Sunday, April 12, 2026

TANZANIA YAJIPANGA NA UTEKELEZAJI WA MRADI WA SOFF AWAMU YA TATU.

 















Morogoro, Tanzania; 09 Aprili 2025.

 

Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Tendaji ya Mradi wa SOFF na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Ladislaus Chang’a alifungua rasmi Mkutano wa Tatu wa Kamati Tendaji ya Mradi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuimarisha Uangazi wa Hali ya Hewa - SOFF (PSC-3) tarehe 9 Aprili 2026 katika Hoteli ya Morena, Morogoro, na kusisitiza dhamira ya Tanzania ya kufikia malengo ya utekelezaji wa Mradi wa SOFF nchini ili kukidhi mahitaji ya Mtandao wa Kidunia wa Uangazi wa Hali ya Hewa (GBON)

 

Akizungumza na wajumbe wa Kamati, Dkt. Chang’a alisema, Mradi wa SOFF unaingia mwaka wa tatu. Hivyo, shughuli zilizopangwa chini ya mradi huu zinakusudia kuhakikisha kuwa ifikapo Desemba 2027, Tanzania itakuwa imefikia malengo ya mradi ya kuhakikisha miundombinu ya hali ya hewa na mifumo yake imesimikwa sambamba na kuwajengea uwezo wataalamu.

 

Mkutano huo ulitoa fursa ya kutathimini maendeleo ya mradi na kufanya maamuzi yatakayoainisha njia na namna bora ya kusonga mbele. "Katika kikao hiki wajumbe wa PSC watapitia taarifa ya maendeleo ya mradi, mpango kazi wa mwaka 2026, na kutoa maelekezo ya kuhakikisha Mradi unafikia malengo ya GBON ifikapo Desemba 2027.". Alisisitiza Dkt. Chang’a

 

Vilevile aliipongeza Sekretarieti na Timu ya Utekelezaji wa Mradi kwa hatua nzuri iliyofikiwa na kuhimiza kuongeza bidii ili kufikia malengo ya mradi na kulinda sifa kubwa ya Tanzania kikanda na kimataifa katika sayansi ya hali ya hewa.

 

"Hatua na mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa ni matokeo ya juhudi za pamoja baina ya wadau wote wa Mradi, lazima tuendelee kufanya kazi kwa bidii ili Tanzania iendelee kuwa mfano wa kuigwa katika ukanda huu," alisema Dkt. Chang’a.

 

Awali Mwenyekiti Mwenza na Mwakilishi Mkazi Msaidizi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bw. Amon Manyama alisema kipaumbele cha UNDP ni kuhakikisha kazi zilizopangwa zinakamilika kwa wakati, ikiwemo ununuzi na ufungaji wa vifaa pamoja na kuwezesha mifumo ya uendeshaji ili kuhakikisha kuwa vifaa hivyo vya hali ya hewa vinafanya kazi katika viwango vya ubora.

 

SOFF ni Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuimarisha Uangazi wa Hali ya Hewa kwa Nchi zinazoendelea na Nchi za Visiwa vidogo. Lengo la Mradi ni kuimarisha huduma za hali ya hewa katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ili kulinda maisha ya watu na mali ikiwemo kuboresha zaidi miundombinu ya uangazi wa hali ya hewa na kuhakikisha Tanzania inakidhi mahitaji ya wadau wa Kitaifa na Kimataifa. Mradi huu unatekelezwa kwa muda wa miaka minne kuanzia Julai 2024 hadi Desemba 2027.

 

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...