Mwanza,
06/11/2019: Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongela amesema kuwa Mamlaka ya
Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kuboresha huduma za hali ya hewa katika
Ziwa Viktoria ambazo zimewanufaisha wananchi wanaofanya shughuli za uvuvi
ziwani na hivyo kuchangia kupunguza majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa.
Aidha, Mhe.
Mongela aliendelea kwa kuipongeza TMA kwa kazi nzuri inayoifanya katika
kufanikisha maboresho ya huduma hizo wakati akifungua rasmi, warsha ya “Utoaji
Elimu Kuhusiana na Huduma za Hali ya Hewa Zinazozingatia Athari (Impact Based
Early Warning Services Awareness Raising Workshop)” inayofanyika katika Ukumbi
wa Chuo cha Benki Kuu, Mwanza, Tarehe 06 hadi 09 Novemba 2019.
“Tunawapongeza sana TMA kwa
kazi nzuri ya kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa katika Ziwa Viktoria, ambazo zimenufaisha wananchi
wanaofanya shughuli za uvuvi ziwani hivyo kuchangia kupunguza majanga
yatokanayo na hali mbaya ya hewa”. Alisema Mhe. Mongela
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika
la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi alitoa taarifa kuwa warsha
hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa WMO wa kuboresha huduma za hali ya
hewa kwa watumiaji wa Ziwa Viktoria uitwao “High impact Weather lAke sYstems
(HIGHWAY), ambao kwa hapa Tanzania unatekelezwa katika wilaya za Sengerema,
Mwanza na Muleba, Kagera kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uingereza
(DFID).
Katika upande mwengine, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza alimpongeza Mkurugenzi
Mkuu wa TMA kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO, na kusema
kwamba mafanikio hayo yamekuja kutokana na utendaji kazi mzuri wa Dkt. Kijazi na wafanyakazi wa Mamlaka
ya Hali ya Hewa, na kuchaguliwa kwake kumeliletea sifa na heshima kubwa Taifa
la Tanzania.
Lengo la warsha hiyo ni
kuwajengea uwezo wadau wa huduma za hali ya hewa wa sekta ya uvuvi ili
kuzielewa na kuzitumia au kuziwasilisha ipasavyo huduma hizo ambazo ni mahususi
kwa sekta ya uvuvi.
No comments:
Post a Comment