Saturday, December 14, 2024

MWENENDO WA KIMBUNGA “CHIDO” KATIKA BAHARI YA HINDI



Dar es Salaam, 14 Disemba, 2024:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa kuhusu mwenendo wa Kimbunga “CHIDO” katika Bahari ya Hindi.

Katika kipindi cha saa 24 zilizopita, Kimbunga “CHIDO kimeendelea kusalia katika eneo la Bahari kati ya Visiwa vya Comoro na kaskazini mwa Kisiwa cha Madagascar huku kikiendelea kuashiria kuelekea katika maeneo ya kaskazini mwa Msumbiji kikiwa katika kiwango cha Kimbunga Kikali (Intense Tropical cyclone) chenye kasi ya upepo unaofika kilomita 200 kwa saa. Kimbunga “CHIDO” kinatarajiwa kupita maeneo ya Visiwa vya Comoro siku ya leo na kuingia nchi kavu kaskazini mwa Msumbiji mnamo asubuhi ya kesho tarehe 15 Disemba 2024 kabla ya kuanza kupungua nguvu yake kuelekea tarehe 16 Disemba, 2024.

Kwa hapa nchini, kimbunga hicho bado hakiashirii uwezekano wa kusababisha athari za moja kwa moja. Hata hivyo, kutokana na ukaribu wa maeneo ambayo Kimbunga “CHIDO” kinatarajiwa kufika (kaskazini mwa Msumbiji) na maeneo ya kusini mwa nchi yetu, upo uwezekano mdogo wa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa katika maeneo ya Mikoa ya Mtwara na Ruvuma na maeneo jirani hususan kwa siku ya kesho tarehe 15 Disemba 2024.

Vilevile, upo uwezekano wa kutokea matukio ya upepo mkali wa bahari unaofika kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofika mita 2 katika maeneo ya mwambao wote wa pwani ya nchi yetu kwa siku ya kesho tarehe 15 Disemba, 2024.

USHAURI: Watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatalia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga “CHIDO” na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...