Thursday, May 2, 2024

TAARIFA MPYA: MWENENDO WA KIMBUNGA “HIDAYA” KATIKA BAHARI YA HINDI MASHARIKI MWA PWANI YA TANZANIA



Dar es Salaam, 03 Mei 2024 saa 3:00 Asubuhi:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” kilichopo katika Bahari ya Hindi mashariki mwa pwani ya nchi yetu. Kimbunga “HIDAYA” kimeendelea kuimarika na kusogea kuelekea maeneo ya pwani ya nchi yetu ambapo hadi kufika saa tisa usiku wa tarehe 03 Mei 2024 kilikuwa kimeimarika zaidi na kufikia hadhi ya Kimbunga kamili kikiwa umbali wa takriban Kilomita 401 Mashariki mwa pwani ya Mtwara.  Katika kipindi hiki kimbunga HIDAYA kimeendelea kuimarika zaidi huku kasi ya upepo ikiongezeka hadi kufikia Kilomita 130 kwa saa.

 

Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini bado inaonesha uwezekano mkubwa wa Kimbunga “HIDAYA” kusalia katika hadhi ya Kimbunga kamili kwa saa 12 zijazo huku kikiimarika, na kendelea kusogea karibu kabisa na pwani ya Tanzania. Kimbunga hiki kinatarajiwa kuendelea kuwepo hadi tarehe 06 mwezi Mei 2024 na kupungua nguvu baada ya tarehe 6 Mei 2024.

 

Uwepo wa kimbunga “HIDAYA” karibu na pwani ya nchi yetu unatarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo ya jirani. Vipindi vya mvua nyepesi na upepo wa wastani tayari vimeanza kujitokeza katika maeneo ya Mtwara. Ongezeko la mvua na upepo mkali utakaoambatana na mawimbi makubwa baharini vinatarajiwa kusambaa katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani kuelekea tarehe 4 hadi 6 Mei 2024.

USHAURI: Wananchi katika maeneo tajwa na wote wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini wanashauriwa kuchukua tahadhari kubwa na pia kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila baada ya masaa matatu, na mara kwa mara kila inapobidi.

TAARIFA MPYA: MWENENDO WA KIMBUNGA "HIDAYA" KATIKA BAHARI YA MASHARIKI MWA PWANI YA TANZANIA


Dar es Salaam, 02 Mei 2024 Usiku: 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” kilichopo katika Bahari ya Hindi mashariki mwa pwani ya nchi yetu. Kimbunga “HIDAYA” kimeendelea kuimarika na kusogea kuelekea maeneo ya pwani ya nchi yetu ambapo hadi kufika saa tatu usiku wa tarehe 02 Mei 2024 kilikuwa umbali wa takriban Kilomita 402 Mashariki mwa pwani ya Mtwara.  Nguvu ya kimbunga HIDAYA imeendelea  kuimarika na kuwa kubwa zaidi, ambapo hadi kufikia usiku huu kasi ya upepo katika kimbunga  imeimarika na kufika Kilomita 110 kwa saa na inatarajiwa kuendelea kuimarika zaidi katika kipindi cha saa 24 zijazo. 

Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini bado inaonesha uwezekano mkubwa wa Kimbunga “HIDAYA” kuendelea kusogea karibu kabisa na pwani ya Tanzania na kuendelea kuwepo hadi tarehe 06 mwezi Mei 2024. Hata hivyo, kimbunga hicho kinatarajiwa kupungua nguvu baada ya tarehe 6 Mei 2024.

Uwepo wa kimbunga “HIDAYA” karibu na pwani ya nchi yetu unatarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo ya jirani. Vipindi vya mvua nyepesi na upepo wa wastani tayari vimeanza kujitokeza katika maeneo ya Mtwara. Ongezeko la mvua na upepo mkali utakaoambatana na mawimbi makubwa baharini vinatarajiwa kusambaa katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani kuelekea tarehe 4 hadi 6 Mei 2024. 

USHAURI: Wananchi katika maeneo tajwa na wote wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini wanashauriwa kuchukua tahadhari kubwa na pia kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila baada ya masaa matatu, na mara kwa mara kila inapobidi.

UWEPO WA KIMBUNGA "HIDAYA" KATIKA BAHARI YA HINDI MASHARIKI MWA PWANI YA MTWARA





Tuesday, April 30, 2024

​TMA YAPONGEZWA KWA KUIMARISHA UBORA NA USAHIHI WA TAARIFA ZA HALI YA HEWA
















Morogoro; Tarehe 30 Aprili 2024;


Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), wamekutana kupitia kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa TMA kilichofanyika katika ukumbi wa NSSF, Morogoro Tarehe 30 Aprili 2024, kwa lengo la kufanya tathmini ya utendaji kazi wa Mamlaka kwa kuzingatia maazimio ya Baraza lililopita pamoja na kupitia bajeti ya mwaka 2024/2025. Baraza hilo lilifunguliwa rasmi na Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Mhe. Jaji Mshibe Ali Bakari.

 

Mhe. Jaji Mshibe aliwapongeza watumishi wote kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya ya utoaji wa taarifa sahihi za hali ya hewa kwa wakati, taarifa ambazo zimesaidia wananchi na Taifa kwa ujumla kuchukua hatua stahiki. Pongezi hizo zilitolewa pia na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Emmanuel Mpeta, viongozi wa TUGHE Taifa, Wizara na TMA.

 

“Kwa namna ya pekee niendelee kuwapongeza Menejimenti na wafanyakazi wote wa TMA kwa kuendelea kutoa na kusambaza kwa wakati utabiri bora ambao unasaidia kuokoa Maisha ya watu na mali zao, ambapo kwa mvua za vuli zilizoambatana na EL NINO kiwango cha usahihi wa utabiri kilikuwa asilimia 98”. Alisema Mhe. Jaji Mshibe.

 

“Aidha, naendelea kuwakumbusha utendaji kazi wenye weledi na unaozingatia sheria na taratibu za kazi, sisi sote tukashirikiane kutimiza majukumu yetu ili kwenda sambamba na falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan ya “Kazi Iendelee”.” Alisisitiza Jaji Mshibe.

 

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Sayansi ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a alieleza kuwa lengo la kikao hicho cha Baraza ni kujadili na kupitisha mapendekezo ya bajeti ya Mamlaka kwa mwaka wa fedha 2024/25 na kufanya tathmini ya utendaji wa Mamlaka katika mwaka wa fedha 2023/2024.

 

Aidha, taarifa ya utendaji kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24 imeainisha kazi zilizotekelezwa katika kipindi tajwa, mafanikio yaliyopatikana, changamoto na mikakati  ya kutatua changamoto husika.

 

“Mafanikio yaliyopatikana yamechagizwa na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali ya Jamhuri ya Tanzania katika kuijengea Mamlaka uwezo wa kitaasisi, ikiwa ni pamoja na kusomesha wataalamu, kununua vifaa vya kisasa vya uangazi wa hali ya hewa, pamoja na uboreshaji wa Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa cha Kigoma.” Alizungumza Dkt. Chang’a. 

 

Baraza hili limejumuisha wajumbe kutoka vituo vyote vya TMA Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji kwa vitendo wa falsafa ya “Kwa maendeleo endelevu ya TMA, Tushirikishane, Tuimarishane na Tutegemezane” na pia ni utekelezaji wa Dira ya TMA “Kuwa kitovu bora cha huduma za hali ya hewa zinazowasaidia WADAU wote kufikia maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii”.

Friday, April 19, 2024

TANZANIA YACHAGULIWA MAKAMU WA RAIS WA TUME YA SHIRIKIA LA HALI YA HEWA DUNIANI

Mhe. Balozi wa Tanzania na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Geneva, Dkt. Abdallah Posi (aliyekaa upande wa kulia) akimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Miundombinu na Huduma za Ufundi - TMA, Dkt. Pascal Waniha baada ya kutangazwa kuwa Makamu wa Rais wa Tume ya INFCOM kupitia Mkutano wa Tume hiyo uliofanyika katika Makao Makuu ya WMO, Geneva.
Dkt. Pascal Waniha (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine wapya wa Tume ya INFCOM mara tu baada ya kuchaguliwa katika nafazi zao kupitia Mkutano wa Tume hiyo uliofanyika katika Makao Makuu ya WMO, Geneva.

Washiriki wa Mkutano wakisikiliza matokeo ya uchaguzi wa viongozi wapya waliochaguliwa kupitia Mkutano wa Tume ya INFCOM uliofanyika katika Makao Makuu ya WMO, Geneva.

Washiriki wa Mkutano wa Tatu wa Tume ya INFCOM wakiwa katika picha ya pamoja kupitia Mkutano wa Tume ya INFCOM uliofanyika katika Makao Makuu ya WMO, Geneva.

Geneva, Uswisi: Tarehe 18/04/2024

Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imechaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Tume ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) inayosimamia uangazi, miundombinu na mifumo ya taarifa za hali ya hewa (WMO Commission for Observation, Infrastructure and Systems - INFCOM). Katika uchaguzi huo Tanzania iliwakilishwa na Mkurugenzi wa Miundombinu na Huduma za Ufundi, TMA, , Dkt. Pascal Waniha. 

Dkt. Waniha amechaguliwa katika nafasi hiyo  tarehe 18 Aprili, 2024 katika uchaguzi wa viongozi wa Tume ya INFCOM uliofanyika katika Mkutano wa tatu wa Tume hiyo (Third Session of the WMO Commission for Observation, Infrastructure and Systems- INFCOM-3)”, unaoendelea katika makao makuu ya WMO, Geneva- Uswisi tarehe 15 hadi 19 Aprili, 2024.

Uchaguzi wa Tume ya INFCOM umefanyika kufuatia muda wa viongozi waliokuwa madarakani kumaliza muda wao ambapo viongozi hao walichanguliwa mwaka 2021 na  waliongoza Tume ya INFCOM katika kipindi cha miaka minne (2020/21 – 2023/24). Uongozi wa juu wa Tume ya INFCOM unaundwa na Rais wa Tume akisaidiana na Makamu watatu wa Rais. Wagombea katika nafasi ya Makamu wa Rais walikuwa wanne (4), kutoka Tanzania, Czech, Hong Kong-China na India. Katika kinyang’anyiro hicho zilihitajika nafasi tatu na viongozi wapya waliochaguliwa ni Rais wa Tume hiyo, Bw. Michel Jean (Canada) ambaye anaendelea katika nafasi yake, na Makamu wa Rais  ambao ni  Dkt. Pascal Waniha (Tanzania), Dk. Chan Pak Wai (Hong Kong, China) na Dkt. Jan Danhelka (Jamhuri ya Czech).

Tume ya INFCOM ni mojawapo ya mihimili mikuu mitatu inayounda Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO). Mihimili hiyo ni: (1) Tume inayosimamia uangazi, miundombinu ya hali ya hewa na mifumo ya Taarifa za Hali ya Hewa (Commission for Observation, Infrastructure and Systems - INFCOM); (2) Tume inayosimamia Matumizi ya Taarifa za Hali ya Hewa (Commission for Weather, Climate, Hydrological, Marine and Related Environmental Services and Applications - SERCOM) na Bodi ya Utafiti (Research Board). Dkt. Waniha atakuwa miongoni mwa viongozi wapya wa Tume ya INFCOM watakaoiongoza Tume hiyo katika kipindi cha miaka minne (2024- 2028).

Dkt. Waniha ni Mtaalamu mbobezi wa hali ya hewa katika eneo la utabiri wa hali ya hewa kwa kutumia modeli (Climate Modelling and Numerical Weather Prediction -NWP) kwa takribani miaka 29, ambapo ametoa mchango mkubwa katika fani ya hali ya hewa ndani na nje ya Tanzania hususan katika WMO kupitia vikosikazi mbalimbali vya kuboresha miundombinu na huduma za hali ya hewa. Kuchaguliwa kwake katika nafasi hii ni muhimu kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla ikizingatiwa kuwa nchi nyingi za Afrika zina changamoto ya upungufu wa miundombinu na teknolojia ya miundombinu ya hali ya hewa. Miundombinu ya hali ya hewa ni muhimu katika kupima na kufuatilia mienendo ya mifumo ya hali ya hewa na kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi. 


Friday, March 22, 2024

TANZANIA YAWANOA WANAMIBIA MASUALA YA HALI YA HEWA




 


Namibia: Tarehe 18/03/2024.

Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imewanoa watumishi wa Taasisi ya Hali ya Hewa Namibia kwa kuwapatia mafunzo ya kuhakiki weledi wa wafanyakazi wote wanaofanya kazi za kutoa huduma za hali ya hewa katika viwanja vya ndege. Mafunzo hayo yalifanyika katika ofisi za Hali ya Hewa Namibia kuanzia tarehe 04 hadi tarehe 18/03/2024, Windhoek, Namibia. 

Akizungumza wakati wa kufunga rasmi mafunzo hayo, Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Caesar Waitara aliishukuru Taasisi ya Hali ya Hewa Namibia kwa kuichagua Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzani kuendesha mafunzo hayo,  pamoja na uwepo wa taasisi nyingi za hali ya hewa barani Afrika. Aidha, alizitaka taasisi zote mbili kuongeza ushirikiano zaidi katika masuala mbalimbali kwa lengo la kunyanyua uchumi na maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya hali ya hewa nchini kwetu ikiwa ni pamoja na kufunga miundombinu ya kisasa ya hali ya hewa, mafunzo kwa watumishi kwa kuzingatia vigezo vya kitaifa na kimataifa, na  kuweka mifumo wezeshi ya usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kwa urahisi kwa watumiaji wa taarifa hizo, pamoja na kuimarisha mifumo ya uhakiki wa ubora wa huduma (QMS) na weledi wa wafanyakazi”. Alisema Mhe.Waitara. 

Aidha, alieleza kuwa Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi za mwanzoni kabisa kufanikisha kupata cheti cha ubora wa kimatiafa cha “ISO 9001:2015” katika utoaji wa huduma za hali ya hewa katika sekta ya usafiri wa anga. Kupitia mafanikio hayo, Tanzania kuipitia TMA imeweza kuzisaidia nchi zingine kama vile Nigeria, Libya, Saudi Arabia, Maldives na Lesotho katika masuala uanzishaji na utekelezaji wa mifumo ya utoaji huduma bora za hali ya hewa katika viwango vinavyotambulika kimataifa. 

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Hali ya Hewa Namibia, Bw. Elias Aiyambo, aliishukuru Serikali yake kwa kukubali maombi ya kufanya mafunzo hayo muhimu kwa nchi, vilevile aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha mafunzo na kuomba ushirikiano huo uendelee baina ya nchi hizi mbili.  

Akitoa mrejesho wa mafunzo hayo kwa mgeni Rasmi, Mratibu wa mafunzo hayo na Mkurugenzi wa Udhibiti na Usimamizi Ubora wa Huduma za Hali ya Hewa TMA, Dkt. Geofrid Chikojo, alisema wamefanikiwa kutoa elimu kwa wafanyakazi 20 wanaofanya kazi katika viwanja 8 vya ndege pamoja na Makao makuu. Kati ya hao 19 walifanikiwa kufanya majaribio ya weledi ambao 17 waliweza kuthibitisha kuwa na weledi unaotakiwa. Dkt. Chikojo alitoa ushauri kwa Serikali ya Namibia kuwa na mpango wa kuhakikisha mifumo ya uhakiki wa ubora wa huduma na weledi inaendelea kuimarishwa na kuwatumia ipasavyo wafanyakazi waliopata vyeti vya weledi katika mafunzo yaliyofanyika.







Saturday, March 16, 2024

KAMATI YA BUNGE YA KUDUMU YA MIUNDOMBINU YAPONGEZA UWEKEZAJI MKUBWA SEKTA YA HALI YA HEWA










Mwanza; Tarehe 16 Machi, 2024


Kamati ya Kudumu ya Miundombinu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa kwenye sekta hali ya hewa nchini wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na TMA ikiwemo rada ya hali ya hewa iliyopo Kiseke, Mwanza, Tarehe 16/3/2024.

Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe.Seleman Kakoso (MB) wakati wa majumuisho ya ziara hiyo kwa kuridhishwa na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali kwenye Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kupelekea nchi yetu kufanya vizuri katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na hivyo kuihakikishia nchi uhakika wa huduma inayotolewa kwa manufaa ya Taifa letu. Aidha, kamati imeipongeza pia TMA kwa kuongeza ubora na usahihi wa utabiri ikiwemo wa mvua zilizoambatana na Elnino. Pongezi hizo zilipokelewa kwa niaba ya Serikali na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David M.Kihenzile (MB) ambaye aliongoza uongozi wa Wizara na TMA.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kakoso aliagiza uboreshaji wa Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa ufanyike pamoja na maslahi bora ya watumishi. “Tunaiomba Serikali imarisheni Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa ili kiweze kuandaa wataalamu watakaofanya kazi, pili lindeni wafanyakazi wa TMA kwa kuwapatia maslahi mazuri, msipofanya hivyo Serikali itakuwa inasomesha vijana wengi na baadaye wote wanaondoka kwasababu hawalipwi vizuri”. Alisema Mhe. Kakoso.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la KImataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt.Ladislaus Chang’a aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutenga fedha zinazowezesha TMA kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya kuboresha huduma za hali ya hewa nchini.

 

“Rada hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kubaini na kufuatilia mwenendo wa hali ya hewa, vimbunga ziwani,hali mbaya ya hewa,upepo mkali na kutoa tahadhari kwa wananchi hususani watumiaji wa ziwa Viktoria na kuboresha taarifa zinazotolewa na kuimairisha tija na usalama kwa watumiaji wengine wa taarifa za hali ya hewa kama sekta ya usafiri wa anga, ulinzi, kilimo,uvuvi na utunzaji wa misitu”. Alieleza Dkt. Changa.

 

Rada ya hali ya hewa iliyopo Mwanza, inauwezo wa kufanya uangazi wa mikoa ya Mwanza, Shinyanga,Kagera, Mara na eneo kubwa la ziwa vicktoria. Vilevile, rada hii ni moja ya uwekezaji mkubwa unaoendelea wa kukamilisha mtandao wa rada saba zenye teknolojia ya kisasa hapa nchini, ambapo rada tano zimeshafungwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Mbeya na Kigoma na rada mbili zitakazofungwa Kilimanjaro na Dodoma zikiendelea na mategenezo Marekani.  

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...