Leo, tarehe 23 Machi 2026, nina furaha kuungana na jamii ya kimataifa katika kuadhimisha miaka 76 ya kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO). Siku hii ni fursa ya kutambua na kupongeza mchango muhimu unaotolewa na Taasisi za Hali ya Hewa Duniani kote katika kuokoa maisha, mali, na kusaidia kuleta maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.
Kaulimbiu ya Siku ya Hali ya Hewa Dunia mwaka huu 2026 ni “Pima hali ya hewa leo, ili kesho iwe salama”. Kaulimbiu hii inasisitiza umuhimu wa ufuatiliaji endelevu wa mifumo ya hali ya hewa na maji na upimaji wa taarifa zake. Kwa kuimarisha mifumo hii ya ufuatiliaji na uangazi wa hali ya hewa na maji, nchi nyingi ikiwemo Tanzania, zinajizatiti zaidi kutoa taarifa za tahadhari za mapema hivyo kupunguza athari zinazohusiana na ongezeko la mabadiliko ya hali ya hewa hususan matukio ya hali mbaya ya hewa yanayoongezeka kwa ukubwa na idadi.
Sote tunafahamu umuhimu wa taarifa sahihi na za wakati za hali ya hewa katika kufanya maamuzi sahihi kwa sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Sekta hizi ni pamoja na uchukuzi, kilimo, nishati, maji, afya, miundombinu, ujenzi, madini, na nyingine nyingi zinazohusiana na zinazoathiriwa na hali ya hewa. Hata hivyo, mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi yanaendelea kusababisha changamoto kubwa katika sekta hizi kutokana na kuongezeka kwa idadi na ukubwa wa matukio ya hali mbaya ya hewa.
Kwa mujibu wa WMO, kati ya mwaka 1970 na 2021, matukio ya hali mbaya ya hewa yamesababisha hasara ya dola za Kimarekani takriban trilioni 4.3 na vifo vipatavyo milioni 2, ambapo zaidi ya 90% ya vifo hivyo vimetokea katika nchi zinazoendelea, hivyo kuonesha udharura wa kuimarisha miundombinu na mifumo ya ufuatiliaji na uangazi wa hali ya hewa ambayo itasaidia kuimarisha mifumo ya utoaji wa tahadhari za mapema kwa jamii leo na wakati ujao, sambamba na kuongeza uwezo wa wataalamu.
Uwekezaji katika miundombinu ya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na mifumo ya utoaji wa tahadhari za mapema ni uamuzi wa kimkakati ambao Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuufanya. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka juhudi za kipekee katika kuwekeza katika miundombinu na mifumo ya hali ya hewa ili kupunguza pengo katika mtandao wetu wa kitaifa wa uangazii wa hali ya hewa, kuendana na teknolojia za kisasa ikiwemo matumizi ya Akili Mnemba (AI) katika sekta utoaji wa huduma za hali ya hewa. Jitihada zote hizi zinafanywa kwa lengo la kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi leo na siku zijazo kama ilivyoainishwa katika kaulimbiu ya Siku ya Hali ya Hewa ya mwaka huu. Hivyo, uwekezaji huu katika utoaji wa huduma za hali ya hewa sio mzigo kwa walipa kodi, bali ni uwekezaji katika usalama wa kitaifa, uthabiti wa kiuchumi na ustahimilivu wa muda mrefu kwa taifa letu.
Aidha, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 (Dira 2050) iliyozinduliwa mwezi Julai mwaka jana, inatambua mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kama hatari kubwa kwa ukuaji wa uchumi wa muda mrefu, maisha ya watu, na usalama wa kitaifa, na inasisitiza haja ya kujenga ustahimilivu dhidi ya hali ya hewa hususan mabadiliko ya muda mrefu katika sekta zote. Kaulimbiu ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka huu inashabihiana vyema na Dira 20250 na inachangia katika utekelezaji wa nguzo tatu za Dira 2050, hasa nguzo ya tatu inayohusiana na Uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya hali ya hew ana tabianchi. Mojawapo ya malengo ya Nguzo hii ya tatu ni kujenga Taifa linaloweza kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na linaloweza kulinda watu, miundombinu na mali zake kutokana na majanga ya asili na yale yanayotokana na binadamu, huku vijana na wanawake wakiwekwa mstari wa mbele katika hatua za kukabiliana na mabadiliko haya ya hali ya hewa na tabianchi.
Vilevile, nguzo ya tatu ya Dira inatambua kuwa, mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, yanayoambatana na ongezeko la joto la dunia, mabadiliko ya mifumo ya hali ya hewa, na kuongezeka kwa matukio ya hali mbaya ya hewa, yanatishia maendeleo endelevu ya Tanzania. Na kuwa, athari zake ni kubwa kwa sekta zinazotegemea sana hali ya hewa, ambazo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania. Kwa kuzingatia haya, kuna haja ya hatua za maksudi kuimarisha uangazi na uchambuzi wa taarifa za hali ya hewa ili taarifa hizi zitumike katika utoaji wa maamuzi sahihi katika sekta mbalimbali kwa jamii kujengewa uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na hivyo kuwa na maendeleo endelevu.
Chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali imeendelea kuweka kipaumbele katika kuimarisha huduma za hali ya hewa na kuboresha utoaji wa huduma hizi kwa nchi nzima. Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa taarifa bora za hali ya hewa zinawafikia wananchi katika ngazi zote. Kama nilivyoainishwa hapo awali, uwekezaji mkubwa uliofanywa katika kuboresha miundombinu ya hali ya hewa, ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Uhakiki wa vifaa vya hali ya hewa kinacho endelea kujengwa jijini Dar es Salaam, utaboresha uwezo wetu wa ufuatiliaji na uangazi wa hali ya hewa na hivyo kuongeza usahihi wa taarifa za hali ya hewa. Huu ni uthibitisho wa dhati wa adhma ya Tanzania kuimarisha mifumo ya uangazi na ufuatiliaji wa hali ya hewa leo ili kesho yetu iwe salama zaidi kama kaulimbiu ya siku ya hali ya hewa Dunia kwa mwaka huu inavyosema.
Kupitia ushirikiano imara na mzuri na wadau wetu wa maendeleo, ikiwa ni pamoja na Shirika la Hali ya Hewa la Dunia (WMO), Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuimarisha mtandao wake wa uangazi na ufuatiliaji wa taarifa za hali ya hewa kupitia utekelezaji wa programu mbalimbali, ikiwemo programu ya WMO ya uwekezaji katika miundombinu ya hali ya hewa wa “Systematic Observing Financing Facility (SOFF)” na ile ya kuboresha mpango wa utoaji wa tahadhari za mapema kwa wote yaani “Early Warning for All (EW4ALL)”. Programu ya SOFF, inatoa mchango mkubwa kwa kuwekeza vituo tisa (9) vipya vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe "Automatic Weather Stations (AWS); vituo vine (4) vya uangazi wa hali ya hewa ya angani za juu "Upper-Air stations", pamoja na ukarabati na uboreshaji wa vituo 18 vya AWS na kituo kimoja (1) cha uangazi wa hali ya hewa ya anga za juu. Mipango mkakati hii ya Serikali inayochagizwa na mchango wa Wadau wetu wa Maendeleo itaongeza uwezo na ufanisi wa Mamlaka yetu ya Hali ya Hewa ya Tanzania (TMA), na kuifanya iendelee kutoa huduma zilizoboreshwa na kwa wakati.
Katika kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Dunia 2026, Serikali inapongeza kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Tanzania (TMA) kwa kuendelea kutoa huduma za hali ya hewa zilizoboreshwa, kwa wakati na kwa umakini mkubwa. Taarifa za TMA ni muhimu sana katika kuokoa maisha, kulinda mali na kusaidia sekta kuu za uchumi wan chi yetu. Napenda pia kutoa shukrani za dhati kwa Shirika la Hali ya Hewa la Dunia (WMO) na Washirika wa Maendeleo kwa mchango wao muhimu na mkubwa katika kuimarisha huduma za hali ya hewa nchini Tanzania, hasa katika kuboresha miundombinu ya uangazi na ufuatiliaji wa hali ya hewa na kujenga uwezo wa wataalamu. Ushirikiano wenu ni muhimu sana katika kuongeza ustahimilivu wetu kama Taifa dhidi ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.
Tunapoendelea kuadhimisha siku hii muhimu, natoa rai kwa wadau wote wakiwemo Taasisi za Serikali, Washirika wa Maendeleo, Sekta Binafsi, Taasisi za Elimu, Vyombo vya Habari na Umma kwa ujumla, kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwekeza kwenye mifumo na miundombinu ya uangazi na uchakataji wa taarifa za hali ya hewa nchini. Aidha, natoa wito kwa wadau wote kuendelea kutumia ipasavyo taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA na kuzingatia Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019.
Taarifa sahihi na za wakati za hali ya hewa ni nyenzo muhimu katika kufanya maamuzi ya kimkakati na kufanikisha maendeleo endelevu ya nchi yetu. Hivyo, tushirikiane kujenga Taifa lenye ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwa kuimarisha zaidi huduma za hali ya hewa, hususan miundombinu ya uangazi ambayo ndiyo msingi wa upatikanaji wa taarifa bora za hali ya hewa na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.
Tuendelee kuwekeza katika mifumo ya uangazi na ufuatiliaji wa hali ya hewa kwa wakati huu ili kulinda mustakabali wa nchi yetu pendwa na wananchi wake.
Nawatakia nyote maadhimisho yenye mafanikio na tija ya Siku ya Hali ya Hewa ya Mwaka 2026.
No comments:
Post a Comment