26/11/2018; DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Hali ya
Hewa Tanzania (TMA) imezindua rasmi programu mpya ya usambazaji wa utabiri wa
kila siku wa hali ya hewa kwa njia ya televisheni kwa kutumia teknolojia ya
kidigitali ya kisasa “Full HD” katika mkutano na vyombo vya habari, Makao Makuu
ya TMA, Ubungo Plaza Dar es Salaam.
Akizindua rasmi programu
hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi alivishukuru vyombo vya habari hapa
nchini kwa kushirikiana na Mamlaka katika kufikisha taarifa za hali ya hewa kwa
jamii pia alisisitiza lengo la Mamlaka kuboresha ubora wa huduma zake kwa jamii
kwa kufuata maoni yao.
‘Napenda
kuvishukuru vyombo vya habari kwa ushirikiano mnaotupatia katika kusambaza
taarifa za hali ya hewa kwa jamii na maoni yenu kuhusu uboreshaji wa huduma
zetu, Mamlaka imekuwa sikivu na kufanyia kazi maoni ambayo mmekuwa mkiyatoa’.
Mamlaka imekuwa
ikiboresha huduma zake kwa jamii ili kukidhi matakwa ya watumiaji na miongoni mwa matakwa hayo ni pamoja na kuwa
na muonekano wa ‘graphics’ zenye mvuto katika utabiri wa kila siku unaotolewa
na televisheni mbalimbali za habari hapa nchini.
‘TMA inatambua kuwa
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizopiga hatua kubwa katika kuboresha
utangazaji wa njia ya televisheni ambapo kwa sasa imeshaingia katika urushaji
kwa njia ya kidigitali. Aidha TMA ikiwa ni mmoja wa wadau wanaotumia vyombo vya
habari hususan televisheni katika
kufikisha taarifa zake kwa jamii imeona pia ni muhimu kuboresha miundombinu
yake ili kuendana na mabadiliko hayo’ alisema Dkt. Kijazi.
Dkt. Kijazi
aliishukuru Taasisi ya Hali ya Hewa ya Uingereza ambayo kupitia Shirika la Hali
ya Hewa Duniani (WMO) waliisaidia TMA kupata ‘software’ hiyo ya kisasa (High
Definition) na pia kutoa mafunzo kwa wataalam wa TMA.
Kutokana na huduma
hizo za usambazaji zilizoboreshwa Dkt. Kijazi aliviomba vyombo vyote vya habari
vinavyotoa taarifa kwa jamii kupitia Televisheni kushirikiana na TMA ili kusambaza
utabiri wa kila siku wa hali ya hewa. Alisema utabiri wa kila siku ni muhimu
kwa usalama wa watu na mali zao pia kwa maendeleo ya Taifa letu, hivyo wote
tushirikiane kulijenga Taifa letu.
No comments:
Post a Comment