Picha: Mgeni rasmi Mhandisi James Ngeleja
aliyemuwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA)(wa
pili kutoka kushoto waliokaa ) na Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi (wa
tatu kutoka kushoto waliokaa) katika picha ya pamoja na washiriki wa warsha ya
kuhamasisha wanasayansi kufanya tafiti za mabadiliko ya hali ya hewa ili
kuchangia katika ripoti ya kimataifa(IPCC report), iliyofanyika katika ukumbi
wa hotel ya Blue Pearl, Tarehe 18 Novemba 2014.
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini imeandaa warsha
ya kuhamasisha wanasayansi wa kitanzania kufanya utafiti wa mabadiliko ya hali
ya hewa ikizingatia matokeo na taarifa za hivi karibuni za Jopo la Kimataifa
linaloshughulikia Sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani (IPCC). Warsha
hiyo imefanyika katika Hoteli ya Blue Pearl, Dar es Salaam, Tarehe 18 Novemba
2014. Warsha hiyo ilifunguliwa na Mhandisi James Ngeleja ambaye alimwakilisha
mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka
ya Hali ya Hewa Bw. Morisson Mlaki. Ushiriki
wa watanzania katika tafiti za mabadiliko ya hali ya hewa dunia ni mdogo hivyo
naomba kutoa rai kwa wanasayansi wote mliopo hapa na nje ya warsha hii
kushiriki katika utafiti hususan katika ripoti ya sita ya IPCC itakayoanza
kuandaliwa hapo baadae’alisema Bwana Morisson Mlaki katika hotuba yake.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya
Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Agnes Kijazi aliwakariribisha washiriki wote na kuwashukuru
Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kwa kufadhili warsha hiyo kupitia
programu ya GFCS. ‘napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha wote mliohudhuria
warsha hii, aidha nawasihi taasis za elimu ya juu hapa nchini kuwahimiza
wanasayansi kufanya tafiti katika mabadiliko ya hali ya hewa ili taarifa za
mabadiliko ya hali ya hewa kwa nchi yetu na Afrika kwa ujumla ziweze kuingia
katika ripoti ya IPCC’ alisema Dkt.Kijazi.
Jopo la Kimataifa
linaloshughulikia Sayansi ya mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani (IPCC) ni chombo cha kimataifa kilichoundwa
ili kutathimini mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Warsha hiyo ilikuwa na washiriki
kutoka COSTECH, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu Dodoma (UDOM) chuo
Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA),Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), wasomi kutoka Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Ofisi ya Waziri
Mkuu,-Kitengo cha Maafa, Wizara ya Kilimo na Usalama wa Chakula, World Food Programme
(WFP),Kituo cha Utafiti wa Masuala ya hali ya hewa (CWCAR), Climate Consult, Baraza
la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Chama cha Msalaba mwekundu
(RedCross) na taasisi mbalimbali za mazingira.
Imetolewa na : Monica
Mutoni, Ofisi ya Uhusiano- Mamlaka ya Hali ya Hewa
No comments:
Post a Comment