisiwa cha Mafia Tanga
na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, Mikoa
ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na
kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
“Mvua
za Masika kwa kipindi cha Machi hadi Mei, 2020 zinatarajiwa kuwa za wastani
hadi juu ya wastani katika maeneo ya mkoa wa Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba,
maeneo mengi ya mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, mashariki mwa mkoa wa Geita
pamoja na mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara”. Alisema Dkt. Kijazi
Aliendelea kwa kuyataja maeneo ya mkoa wa Kagera,
magharibi mwa mkoa wa Geita, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Pwani
ikijumuisha kisiwa cha Mafia pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro kuwa yanatarajiwa
kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani. Aidha, Dkt. Kijazi alifafanua
kuhusu mvua za nje ya msimu zinazoendelea katika maeneo yanayopata mvua za
Masika hususan maeneo yaliyopo katika pwani ya kaskazini, mvua hizo zinatarajiwa
kuendelea na kuungana na msimu wa mvua wa Masika 2020.
Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza,
Dkt. Kijazi alisema vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza hata
katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani,
hivyo jamii inashauriwa kuchukua hatua stahiki kupunguza athari zinazoweza
kujitokeza.
No comments:
Post a Comment