Saturday, March 16, 2024

KAMATI YA BUNGE YA KUDUMU YA MIUNDOMBINU YAPONGEZA UWEKEZAJI MKUBWA SEKTA YA HALI YA HEWA










Mwanza; Tarehe 16 Machi, 2024


Kamati ya Kudumu ya Miundombinu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa kwenye sekta hali ya hewa nchini wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na TMA ikiwemo rada ya hali ya hewa iliyopo Kiseke, Mwanza, Tarehe 16/3/2024.

Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe.Seleman Kakoso (MB) wakati wa majumuisho ya ziara hiyo kwa kuridhishwa na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali kwenye Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kupelekea nchi yetu kufanya vizuri katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na hivyo kuihakikishia nchi uhakika wa huduma inayotolewa kwa manufaa ya Taifa letu. Aidha, kamati imeipongeza pia TMA kwa kuongeza ubora na usahihi wa utabiri ikiwemo wa mvua zilizoambatana na Elnino. Pongezi hizo zilipokelewa kwa niaba ya Serikali na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David M.Kihenzile (MB) ambaye aliongoza uongozi wa Wizara na TMA.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kakoso aliagiza uboreshaji wa Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa ufanyike pamoja na maslahi bora ya watumishi. “Tunaiomba Serikali imarisheni Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa ili kiweze kuandaa wataalamu watakaofanya kazi, pili lindeni wafanyakazi wa TMA kwa kuwapatia maslahi mazuri, msipofanya hivyo Serikali itakuwa inasomesha vijana wengi na baadaye wote wanaondoka kwasababu hawalipwi vizuri”. Alisema Mhe. Kakoso.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la KImataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt.Ladislaus Chang’a aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutenga fedha zinazowezesha TMA kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya kuboresha huduma za hali ya hewa nchini.

 

“Rada hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kubaini na kufuatilia mwenendo wa hali ya hewa, vimbunga ziwani,hali mbaya ya hewa,upepo mkali na kutoa tahadhari kwa wananchi hususani watumiaji wa ziwa Viktoria na kuboresha taarifa zinazotolewa na kuimairisha tija na usalama kwa watumiaji wengine wa taarifa za hali ya hewa kama sekta ya usafiri wa anga, ulinzi, kilimo,uvuvi na utunzaji wa misitu”. Alieleza Dkt. Changa.

 

Rada ya hali ya hewa iliyopo Mwanza, inauwezo wa kufanya uangazi wa mikoa ya Mwanza, Shinyanga,Kagera, Mara na eneo kubwa la ziwa vicktoria. Vilevile, rada hii ni moja ya uwekezaji mkubwa unaoendelea wa kukamilisha mtandao wa rada saba zenye teknolojia ya kisasa hapa nchini, ambapo rada tano zimeshafungwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Mbeya na Kigoma na rada mbili zitakazofungwa Kilimanjaro na Dodoma zikiendelea na mategenezo Marekani.  

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...