Kigali, Rwanda; Tarehe 08 Februari,
2020;
Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambaye pia ni Makamu wa Tatu wa
Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Lawrence Kijazi amewashukuru
wakuu wa Taasisi za Hali ya Hewa katika Jumuia ya Afrika Mashariki kwa
ushirikiano mkubwa waliompatia katika kuwania nafasi ya Makamu Watatu wa Rais
wa WMO
“Naomba ushirikiano huu (teamwork) tulio uonyesha katika kipindi cha uchaguzi uendelee pia katika utekelezaji wa majukumu ya Kikanda kwenye uboreshaji na utoaji huduma za hali ya hewa”. Alizungumza Dkt. Kijazi wakati akitoa shukrani hizo kwa niaba ya nchi katika Mkutano wa Wakuu wa Taasisi za Hali ya Hewa za Afrika Mashariki (Heads of EAC Meteorological Service Meeting), uliofanyika tarehe 7 hadi 8 Februari, 2020, Kigali, Rwanda.
Dkt. Kijazi
alisisitiza umuhimu wa kufanya vikao kazi vya pamoja ili kuhakikisha masuala
muhimu yanayohusiana na utoaji huduma ikiwa ni pamoja na kubadilishana taarifa
za hali ya hewa yanapewa kipaombele.
“Kwa kutambua kuwa hali ya hewa haina mipaka ya nchi, hivyo ni wakati muafaka kwa Taasisi zetu kuwa na vikao vya kujadili masuala mbalimbali ya kuboresha huduma, tukichukua mfano wa hali ya hatari iliyopo kwa sasa ya uvamizi wa nzige na mlipuko wa virusi vya corona ambapo kwa kiasi kikubwa hali hizo zinauhusiano na hali ya hewa”. Alisisitiza Dkt. Kijazi.
Masuala
muhimu yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na nchi wanachama wa EAC
kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa viwango vya kimataifa ikiwa
pamoja na kupata cheti cha ubora cha utoaji wa huduma za hali ya hewa yaani ISO
9001:2015 (Tanzania kupitia TMA imeshapata cheti hicho cha ubora cha utoaji wa huduma
za hali ya hewa katika sekta ya usafiri wa anga). Vile vile nchi wanachama wa
EAC kuongeza kasi katika upanuaji wa mtandao wa vituo vya upimaji wa hali ya
hewa na mawasiliano ya data hizo na ubadilishanaji wa ujuzi kuhusu matumizi ya
teknolojia mpya za upimaji wa hali ya hewa katika eneo la Jumuia ya Afrika
Mashariki.
Aidha,
suala la uchangiaji wa huduma za hali ya hewa kwa sekta zinazotumia huduma za
hali ya hewa kibiashara (cost recovery) lilipewa kipaombele pamoja na taasisi
za hali ya hewa kuendelea kuhifadhi data za hali ya hewa kwa kutumia kanzi data
ambazo ni imara kutokana na uhitaji wa matumizi ya data hizi katika maendeleo
endelevu ya nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki.
Kutokana
na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababisha mabadiliko makubwa
katika mifumo ya hali ya hewa mkutano huo umefikia makubaliano kwamba nchi
wanachama waendelee kufanya tafiti na kushiriki katika mijadala ya kukabiliana
na mabadiliko ya hali ya hewa kimataifa kwa maendeleo endelevu ya nchi hizo. Tanzania imeng’ara katika mkutano huo kwa
kuonekana kwamba imetekeleza makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa awali
kwa kiwango cha kuridhisha na hiyo imepelekea TMA kupewa jukumu la kuzisaidia
taasis zingine za Hali ya Hewa katika Jumuia ya Afrika Mashariki zenye
changamoto katika utoaji wa huduma ikiwemo Burundi na Sudan ya kusini.
No comments:
Post a Comment