Baadhi ya washiriki wakichangia mada katika mkutano wa wadau wa huduma za hali ya hewa katika sekta ya usafiri wa anga uliyofanyika katika ukumbi wa TB II, JNIA - Dar es salaam, Tarehe 07/11/2019. |
Dar es Salaam, Tarehe 07/11/2019: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekutana na wadau wa huduma za hali ya hewa katika sekta ya usafiri wa anga ili kupata mrejesho wa wadau na maoni yao katika kuendeleza uboreshaji wa huduma hizo kitaifa na kimataifa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo,
Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO, Dkt. Agnes Kijazi alielezea
jinsi TMA ilivyopiga hatua katika sehemu ya miundombinu ikiwa ni pamoja na
kusimikwa kwa rada za hali ya hewa, kununuliwa vifaa vya kuhakiki ubora wa
vifaa vya hali ya hewa na kubadilishwa kwa vifaa vinavyotumia zebaki. Aidha,
aliongeza kusema uboreshaji huo ni pamoja na kuendelea kumiliki cheti cha ubora
wa kimataifa (ISO 9001:2015), kuboreshwa kwa mfumo wa usambazaji wa taarifa za
hali ya hewa na kuwajengea uwezo (competence) wataalam, hivyo kuchangia katika
maboresho endelevu yanayoendelea katika Mamlaka katika utoaji huduma.
“TMA inatambua sana mchango wa wadau katika kuboresha
huduma za hali ya hewa hususani kupitia maoni yanayotufikia kupitia njia
mbalimbali, hivyo basi napenda kuwajulisha kwamba TMA imeendelea kupiga hatua
chanya ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu, kumiliki cheti cha ubora cha
kimataifa, kuboreshwa kwa mfumo wa usambazaji na kuhakikisha wataalam wa TMA wana weledi na maarifa ya kutosha katika kutoa
huduma za hali ya hewa kwenye sekta ya usafiri wa anga”. Alisema Dkt. Kijazi
Aidha, wadau walipata fursa ya kupata mrejesho wa namna
maoni yao yalivyofanyiwa kazi pamoja na kupata elimu juu ya matumizi na
maboresho ya mfumo wa usambazaji taarifa za hali za hewa kwa wadau wa usafiri
wa anga (MAIS) ambao ulibuniwa na wataalam wa TMA na kuzinduliwa rasmi na
Mheshiwa Isack Kamwele, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Wadau
waliendelea kusisitizwa umuhimu wa huduma za hali ya hewa katika shughuli zao hususan sekta ya usafiri
wa anga.
Naye mmoja wa wadau kutoka Rwanda Air Bi. Umulisa
Alice wakati wa mkutano huo alisema kuwa ni jambo jema TMA imefanya kukutana na
wadau na kuahidi kutoa ushirikiano wa namna ya kupata maoni zaidi kutoka kwa
marubani wa ndege hiyo ili kuongeza ufanisi wa huduma za Mamlaka.
Kwa kuzingatia umuhimu wa taarifa za hali ya hewa
katika sekta ya usafiri wa anga na kwamba ndege haziwezi kuruka, kutua na hata
kusafiri angani bila taarifa za hali ya hewa na kwa kutambua umuhimu wa sekta
ya usafiri wa anga katika ukuaji wa uchumi wa taifa letu, TMA imejiwekea
malengo ya kuboresha huduma zake inazotoa katika sekta ya usafiri wa anga ili
kutoa mchango chanya katika Azma ya Mheshimiwa Rais ya kufikia uchumi wa kati
ifikapo 2025. Katika kuhakikisha malengo ya kuwa karibu na wateja na kutoa huduma
zinazokidhi matakwa ya wateja katika sekta ya usafiri wa anga, TMA imejiwekea
utaratibu wa kukutana na wadau hao ana kwa ana na kujadili masuala mbalimbali
ya kuboresha huduma kwa mustakabali wa maendeleo ya sekta hiyo na Taifa kwa
ujumla.
No comments:
Post a Comment