Kibaha,Tarehe 11/11/2019: Wataalamu wa hali ya hewa kutoka vituo mbalimbali vya hali ya hewa nchini wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya lugha ya programu za kisayansi (programming languages) yanayofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 15 novemba 2019, katika ukumbi wa mikutano, TARI,Kibaha.
Mafunzo hayo yalifungiliwa rasmi na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani, Dkt. Agnes Kijazi ambaye alieleza kuwa matarajio yake ni kuona ongezeko la ujuzi wa uchambuzi wa data za hali ya hewa na hivyo kuchangia katika kuongeza usahihi wa utabiri wa hali ya hewa.
“Ni mategemeo yangu kuwa, matokeo ya jumla ya mafunzo haya yataleta mabadiliko katika Mamlaka ikiwa ni ongezeko la jumla la usahihi wa taarifa zinazotolewa na ongezeko la ujuzi wa wafanyakazi katika uchambuzi wa data za hali ya hewa”. Alisisitiza Dkt. Kijazi.
Aliendelea kwa kueleza kuwa akiwa kama mmoja wa wajumbe kumi wanaomshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) katika masuala ya teknolojia anatambua kuwa teknolojia ni jambo muhimu sana ili kuweza kufikia malengo ya maendeleo endelevu na hivyo kupitia mafunzo hayo anawataka washiriki kujikita katika kufikia malengo hayo katika utoaji wa huduma wa za hali ya hewa.
Kwa upande wa mratibu wa mafunzo hayo, Dkt. Habiba Mtongori ambaye pia ni mtaalamu wa hali ya hewa mwandamizi alielezea lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea maarifa ya msingi katika lugha ya programu za kisayansi (CDO na R) ambazo zitawajengea uwezo wa kushughulikia idadi kubwa ya data za hali ya hewa (kama vile netCDF) kwa muda mfupi na kuchakata takwimu mbali mbali (statistical analysis) za hali ya hewa kutoka katika data hizo ili kutoa huduma bora za hali ya hewa za uhakika ambazo zitatumiwa na wadau mbalimbali wa TMA.
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo Bi. Asya kutoka kituo cha Zanzibar alionesha furaha yake ya ushiriki wa mafunzo hayo na kukiri kongeza ufanisi wa majukumu yake kwa manufaa ya Mamlaka na Taifa kwa ujumla kupitia huduma za hali ya hewa.
Aidha, ili kuboresha huduma za hali ya hewa pamoja na umuhimu wa kuwa na vifaa vya kisasa, wataalamu wenye ujuzi wanahitajika, hivyo TMA imeweka mkakati wa kuwa na mafunzo ya ndani kwa watumishi wake ili kuhakikishawana ujuzi wa kutosha kuhakikisha Mamlaka inafikia malengo yake
Mafunzo hayo yameandaliwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa ufadhili wa Serikali ya Norway na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kupitia Awamu ya Pili yaProgramu ya Kidunia ya Utoaji wa Huduma za Hali ya Hewa ya GFCS (Global Framework for Climate Services Adaptation Programme in Africa (APA) II).
No comments:
Post a Comment