Mkutano
wa Jinsia kuhusu huduma za hali ya hewa ulioandaliwa na Shirika la Hali ya Hewa
Duniani (WMO) ulifanyika Geneva Uswis kuanzia tarehe 5-7 Novemba 2014. Mkutano uliazimia
mambo mbalimbali ikiwa pamoja na
jinsi ya kuhakikisha wanawake wanajiunga kwa wingi katika fani ya sayansi ya hali
ya hewa na maji. Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamuhuri ya Muungano
wa Tanzania alialikwa kutoa hotuba katika ufunguzi wa mkutano huo.
Katika hotuba yake ambayo
imenukuliwa katika hadidu za mkutano Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alisema upo uhusiano wa wazi kabisa kati ya athari za
mabadiliko ya hali ya hewa na usawa wa kijinsia. Alisema, wanawake wanaoishi katika maeneo ya vijijini ndio
ambao kwa kiwango kikubwa wanakumbwa na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba wanakabiliwa na changamoto zinazotokana na
mazingira au mila ambazo zinawazuia kuwa na uwezo wa kumiliki rasilimali na pia
kuwanyimwa haki na sauti ya kushiriki katika kutoa maamuzi mbalimbali. “Ni
muhimu masuala ya jinsia yakajumuishwa na kupewa kipaumbele katika huduma za
hali ya hewa ili kuhakikisha kwamba wanawake wanakuwa na sauti katika kutoa maamuzi ya
hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya
hali ya hewa”
ilieleza hotuba hiyo ya mheshimiwa Rais.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Shirika la hali ya Hewa Duniani
(WMO), Bwana Michael Jarraud alisema kwa kiasi kikubwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani limepata mafanikio
kwa kuongeza utoaji wa huduma zenye mtazamo wa kijinsia kwa wakati na kwa ufanisi.
“Hilo limewezekana kwa kupitia dhamira ya WMO ya kuzingatia mahitaji maalum ya
wanawake na wanaume, pia ushirikishwaji wa wanawake na wanaume katika kuandaa
na kubuni huduma mbalimbali kwa kuzingatia
usawa wa kijinsia”. Aliongeza Bwana Jarraud. Katika hotuba yake ya kufunga
mkutano huo, Katibu Mkuu huyo wa WMO alitoa pongezi maalum kwa Bara la Afrika kwa kuongoza Duniani katika kuteua wanawake kuwa
wakuu wa Taasisi za Hali ya Hewa. Mpaka sasa kuna takribani jumla ya nchi sita za Afrika ikiwemo
Tanzania ambazo wakuu wa Taasisi za Hali ya Hewa ni wanawakwe.
“ Athari za mabadiliko ya hali ya hewa zinawapata wanawake na wanaume
kwa wakati mmoja ingawa wanaoathirika zaidi ni wanawake kutokana na kukosa
elimu ya namna ya kujikinga”, alisema Dkt. Elena
Manaenkova, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Shirika la hali ya Hewa Duniani (WMO). Bi. Elena Manaekova aliongeza kuwa, wanawake na wanaume wanahitaji kuwa
na haki sawa katika kupata ujuzi wa namna ya kutumia taarifa za hali ya hewa,
hivyo kuwawezesha wanawake
ni muhimu ili kuwajengea uwezo katika kukabiliana na na athari zinazotokana na mabadiliko
ya hali ya hewa.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na mwakilishi wa kudumu wa
Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi alisema
kuna haja ya kuwatia moyo wasichana wenye ndoto za kuwa wanasayansi mahiri wa
baadae ili waweze kutimiza ndoto zao na kufikia
malengo waliyojiwekea. “Vijana wa kike
wanahitaji kukataa kukatishwa tamaa bali waangalie wanawake ambao wamepata mafanikio
katika sayansi na kufuata mifano yao” aliongeza Bi. Agnes Kijazi akizungumza
katika mkutano huo.
“Sekta ya Afya inatakiwa kuwa mstari
wa mbele katika kueleza huduma wanazohitaji kutoka Taasisi za hali ya hewa ili
kuziwezesha Taasisi hizo kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya watumiaji. Aidha,
Taasisi za hali ya hewa zinapaswa kuanzisha
mfumo mahususi wa usambazaji wa taarifa za hali ya hewa ili ziwafikie walengwa
kwa wakati” alisema Bi. Hellen
Msemo mwanasayansi kutoka Mamlaka ya
Hali ya Hewa wakati akitoa mada katika
Mkutano huo.
Mkutano huo ulitoa mapendekezo mbalimbali ikiwa pamoja na
kuwaongezea uwezo wanawake ili waweze kupata na kuzitumia taarifa za hali ya
hewa, kuhamasisha Taasisi za Hali ya Hewa Duniani kuandaa mikakati ya mafunzo
na kampeni zinazolenga kuhamasisha wanawake kusoma masomo ya sayansi ili
kujiunga katika fani ya hali ya hewa na kuboresha njia za usambazaji wa taarifa za hali ya hewa ili taarifa hizo ziwafikie wanawake
wengi. Aidha Taasis za Hali ya Hewa zimetakiwa kuhakikisha taarifa zinatolewa
katika lugha nyepesi ya kueleweka kwa wanawake na wanaume.
Imetolewa na : Monica Mutoni Afisa
Mahusiano wa TMA.
No comments:
Post a Comment