Monday, February 10, 2020

SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO) LAWASHAURI WADAU WA MAENDELEO KUZIJENGEA UWEZO NCHI WANACHAMA KATIKA MASUALA YA USHIRIKIANO BAINA YA SEKTA YA UMMA NA SEKTA BINAFSI KATIKA UTOAJI WA HUDUMA ZA HALI YA HEWA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirikia la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Lawrence Kijazi (aliyeshika kipaza sauti ) akichangia mada katika “Kongamano la Kidunia la Huduma za Hali ya Hewa (Global Weather Enterprise Forum)”,  liliofanyika tarehe 15 Januari, 2019, Boston nchini Marekani.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Lawrence Kijazi, pamoja na washiriki wengine wa “Kongamano la Kidunia la Huduma za Hali ya Hewa” wakifuatilia mada iliyowasilishwa na Benki ya Dunia ya pendekezo la mradi wa majaribio wa ushirikiano baina ya sekta ya umma na sekta binafsi katika huduma za hali ya hewa.
Bw. Makoto Suwa, mtaalamu kutoka Bank ya Dunia, akiwasilisha mada ya pendekezo la mradi wa majaribio wa ushirikiano baina ya sekta ya umma na sekta binafsi katika huduma za hali ya hewa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirikia la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Lawrence Kijazi (wa pili kutoka kushoto mwenye compyuta mpakato) akichangia mada katika “Mkutano wa Tano wa Ushirikiano wa Kimataifa (5th Annual Symposium on U.S–International Partnerships)”. Dkt. Kijazi alikuwa miongoni mwa wachangia mada (Pannelists) katika mkutano huo.
Washiriki wa Mkutano wa “Mkutano wa Tano wa Ushirikiano wa Kimataifa (5th Annual Symposium on U.S–International Partnerships)” wakifuatilia kwa makini wakati Dkt. Kijazi alipokuwa akichangia mada kuhusu nafasi ya WMO katika kuratibu ubadilishanaji wa takwimu za hali ya hewa




Boston, Marekani; Tarehe 15 Januari, 2020;

Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) limeishauri Benki ya Dunia pamoja na wadau wengine wa maendeleo (Development Parners) kuzijengea uwezo nchi wanachama katika masuala ya ushirikiano baina ya sekta ya umma na sekta binafsi (Public-Private Partnerships) katika utoaji wa huduma za hali ya hewa, ili mfumo wa ushirikiano huo uwe na uendelevu (sustainability). Ushauri huo ulitolewa na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO, ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Mwenyekiti wa Jopo la kujenga uwezo la WMO (WMO Capacity Building Pannel), Dkt. Agnes Lawrence Kijazi, katika “Kongamano la Kidunia la Huduma za Hali ya Hewa (Global Weather Enterprise Forum), lililofanyika tarehe 15 Januari, 2019, Boston nchini Marekani.

Kongamano hilo liliandaliwa na WMO kwa kushirikiana na Mfuko wa Benki ya Dunia wa Kupunguza Majanga “World Bank Group Global Facility for Disaster Reduction and Recovery (WBG/GFDRR)” na Chama cha Wadau wa Huduma za Hali ya Hewa cha Marekani “American Meteorological Society (AMS)”. Lengo la kongamano hilo lilikuwa ni kuwaleta pamoja wadau wa sekta ya umma na sekta binafsi ili kujadili maeneo ya ushirikiano katika utoaji wa huduma za hali ya hewa, ikiwa ni utekelezaji wa malengo ya mpango mkakati wa WMO na maazimio ya mkutano mkuu wa shirika hilo uliofanyika Juni, 2019. Kongamano hilo lilifunguliwa na Mkurugenzi Msaidizi wa AMS, Bwana Bill Hooke, ambaye alisema kwamba kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za hali ya hewa yanayochangiwa na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, na kwa kutambua mchango wa sekta binafsi, ni muhimu kujadili maeneo muhimu ambayo sekta ya umma inaweza kushirikiana na sekta binafsi, ili kuboresha zaidi kuduma za hali ya hewa kwa jamii.

Majadiliano katika kongamano hilo yaliongozwa na mada mbalimbali zilizowasilishwa na wataalamu kutoka Mfuko wa Benki ya Dunia wa Kupunguza Majanga(WBG/GFDRR), ambazo zilieleza umuhimu wa ushirikiano baina ya sekta ya umma na sekta binafsi. Aidha, mapendekezo ya namna ya kutekeleza ushirikiano huo yaliwasilishwa, ambapo Mkuu wa programu ya masuala ya hali ya hewa (Hydromet Programme) ya WBG/GFDRR, Bwana Vladimir Tsirkunov, aliwasilisha pendekezo la kutekeleza mradi wa majaribiowa kuandaa mfumo wa kisheria (Regulatory Framework) utakaoratibu ushirikiano baina ya sekta ya umma na sekta binafsi, ambao ulipendekezwa kutekelezwa katika nchi za Ghana na Rwanda chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.

Wadau walitoa maoni yao kuhusiana na mradi wa majaribio uliopendekezwa, maeneo muhimu ya kushirikiana, pamoja na muundo wa mfumo mzima wa ushirikiano ambapo walishauri masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na: kujumuisha wadau wote muhimu katika ngazi ya nchi, zikiwemo taasisi za utafiti, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na vyama vya wataalamu wa hali ya hewa (National Meteorological Societies); kutolewa elimu kwa wadau wote ili kujenga uelewa wa kutosha; kuandaliwa kwa miongozo ya ushirikiano; kuzingatia uwezo na malengo ya sekta binafsi kuendana na vipaumbele katika nchi/kanda; kuimarisha uwezo wa nchi wanachama/kanda katika sayansi ya hali ya hewa; kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa katika nchi/kanda; kuboresha upatikanaji wa takwimu za hali ya hewa; mfumo wa ushirikiano kuwa na dira maalumu; na mradi wa majaribio ujikite kutengeneza mfumo wa ushirikiano. Aidha, Mkuu wa Taasisi ya Hali ya Hewa ya Marekani, Dkt. Louis Uccellini alielezea uzoefu wa namna taasisi yake inavyoshirikiana na sekta binafsi hususani katika masuala ya teknolojia ya huduma za hali ya hewa.

Akitoa maelezo ya jumla alipochangia mada hiyo, Dkt. Kijazi alisema kwamba, kwa kuwa uwezo wa nchi wanachama kusimamia masuala hayo bado ni mdogo, ni vyema Benki ya Dunia wakajielekeza kujenga uwezo kwanza kuanzia ngazi ya nchi hadi kanda, ikiwa ni pamoja na uwezo wa rasilimali watu, ili kuweka uendelevu katika utekelezaji wa mfumo ya ushirikiano huo. Aidha, Dkt. Kijazi alishauri jukumu la kutengeneza mifumo ya kisera na kisheria liachwe kwa Serikali za nchi wanachama kwa kuwa masuala ya kisera na kisheria ni jukumu la Serikali.

“Nashauri mradi huo ujikite kujengea uwezo wadau wote wanaohusika na ushirikiano huo katika nchi wanachama, ikiwemo rasilimali watu. Pia ni vyema jukumu la kutengeneza mifumo ya kisera na kisheria likaachiwa Serikali za nchi wanachama kwani hilo ni jukumu la Serikali za nchi husika”. Alisema Dkt. Kijazi.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na aliyekuwa Rais wa WMO kwa kipindi cha mwaka 2016 hadi 2019 (ambaye ni raia wa Canada), Bwana David Grimes; Makamu wa Pili wa WMO wa sasa (Argentina), Prof. Celeste Saulo; baadhi ya Wakuu wa Taasisi za hali ya hewa; Rais wa Chama cha Wataalamu wa Hali ya Hewa cha Tanzania (Tanzanian Meteorological Society), Dkt. Buruhani Nyenzi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kijazi alitoa rai kwa wadau wa sekta binafsi kuwekeza katika mifumo ya ukusanyaji wa takwimu za hali ya hewa ili kuboresha upatikanaji wa takwimu(data availability), hususan katika Nchi zinazoendelea, zikiwemo za bara la Afrika, kabla ya kutekeleza mpango wa ubadilishanaji wa takwimu (data sharing), kwa kuwa takwimu zilizopo bado hazitoshelezi.

Dkt. Kijazi alitoa rai hiyo katika Mkutano wa Tano wa Ushirikiano wa Kimataifa katika masuala ya hali ya hewa (5th Annual Symposium on U.S–International Partnerships), ulioandaliwa na Chama cha Wadau wa Huduma za Hali ya Hewa cha Marekani (AMS) kwa lengo la kujadili nafasi ya sekta binafsi katika programu za kidunia za masuala ya hali ya hewa, ambapo Dkt. Kijazi alikuwa miongoni mwa wachangia mada katika mkutano huo (Pannelists) kama Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO. Dkt. Kijazi alikuwa akijibu hoja iliyotolewa kuhusunafasi ya WMO katika kuratibu ubadilishanaji wa takwimu za hali ya hewa ilizisaidie katika utafiti na ubunifu wa mifumo iliyoboreshwa zaidi.

Mkutano wa Tano wa Ushirikiano wa Kimataifa ulihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa WMO, Prof. Petteri Taalas,ambaye aliwasilisha mada iliyoelezea nafasi ya sekta binafsi katika utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa kushirikiana na sekta ya umma (Public-Private Partnership).

Mikutano hiyo iliandaliwa sambamba na Mkutano Mkuu wa Wadau wa Huduma za Hali ya Hewa wa Marekani “100th Annual meeting of the American Meteorological Socity (AMS)”,ambao ulifanyika kuanzia tarehe 10 hadi 16 Januari, 2020, Boston, Marekani.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...