Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri
wa mwelekeo wa hali ya hewa kwa kipindi cha Juni hadi Agosti mwaka huu.
Akizungumzia kuhusiana na mwelekeo huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Meneja
Kituo Kikuu cha Utabiri Bw. Samwel Mbuya alisema “Nchi yetu inatarajia kuwa na hali ya baridi kiasi katika
kipindi hiki sambamba na vipindi vifupi vya mvua vinavyotarajiwa kujitokeza
katika maeneo machache hususan ya ukanda wa Ziwa Viktoria na ukanda wa pwani ya
Kaskazini (Visiwa vya Unguja na Pemba). Katika kipindi cha mwezi Juni hadi Agosti 2016, maeneo mengi ya nchi
yanarajiwa kuwa makavu na yenye hali ya baridi kiasi katika majira haya ya kipupwe.
Mifumo ya hali ya hewa
inaonesha matarajio ya hali ya joto la wastani hadi chini ya wastani katika
maeneo yaliyopo Kusini-magharibi mwa nchi. Hata hivyo, katika msimu wa Kipupwe
wa mwaka huu maeneo mengi ya nchi yanatarajiwa kuwa na joto la wastani hadi juu
ya wastani. Aidha, izingatiwe kuwa hali ya ubaridi inatarajiwa zaidi nyakati za
usiku hadi mapema asubuhi.
“Aliendelea kueleza sababu za
hali hiyo kuwa ni pamoja na kupungua kwa joto la bahari katika eneo la
ukanda wa Tropiki la bahari ya Pasifiki sambamba na Joto la baharà katika eneo
la magharibi wa bahari ya Hindi kuwa la
wastani kwa kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti 2016”. Aidha, joto katika
bahari ya Atlantiki linatarajiwa kuwa chini ya wastani. Hali hiyo inatarajiwa
kusababisha upepo kuvuma kutoka magharibi ukielekea mashariki hususan katika
maeneo ya Ukanda wa Ziwa Viktoria. Joto la bahari la juu ya wastani
linatarajiwa katika eneo la ncha ya kusini ya bara la Afrika hivyo kuathiri
msukumo wa upepo wa kusi.
Kwa upande mwengine, Afisa
Uhusiano wa TMA, Bi. Monica Mutoni alitoa msisitizo kwa wananchi kufuatilia taarifa
hususan za tahadhari zinazotolewa na Mamlaka kupitia vyombo mbalimbali vya
habari, tovuti ya Mamlaka n.k ili kuokoa maisha na mali. Bi. Monica alisema “Hivi
karibuni TMA imekuwa ikitoa tahadhari mbalimbali ikiwa ni pamoja na za kuwepo
kwa upepo mkali na mawimbi makubwa kwenye ukanda wa Bahari Hindi, Maziwa na nchi
kavu hivyo ni vyema wananchi hasa wale watumiaji wa bahari na maziwa kuchukua
hatua stahiki pindi taarifa kama hizo zinapotolewa”.
Aidha, TMA ilipongeza sekta mbalimbali
pamoja na Taasisi, Mamlaka za Serikali na jamii kwa ujumla kwa hatua stahiki zilizochukuliwa katika kipindi
cha msimu wa mvua za Masika 2016 kwa
kutumia Taarifa, Agalizo na Tahadhari za utabiri zilizotolewa na Mamlaka. Ni
wazi kuwa kwa hatua hizo madhara ambayo yangeweza kujitokeza yalidhibitiwa na
hivyo kuchangia katika kufanikisha mipango na utekelezaji wa shuguli za
kiuchumi na kijamii katika kipindi husika.
Kwa tarifa ya kina kuhusiana na
mwelekeo wa hali ya hewa kwa mkoa wako ingia kwenye tovuti ya TMA www.meteo.go.tz au tembelea ofisi zetu
IMETOLEWA
NA MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA
No comments:
Post a Comment