Dar es Salaam, 15 Disemba, 2024:
Taarifa hii inahitimisha mfululizo wa taarifa za mwenendo wa Kimbunga “CHIDO” zilizokuwa zikitolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) tangu tarehe 12 Disemba 2024. Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kuwa katika kipindi cha saa 6 zilizopita, Kimbunga “CHIDO” kimeingia nchi kavu katika eneo la kaskazini mwa Msumbiji na kimeanza kupoteza nguvu yake huku kikielekea kusini magharibi mbali zaidi ya nchi yetu.
Aidha, kutokana na ukaribu wa njia yake na maeneo ya hapa nchini, wakati Kimbunga ”CHIDO” kikiingia nchi kavu huko kaskazini mwa Msumbiji mnamo asubuhi ya leo tarehe 15 Disemba, 2024 kimeweza kusababisha vipindi vya mvua kwa mkoa wa Mtwara na maeneo jirani.
Hivyo, kwa sasa hakuna tena tishio la kimbunga “CHIDO” katika nchi yetu na hakuna madhara zaidi ya moja kwa moja yanayotarajiwa yakihusishwa na kimbunga hicho. Hata hivyo ikumbukwe kuwa, kwakuwa tupo ndani ya msimu wa mvua katika maeneo mengi hapa nchini, matukio ya mvua za kawaida za msimu yanatarajiwa kuendelea katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
USHAURI: Watumiaji wa taarifa za hali ya hewa na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.
No comments:
Post a Comment